Mwanza. Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) imepokea kontena tisa zenye samani za viti vitakavyowekwa ndani ya Meli ya MV Mwanza inayojengwa katika Bandari ya Mwanza Kusini jijini hapa.
Hafla ya kupokea kontena zenye viti hivyo imefanyika leo Jumatatu Machi 24, 2025, inapojengwa meli hiyo na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Mradi wa Ujenzi wa MV Mwanza unajengwa na mkandarasi wa Kampuni ya Gas Entec Ship-Building Engineering ya Nchini Korea kwa gharama ya zaidi ya Sh124 bilioni.
Ujenzi wa meli hiyo itakayokuwa kubwa zaidi ndani ya Ziwa Victoria ikifanya safari zake kati ya Bandari ya Mwanza Kaskazini, Kemondo, Kenya na Uganda, umefikia asilimia 96 huku ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na magari makubwa 3.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Tashico, Eric Hamissi, Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Amina Ntibampema amesema mradi huo unatarajia kukamilika ifikapo Mei 31, mwaka huu huku ukitarajiwa kuchochea uchumi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
“Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuongeza chachu kwa ukuaji wa uchumi kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na nchi jirani kwa kutoa huduma za usafiri zilizo salama, bora na za uhakika,” amesema Ntibampema.

Wafanyakazi wa Kampuni ya Meli Tanzania wakiwa wanabeba samani za viti kuviingiza ndani ya Meli ya MV Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira.
Ntibampema amesema hadi sasa mkandarasi ameshalipwa Sh115.9 bilioni sawa na asilimia 93.5 ya gharama zote za mradi huo.
Amesema samani nyingine, ikiwemo vitanda zitaendelea kutengenezwa na kupachikwa ndani ya meli hiyo kabla ya muda wa mradi kukamilika, ili kuruhusu mamlaka nyingine za ukaguzi wa vyombo vinavyofanya shughuli zake majini kutimiza wajibu wao.
Kwa upande wake, meneja wa mradi wa ujenzi wa meli hiyo, Kanali Vitus Mapunda amesema baada ya kukamilika kusimika samani hizo, Tashico itatakiwa kusubiri kibali kutoka kwenye mamlaka za ukaguzi.
“Baada ya Mei 31 kutakuwa na jukumu kubwa la Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) wakifanya kazi yao kisha kuipitisha meli hiyo kuanza kufanya safari zake. Huo ndiyo utaratibu unaotumika hivyo siyo kwamba ikishakamilika basi inaanza kazi hapohapo,” amesema Kanali Mapunda.
Mkataba wa ujenzi wa meli ya MV Mwanza ulisainiwa mwaka 2019 na ujenzi wake kuanza rasmi 2020, ukitarajiwa kukamilika baada ya miezi 24, hata hivyo kutokana na changamoto zilizojitokeza ujenzi wake ulichelewa.
“Hapo katikati mradi huu ulisuasua kidogo kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi duniani likiwemo janga la Uviko-19, hali iliyoathiri usafirishaji mizigo duniani kote lakini pia baadhi ya nchi kufunga mipaka.”

Wafanyakazi wa Kampuni ya Meli Tanzania wakiwa wanabeba samani za viti kuviingiza ndani ya Meli ya MV Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira.
“Hali hii ilisababisha pia kupanda kwa bei ya baadhi ya bidhaa ikiwemo makasha ya kusafirishia vifaa baada ya janga la Uviko-19 tunaishukuru Serikali ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kuhuishwa upya kwa gharama za mradi huu ambao awali ulikuwa na thamani ya Sh94 bilioni lakini hadi hii leo utakamilika kwa thamani ya Sh124 bilioni,” amesema.
Machi 2024, Kampuni ya Gas Entec Ship-Building Engineering ya nchini Korea iliifanyia majaribio ya kuiendesha meli hiyo kwa kasi kwa siku tatu mfululizo kwenye maji ili kuona ufanisi wake, ambapo jaribio hilo lilifanikiwa kwa asilimia 100.
Akizungumza na Mwananchi, Mkazi wa Luchelele, Oseah John amesema kiu yake ni kuona Serikali ikitangaza kuanza safari rasmi za meli hiyo, kwa kile alichodai umepita muda mrefu tangu ujenzi wake uanze.
“Mkataba wa ujenzi wa meli hii uliposainiwa niliushuhudia, lakini hadi leo tunapopita barabarani kwenda Buhongwa tunaona ipo imeegeshwa tu hapo bandarini. Matamanio ya wengi ni kuona inafanya kazi siyo ikiwa imeegeshwa tu hapo,” amesema John.
Salima Abdul amesema anaamini kukamilika kwake kutaongeza wigo na fursa kwa wajasiriamali wadogo ‘kupiga’ pesa na kukuza uchumi wao kutokana na kuongezeka mzunguko wa fedha utakaochochewa na bidhaa zinazosafirishwa kwa kutumia meli hiyo