VIDEO: Singida BS yaingia anga za Bayern Munich kisa mashabiki

MTENDAJI Mkuu wa Singida Black Stars, Jonathan Kasano, amefichua kuwa kuanzia msimu ujao, jezi namba 12 haitavaliwa na mchezaji yeyote kwenye kikosi cha timu hiyo, badala yake itakuwa maalum kwa heshima ya mashabiki wao.  

Kasano alitoa kauli hiyo leo, Jumatatu, wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la klabu hiyo katika eneo la Mtipa, ambalo sasa ni maskani rasmi ya Singida Black Stars baada ya kuhamia huko kufuatia ujenzi wa uwanja wao mpya.  

Uwanja huo una uwezo wa kuchukua mashabiki kati ya 5,000 hadi 7,000, na klabu hiyo imeweka mkakati wa kuwa na jukwaa maalum kwa mashabiki wake kama sehemu ya kuthamini mchango wao kwa timu hiyo.

“Kuanzia msimu ujao, jezi namba 12 itakuwa maalum kwa mashabiki wetu. Tunatambua na kuthamini mchango wao katika mafanikio ya timu, na hii ni njia yetu ya kuwaonyesha kwamba wao ni sehemu muhimu ya Singida Black Stars,” alisema Kasano.  

Katika hafla hiyo, Kasano alifuatana na viongozi wengine wa klabu akiwamo Makamu Mwenyekiti wa timu, Omary Kaaya, ambaye alisisitiza kuwa mashabiki ni nguzo muhimu katika safari ya mafanikio ya timu.

“Timu haiwezi kufanikiwa bila mashabiki. Uamuzi huu unalenga kuwaweka karibu zaidi na klabu yao. Tunataka wajihisi kuwa sehemu ya timu si kwa maneno tu, bali kwa vitendo,” alisema.

Katika uzinduzi huo, pia ulitangazwa rasmi uongozi wa tawi hilo la Mtipa lenye wanachama 100, ambapo Omary Ramadhani aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa tawi, huku Jumanne Ivanga Wawa akichukua nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Lameck Masense Yohana akiteuliwa kuwa katibu.  

Mashabiki waliohudhuria hafla hiyo walipokea tangazo hilo kwa shangwe na nderemo, wakisema kuwa hatua hiyo inaonyesha namna klabu yao inavyowajali na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya timu.  

“Hii ni historia kwa Singida Black Stars. Hatukuwahi kufikiria kwamba klabu ingefanya uamuzi wa kututambua kwa namna hii. Sasa tunajiona kama sehemu halisi ya timu,” alisema Emmanuel Msangi, mmoja wa mashabiki waliohudhuria.

Jezi namba 12 ambayo haitatumiwa na mchezaji yeyote kuanzia msimu ujao, msimu huu inavaliwa na Amas Obasogie.

Hatua hii ya Singida Black Stars inaendana na utamaduni wa baadhi ya klabu kubwa duniani ambazo hutunza jezi fulani kwa heshima ya wachezaji au mashabiki wao.

Mfano mzuri ni Bayern Munich. Ingawa hawakutunza rasmi jezi namba 12, miamba hao wa soka la Ujerumani wanaheshimu mashabiki wao kama “mchezaji wa 12” na mara kwa mara wamekuwa wakitumia namba hiyo katika matangazo ya klabu.

Related Posts