Dar es Salaam. Vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) vimepungua kutoka 56,000 mwaka 2015 hadi 18,400 mwaka 2024, hii ikiwa ni sawa na punguzo la asilimia 68.
Katika mgawanyo kitakwimu, ugonjwa wa kifua kikuu huua watu 1,500 kila mwezi nchini, kutoka watu 4,332 mwaka 2015.
Kiwango hicho kimesababisha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 13 duniani zilizo katika hatua sahihi kuelekea kufikia lengo la dunia la kutokomeza kifua kikuu ifikapo 2030.
Hatua hizi zimetajwa kuchangiwa na jitihada kubwa zilizochukuliwa katika kuongeza wigo wa mtandao wa huduma za uchunguzi na upimaji kifua kikuu, ushirikishwaji wa jamii na upatikanaji madhubuti wa dawa na vifaatiba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa mawasiliano na uhamasishaji kutoka Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma, Wizara ya Afya, Juma Said imeeleza kuwa nchi imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo na maambukizi mapya.
“Maambukizi mapya ya ugonjwa wa kifua kikuu yamepungua kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mnamo 2015, hadi wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000 kwa mwaka 2024, ikiwa ni sawa na punguzo la asilimia 40.
“Pia vifo vitokanavyo na ugonjwa wa kifua kikuu vimepungua kutoka 56,000 mwaka 2015 hadi vifo 18,400 mwaka 2024, hii ikiwa ni sawa na punguzo la asilimia 68,” amesema Juma.
Amesema takwimu hizo zinatoa matumaini ya kufikia lengo la kutokomeza kifua kikuu ifikapo 2030. Hata hivyo lengo hili linaweza lisifikiwe kama nchi haitawekeza katika kutatua changamoto zinazorudisha nyuma jitihada zinazoendelea sasa.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu dalili za ugonjwa wa kifua kikuu, unaosababisha watu kuchelewa kuchukua hatua mapema na hivyo kuendeleza mnyororo wa maambukizi katika jamii.
Ametaja kushindwa kuyafikia makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuugua ugonjwa huo kama vile wachimbaji wadogo wa madini, wavuvi, wafungwa na mahabusu, waishio katika makazi holela na wengine.
Pia ametaja ushiriki finyu wa sekta binafsi katika kusaidia jitihada za kutokomeza kifua kikuu nchini, mathalan kati ya vituo binafsi 3,000 vya kutolea huduma za afya vilivyopo, ni asilimia 16 pekee ndio vinashiriki kutoa huduma za kifua kikuu.

Juma amesema katika kukabiliana na changamoto hizo na nyingine, Wizara, kwa kushirikiana na wadau, kwa kipindi cha kuanzia Desemba 2024 hadi Machi 2025, inaendesha kampeni maalumu katika halmashauri 76 zilizopo katika mikoa 9 nchini.
“Kampeni hii inalenga kuchochea kasi ya kuibua wagonjwa na kuwaweka katika matibabu, hususan makundi yaliyo katika hatari ya kuugua kifua kikuu na pia kuongeza ufahamu juu ya ugonjwa huu katika jamii. Hadi sasa matokeo ya awali yanaonesha kuwepo kwa mafanikio katika kampeni hii,” amesema.
Amefafanua kuwa kupitia kampeni hiyo, mpaka sasa, jumla ya wagonjwa 9,585 wa kifua kikuu wameibuliwa na kuwekwa kwenye matibabu, ikiwa ni sawa na asilimia 66 ya lengo la kampeni la kuibua wagonjwa 14,471.
Pia amesema, wagonjwa wa kifua kikuu sugu 36 wamebainika na kuwekwa katika matibabu.
“Pili, kuongeza hamasa na utashi juu ya ugonjwa wa kifua kikuu katika ngazi ya mikoa na halmashauri, kampeni hii ilizinduliwa Kitaifa, lakini pia kila mkoa nao uliweza kufanya mkutano mkubwa wa wadau ulioratibiwa na ofisi ya mkuu wa mkoa husika,” amesema.
Kidunia, siku hii hutumika kuchagiza hamasa na elimu kwa jamii ili kuufahamu zaidi ugonjwa wa kifua kikuu, hususan njia za kujikinga, kukumbusha kuhusu wajibu wao katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kwa mwaka huu, kauli mbiu ya siku ya kifua kikuu duniani, inasema, “kwa pamoja tunaweza kutokomeza kifua kikuu: azimia, wekeza, timiza.”
Kauli mbiu hii imejikita katika kuhamasisha jamii na wadau wote juu ya wajibu wao katika kuchochea jitihada za kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu nchini. Pia inahimiza azma ya pamoja katika kuchangia rasilimali muhimu za kuwezesha mapambano hayo.