AU YAPONGEZA MCHANGO WA TANZANIA KATIKA KULETA AMANI NA USALAMA BARANI AFRIKA


• Naibu Waziri Chumi ataja masuala sita muhimu kufika Afrika yenye amani na usalama wa kudumu

Umoja
wa Afrika (AU) umeipongeza Tanzania kwa mchango wake wa kipekee wa
kuleta amani na usalama wa kudumu katika maeneo mbalimbali barani
Afrika.  

Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 25, 2025 kwenye
ufunguzi wa mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama  Umoja wa
Afrika – African Union Peace and Security Council (AU-PSC) uliofanyika
jijini Arusha.

Akitoa pongezi hizo Kamishina wa Masuala ya
Siasa, Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika Mhe. Balozi Bankole Adeoye
kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja huo Mhe. Azali Assoumani,
ameeleza kuwa siku zote Tanzania imekuwa mstari wa mbele, ikijitoa kwa
hali na mali katika kuongoza juhudi za kuleta amani na usalama barani
Afrika.

Aliongeza kusema kuwa mchango huo unatokana na sera
madhubuti na misingi imara iliyowekwa na Mwasisi wa Taifa la Tanzania
Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kuendelea kusimamiwa kwa ufanisi
na uongozi mahiri wa sasa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.  

Tuko hapa jijini Arusha leo sio
kwa bahati mbaya, hii ni ishara ya kutambua na kupongeza rekodi ya
kipekee ya Tanzania katika kuleta amani na usalama barani Afrika. Sote
tunatambua tokea zama za kupigania uhuru, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa
Mataifa mengi na ilitoa mchango wake wa hali na mali kuhakikisha mataifa
mengine ya Afrika yakuwa huru. Juhudi hizo hazikuishia hapo, hadi leo
Tanzania imeendelea kuwa kinara katika utatuzi wa migogoro sehemu
mbalimbali ili kuhakikisha Waafrika wanafurahia matunda ya uhuru wao.
Alisema  Balozi Adeoye.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato David Chumi
akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Waziri Mhe. Balozi Mahmoud Thabit
Kombo amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono bila kuyumba
katika kutekeleza mipango ya Baraza la Amani na Usalama la AU  kwenye
kutimiza malengo ya agenda 2063  kuhusu Afrika yenye maendeleo endelevu.

Tanzania tumekuwa taifa ambalo mara kwa mara tanatetea “Amani
na Umoja,”  dhana ambayo inaonesha na kudhibitisha kujitoa kwetu katika
kujenga, kulinda na kutetea misingi ya kutafuta amani na usalama wa
kudumu barani Afrika bila kuchoka. Kiongozi wetu Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassa ameendelea kuhimiza na
kutekeleza hayo kwa vitendo.  Alieleza Mhe. Chumi

Mbali na hayo
Naibu Waziri Chumi amependekeza masuala sita muhimu ya kuzingatiwa na
PSC ili kufikia Afrika yenye amani na utulivu wa kudumu. Masuala ni;
umoja na mshikamano katika kuteleza majukumu, kuepuka kutoa kipaumbele
kwa maslahi binafsi na utoaji wa michango ya fedha kwa wakati,

Masuala
mengine muhimu ni; kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya
Umoja wa Afrika na taasisi zingine za kikanda na kimataifa, utekelezaji
mzuri wa makubaliano ya Amani yanayofikiwa na mwisho kuhakikisha
ushirikishwaji wa makundi maalumu katika juhudi za kutafua amani na
usalama wakiwemo vijana na wanawake.

Mafunzo hayo ya Wajumbe wa
Baraza la Amani na Usalama la AU yalianza  Machi 23, 2025 na
yanatarajiwa kufikia tamati Machi 27, 2025 yakilenga kuwajengea uwezo
wajumbe hao kuhusu masuala mbalimbali muhimu ya kuwawezesha kutekeleza
majukumu ya baraza hilo kwa ufanisi.  Mafunzo najumuisha wajumbe wapya
walioteuliwa hivi karibuni, pamoja na wengine kumi ambao wameendelea
kutetea nafasi zao katika Baraza la Amani na Usalama la AU.

Aidha,
Tanzania, ambayo imetumikia kama mwanachama wa Baraza la Amani na
Usalama kwa kipindi cha miaka miwili, katika mafunzo hayo inawakilishwa
na Ujumbe wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa
Afrika ambao unaongozwa na   Mhe. Balozi Innocent Shiyo

Mafunzo
hayo yanalenga kuwajengea uwezo wajumbe hao, hasa wale walioteuliwa hivi
karibuni kuhusu masuala mbalimbali muhimu ya kuwawezesha kutekeleza
majukumu ya baraza hilo kwa ufanisi na tija zaidi ikiwemo kuelewa
misingi na mamlaka ya PSC, kazi zake, mbinu za kufanya kazi na
kushirikiana na Tume nzima ya AU na wadau wengine wa kikanda na
kimataifa ikiwemo Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Mataifa.

Baraza
la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU-PSC) liliundwa mwaka 2004
kupitia Itifaki ya kuanzishwa kwa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa
Afrika. AU-PSC linawajibika kuzuia, kusimamia, na kutatua migogoro
katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika. Programu hii ya mafunzo
itajumuisha shughuli mbalimbali zitakazoongozwa na wanadiplomasia wakuu,
wataalamu wa sera, na maafisa wa AU kwa lengo la kuwawezesha wajumbe
kuelewa masuala muhimu ya PSC ikiwemo kuhusu muundo, majukumu na juhudi
zinazofanyika ili kuleta amani na usalama endelevu barani Afrika.

Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato
David Chumi akifungua mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama  Umoja wa Afrika – African Union Peace and Security Council (AU-PSC) yanayoendelea jijini Arusha. Machi 25, 2025.


Mwakilishi
wa Kudumu wa Ufalme wa Morocco katika Umoja wa Afrika na Mwenyekiti wa
Baraza la Amani na Usalama kwa mwezi Machi 2025 Mhe. Balozi Mohamed
Arrouchi kwenye ufunguziwa 
mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama  Umoja wa Afrika – African Union Peace and Security Council (AU-PSC) yanayoendelea jijini Arusha Machi 25, 2025

Mwakilishi
wa Kudumu wa Ufalme wa Morocco katika Umoja wa Afrika na Mwenyekiti wa
Baraza la Amani na Usalama kwa mwezi Machi 2025 Mhe. Balozi Mohamed
Arrouchi kwenye ufunguziwa 
mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama  Umoja wa Afrika – African Union Peace and Security Council (AU-PSC) yanayoendelea jijini Arusha Machi 25, 2025



 

Related Posts