Na: Calvin Gwabara – Mvomero
Wakulima wa mahindi Wilayani
Mvomero Mkoani Morogoro wameiomba Serikali kupitia watafiti wake kutafuta
suluhisho la kudumu la namna ya kuwakabili viwavi jeshi vamizi ambao wanaharibu
zao la mahindi na kuziacha familia nyingi na njaa na umasikini mkubwa.
Mkulima wa mahindi kutoka kata ya Wami Dakawa wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, Salehe Mwendi akizungumza na watafiti wa mradi wa AGRISPARK – SUA. |
Wakiongea na watafiti wa mradi wa
AGRISPARK – SUA wilayani humo wamesema kila mwaka hali inakuwa mbaya zaidi
kutokana na kushindwa kuwadhibiti wadudu hao hatari ambao sasa wanashambulia na
mazao mengine yote ya kijani pale mahindi yanapokauka shambani.
Akizungumza kwenye kikao hicho
kuwakilisha wakulima wengine Mkulima wa mahindi kutoka kata ya Wami Dakawa
wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, Salehe Mwendi amesema kwa sasa kilimo
kimekuwa kigumu na changamoto za wadudu na ukame vinatuacha masikini wakulima
wengi kwenye maeneo mengi.
“Jamani tunaiomba serikali
kupitia watafiti wake na mamlaka zingine zenye uwezo wa kusaidia kupata
ufumbuzi wa wadudu hawa, miaka ya nyuma tulizoea ukilima mahindi unasubiria
kuvuna lakini kwa sasa hali imekuwa mbaya sana bila kupuliza madawa hupati
chochote shambani, tunatumia nguvu kubwa kulima lakini wadudu wanatunyima mazao
yetu hasa kwa sisi ambao hatuna uwezo wa kununua madawa” alisema Mzee Mwendi.
Aliongeza “Kwa sasa tunalima
shamba tunapanda na kuhudumia kwa kupalilia kisha tunaacha wadudu wale na kile
watakachobakisha shambani ndicho na sisi mwisho tunaenda kuokoteza na kurudisha
nyumbani kula na familia yetu, maana tulikimbilia kwenye zao la mpunga ambalo
nalo haliathiriwi na wadudu hawa lakini sasa kwa miaka mitatu mfululizo ndege
wanakuja makundi kama mchanga wakishuka shambani siku moja wanamaliza hata
ekari 12, yani tunateseka sana”.
Nae Mkulima mwingine Mzee Mohamed
Kigonile ameomba watafiti wa Mradi wa AGRISPARK – SUA kuwa kama kuna elimu
sahihi ya kukabiliana na wadudu hao basi waandike vitabu na vipeperushi
vinavyoweza kutoa maelekezo sahihi ya namna ya kufanya ili kuokoa mazao yao.
![]() |
Mkulima wa Mahindi wilayani Mvomero Mzee Mohamed Kigonile akizungumza na watafiti wa mradi wa AGRISPARK shambani kwake Wami Dakawa. |
“Tunajua nyinyi watafiti kutoka
kwenye Chuo chetu kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) mnafanya kazi nzuri na
tafiti nzuri kutusaidia wakulima tuzalishe kwa tija, sasa tusaidieni kama kuna
tafiti mlizofanya kuhusu wadudu hawa mtuletee tujifunze ili zitusaidie
kuwatokomeza maana kwa uwezo wetu sisi tumefika mwisho tunahitaji msaada wenu
na serikali mtuokoe njaa itatumaliza” alieleza Mzee Kigonile.
Akizungumzia tatizo hilo Mtafiti
mkuu mwenza wa mradi wa AGRISPARK kutoka SUA Dkt. Nicholaus Mwalukasa
amewaambia kuwa amepokea maombi yao hivyo wanakwenda kutafuta machapisho ya
kisayansi mbalimbali ambayo yamefanyika kuhusu namna ya kupambana na wadudu hao
na wakiyapata wataandika vitabu vidogo ambayo vitaelezea na kufundisha namna ya
kuwadhibiti wadudu hao.
“Tulipokuwa kwenye kata ya
Nyandira pia wakulima wametoa kilio hichocho kwa wadudu hao katika zao la
mahindi hivyo sisi kama watafiti tunalichukua na kwenda kulifanyia kazi maana
tunamini zitakuwepo tafiti ambazo zimefanyika na kuchapishwa kwenye majarida ya
kisayansi ya kimataifa ambayo sio rahisi nyinyi kuyafikia lakini sisi tutafanya
hivyo kwa niaba yenu na kuwaletea kwa lugha rahisi ili muweze kuelewa”
alifafanua Dkt. Mwalukasa.
Watafiti hao wa mradi wa AGRISPARK kutoka SUA
wametembelea wakulima kwenye wilaya ya Mvomero, Morogoro Manispaa na
Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Vijijini na kukutana na wakulima na kuungumza
nao kuhusu mahitaji yao ya elimu kwenye shughuli za kilimo na changamoto
zinazowakabili ili wweze kuwatafutia ufumbuzi wa changamoto zao kwa kuandaa
vitabu vidogo vya kuwaelimisha kuhusu mahitaji yao.
Mradi wa AGRISPARK unafadhiliwa na Serikali ya jamahuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kama maono
mapana ya uongozi wa chuo wa kutenga fedha za ndani kwaajili ya kuwawezesha
watafiti wake kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
![]() |
Kiwavijeshi vamizi akiwa kwenye mmea wa mhindi shambani akishambulia mazao. |