Benki ya NBC Yashiriki Uzinduzi Uwanja Mpya Wa Singida Blakc Stars, Yasisitiza nia Kuboresha Viwanja.

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) , mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya NBC imeshiriki kikamilifu kwenye uzinduzi wa uwanja mpya wa Airtel Stadium wa klabu ya soka ya Singida Black Stars uliopo mkoani Singida, huku ikielezea nia yake kuwekeza zaidi kwenye maboresho ya viwanja vinavyotumiwa na vilabu mbalimbali nchini vinavyoshiriki ligi hiyo. Benki hiyo ni moja ya wadhamini muhimu waliofanikisha ujenzi wa Uwanja huo mpya kupitia msaada wake wa fedha kiasi cha sh milioni 50.

Katika uzinduzi huo ulioongozwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw, Hamis Mwinjuma, benki ya NBC iliwakilishwa na Mkurugenzi wake wa Biashara Bw, Elvis Ndunguru, Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Umma na Mawasiliano Bw Godwin Semunyu, Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Biashara ambae ndio Mwenyekiti wa kamati ya Ligi hiyo ndani ya NBC Bw Joseph Lyuba pamoja na maofisa wengine wa benki hiyo tawi la Singida.

Katika hotuba yake Naibu Waziri Mwinjuma pamoja na kuipongeza klabu ya Singida Black Stars kwa hatua hiyo, aliwashukuru wadau waliyoiunga mkono klabu hiyo ikiwemo benki ya NBC aliyoitaja kama mdau muhimu zaidi katika ukuaji wa sekta ya michezo nchini ikiwemo mpira wa miguu.

“Uzinduzi wa uwanja huu wa Singida Black Stars ni muelekeo sahihi kuelekea mageuzi kwenye sekta yetu ya michezo hususani mpira wa miguu na ninapongeza sana kwa hilo. Nimefurahi kuona uwepo wa Benki ya NBC kwenye hatua hii na huu ni mwendelezo tu wa jitihada zao kwenye maendeleo ya michezo hapa nchini…hongereni sana NBC tunawashukuru kwa hilo’’ alisema.

Akizungumzia mkakati wa uboreshaji wa miundombinu ya viwanja, Bw Ndunguru alisema unakwenda sambamba na mikakati mingine ya benki hiyo katika kuboresha ligi hiyo ikiwemo utoaji wa mikopo ya usafiri kwa vilabu, utoaji wa huduma za bima ya afya kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi, usajili wa kadi za wanachama na utoaji wa elimu ya fedha kwa vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo.

“Suala la uboreshaji wa viwanja kwasasa tunaliona kama agenda muhimu zaidi katika udhamini wetu kwenye ligi hii. Tumeshafanya jitihada kadhaa kwenye eneo hilo na sasa tunaona wazi kabisa kwamba tunahitaji kuwekeza nguvu zaidi kwenye eneo hilo. Mbali na uwanja huu ambapo tuliwekeza kiasi cha sh milioni 50 tumeshasaidia viwanja vingine kwenye maboresho madogo madogo ukiwemo Uwanja wa Jamhuri Dodoma ambapo kupitia tawi letu la huko tulisaidia maboresho kwenye mfumo wa umwagiliaji wa uwanja,’’ alisema Ndunguru.

Pamoja na maboresho ya viwanja, Ngunguru pia alivisisitiza vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo kuwekeza nguvu zaidi kwenye suala zima la utoaji wa kadi za kielectroniki kwa wanachama wake, hatua ambayo alisema itavisaidia vilabu hivyo kujiongezea mapato na kutunza taarifa sahihi za wananchama wao.

Akizungumzia mikakati ya kamati ya benki hiyo, Bw Lyuba alisema kamati yake imejizatiti zaidi kuhakikisha inaendelea kuboresha na kulinda hadhi ya ligi hiyo huku akionyesha kuridhishwa kwa kiasi kikubwa na mwenendo wa ligi hiyo hususani kwenye eneo la ushindani baina ya vilabu, muitikio wa mashabiki na hali ya kiuchumi miongoni mwa vilabu husika hali ambayo imeviwezesha vilabu hivyo kuweza kusajili wachezaji wenye viwango bora zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.

Naye Bw Semunyu pamoja na mambo mengine alionesha kuguswa na ushirikiano baina ya wadau mbalimbali wa ligi hiyo ikiwemo serikali, vilabu, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), wadau wa Habari na mashabiki jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaiwezesha benki hiyo kama mdhamini mkuu kutimiza wajibu wake kwa ufasaha na kuiongezea hari ya kuendelea kuboresha zaidi udhamini wake.

