KIKOSI cha Simba kinatarajiwa kuondoka nchini Ijumaa ya Machi 28 mwaka huu kwenda Misri kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, utakaopigwa Aprili 2, kwenye Uwanja wa New Suez Canal huku kukiwa na mtego ambao utaamua hatma yao.
Taratibu hizo zimeanza mapema kwa mabosi hao kuhakikisha kikosi hicho kinafika mapema ili kuzoea hali ya hewa, ikiwa ni baada tu ya kuisha kwa mchezo wa hatua ya 16 bora wa Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Bigman FC, utakaopigwa Machi 27.
Katika kuhakikisha wachezaji wanaendelea kujiweka fiti hasa kwa wale ambao hawako katika timu zao za taifa zinazopambana kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, Simba ilicheza mchezo wa kirafiki juzi na kuichapa KMC FC mabao 4-0.
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam, mabao ya Simba yalifungwa na Leonel Ateba aliyefunga mawili, huku Edwin Balua na Valentino Mashaka wakifunga bao moja kila mmoja.
Wakati Simba ikitarajia kuondoka nchini Machi 28, rekodi zinaibeba zaidi timu hiyo ya Msimbazi kutokana na uwiano mzuri wa kufunga mabao mengi na kujilinda vyema zaidi, ukilinganisha na wapinzani wao Al Masry.
Simba inayoshika nafasi ya pili kwa pointi zake 57, nyuma ya Yanga yenye 58, baada ya kucheza michezo 22, imeshinda 18, sare mitatu na kupoteza mmoja, imefunga mabao 52, ambapo kati yake 29 ni ya kipindi cha kwanza na 23 ni ya kipindi cha pili.
Kwa upande wa Al Masry iliyocheza michezo 18 ya Ligi Kuu ya Misri, inashika nafasi ya nne na pointi zake 31, baada ya kushinda minane, sare saba na kuchapwa mitatu, imefunga mabao 19, sawa na wastani wa kufunga bao moja kwa kila mchezo.
Katika mabao hayo 19, tisa imeyafunga kipindi cha kwanza na 10 kipindi cha pili, huku eneo la ulinzi likiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 11, ikionyesha wazi safu ya uzuiaji sio nzuri tofauti na Simba iliyoruhusu manane.
Simba iliyomaliza kinara wa kundi A na pointi 13, imepangwa kucheza na Al Masry iliyomaliza nafasi ya pili kundi D na pointi tisa, nyuma ya wapinzani wao kutoka Misri, Zamalek ambao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo msimu wa 2023-2024.
Wakati kwenye ligi zao hali ikiwa hivyo, upande wa mechi za kimataifa kuanzia hatua ya makundi ambapo kila timu ilicheza mechi sita, mabao yao ya kufunga na kufungwa yameonekana kugawanyika huku Simba ikiyagawa vizuri kulinganisha na wapinzani wao.
Katika michezo sita ya hatua ya makundi ambayo Simba imecheza, imeshinda minne, sare mmoja na kutoa pia sare mmoja, ikifunga mabao manane huku manne kipindi cha kwanza na mengine cha pili, pia imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne ikiwa mawili kipindi cha kwanza na mawili cha pili.
Kwa upande wa Al Masry katika michezo sita ya hatua ya makundi, imeshinda miwili, sare mitatu na kupoteza mmoja, huku ikifunga mabao saba, kati ya hayo sita kipindi cha kwanza na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne ambayo yote kipindi cha pili.
Kitendo cha Al Masry kumaliza nafasi ya pili huku Simba ikimaliza ya kwanza, kimezifanya timu hizo kukutana tena ambapo pambano hilo la Aprili 2, litakuwa ni la tatu kwao kukutana kwa miaka ya hivi karibuni baada ya kutokea pia mwaka 2018.
Timu hizo zilikutana raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo mechi ya jijini Dar es Salaam zilitoka sare ya mabao 2-2, Machi 7, 2018, kisha marudiano Misri zikatoka suluhu (0-0), Machi 17, 2018, na Simba kutolewa kwa mabao ya ugenini.
Refa wa kati atakayechezesha pambano hilo ni Boubou Traore kutoka Mali, huku rekodi zikionyesha amechezesha michezo 25 ya kimataifa, ambapo kwa timu mwenyeji imeshinda 17, sare miwili huku zile za ugenini zikiambulia ushindi mara sita tu.
Mwamuzi huyo ndiye aliyechezesha mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati ya Yanga iliyoifumua CR Belouizdad ya Algeria mabao 4-0, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Februari 24, 2024 na kutinga robo fainali kibabe.
Simba imetinga hatua ya robo fainali kwa msimu wa sita kati ya saba katika ushiriki wa michuano ya CAF tangu mwaka 2018, zikiwemo mbili ya Shirikisho Afrika na nne Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikiwa kinara wa kundi kwa mara yake ya pili.
Mara ya kwanza Simba kuongoza kundi tangu kipindi hicho ilikuwa msimu wa 2020-21, iliposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikimaliza kundi A na pointi 13, ikifuatiwa na Al Ahly ya Misri iliyomaliza ya pili na pointi 11.
AS Vita Club ya DR Congo ilimaliza ya tatu na pointi saba, huku Al Merrikh ya Sudan ikiburuza mkiani na pointi mbili tu. Simba iliishia robo fainali baada ya kutolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-3.