“Tunapoona muitikio mkubwa kutoka kwa kila mdau ikiwemo vilabu vinahamasika kufanya uwekezaji muhimu kama huu uliofanywa na Singida Black Stars na vilabu vingine, kiasi cha kuvutia ushiriki wa wadau wengine tunafarijika zaidi na tunaamini tupo na wadau sahihi zaidi. Ushiriki wa viongozi wa serikali kwenye matukio kama haya nayo ni hamasa nyingine ya ziada kabisa.Naamini tunapoelekea ni kuzuri zaidi,’’ alisema Semunyu huku akiipongeza klabu ya Singida Black Stars kwa hatua hiyo.

Hafla ya uzinduzi wa Uwanja huo wa Airtel Stadium ilipambwa na mechi ya kirafiki kati ya mwenyeji Singida Black Stars dhidi ya Yanga SC mechi ambayo hata hivyo ililazimika kuhairishwa katikati ya kipindi cha pili huku matokeo yakiwa ni 1 – 1 kutokana na hali ya mvua kuzidi.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw, Hamis Mwinjuma (katikati) akikata utepe kushiria uzinduzi wa Uwanja mpya wa Airtel Stadium unaomilikiwa na klabu ya Singida Blacks Stars ya mkoani Singida wakati wa hafla ya uzinduzi wa uwanja huo iliyofanyika jana mkoani humo. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkurugenzi wa Biashara wa benki ya NBC Bw, Elvis Ndunguru (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa TEHAMA wa kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Bw Frank Filmany (wa pili kulia) Mwenyekiti wa Klabu ya Singida Black Stars Bw Ibrahim Mirambo (kulia) na Mjumbe wa Bodi ya klabu hiyo Bw Festo Sanga.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw, Hamis Mwinjuma (wa pili kulia) sambamba na wadau wengine wa mchezo wa mpira wa miguu na viongozi wa serikali wakikagua ubora wa uwanja mpya wa Airtel Stadium unaomilikiwa na klabu ya Singida Blacks Stars ya mkoani Singida wakati wa hafla ya uzinduzi wa uwanja huo iliyofanyika jana mkoani humo jana. Wengine ni pamoja na Mkurugenzi wa Biashara wa benki ya NBC Bw, Elvis Ndunguru (kushoto mstari wa mbele), Mkurugenzi wa TEHAMA wa kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Bw Frank Filmany (wa pili kushoto – mstari wa mbele) Mwenyekiti wa Klabu ya Singida Black Stars Bw Ibrahim Mirambo (wa tatu kushoto – ,mstari wa mbele) na Mjumbe wa Bodi ya klabu hiyo Bw Festo Sanga (Kulia)

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw, Hamis Mwinjuma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wachezaji wa Singida Black Stars sambamba na wadau wengine wa mchezo wa mpira wa miguu na viongozi wa serikali wakati wa hafla ya uzinduzi wa uwanja mpya wa Airtel Stadium unaomilikiwa na klabu ya Singida Blacks Stars ya mkoani Singida iliyofanyika jana mkoani humo jana.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw, Hamis Mwinjuma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wachezaji wa Yanga SC sambamba na wadau wengine wa mchezo wa mpira wa miguu na viongozi wa serikali wakati wa hafla ya uzinduzi wa uwanja mpya wa Airtel Stadium unaomilikiwa na klabu ya Singida Blacks Stars ya mkoani Singida iliyofanyika jana mkoani humo jana.

Muonekano wa Uwanja mpya wa Airtel Stadium unaomilikiwa na klabu ya Singida Blacks Stars ya mkoani Singida.

Mkurugenzi wa Biashara wa benki ya NBC Bw, Elvis Ndunguru (kushoto) akijadili jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) Steven Mnguto (katikati) na Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Bw Jackson Mbando (kulia) wakati wa hafla ya uzinduzi wa uwanja mpya wa Airtel Stadium unaomilikiwa na klabu ya Singida Blacks Stars ya mkoani Singida iliyofanyika jana mkoani humo jana

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw, Hamis Mwinjuma (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Umma na Mawasiliano Bw Godwin Semunyu wakati wa hafla ya uzinduzi wa uwanja mpya wa Airtel Stadium unaomilikiwa na klabu ya Singida Blacks Stars ya mkoani Singida iliyofanyika jana mkoani humo jana. Kushoto ni Mwenyekiti wa kamati ya Ligi hiyo ndani ya NBC Bw Joseph Lyuba.

Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Biashara wa Benki ya NBC ambae ndio Mwenyekiti wa kamati ya ligi ndani ya NBC Bw Joseph Lyuba (wa pili kushoto) na Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Umma na Mawasiliano Bw Godwin Semunyu (wa tatu kushoto) pamoja na maofisa wengine wa benki hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa hafla ya uzinduzi wa uwanja mpya wa Airtel Stadium unaomilikiwa na klabu ya Singida Blacks Stars ya mkoani Singida iliyofanyika jana mkoani humo jana.

Related Posts