Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, amemjibu ‘kiaina’ Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, akisema kikao cha Baraza Kuu la Chadema kilichoketi Januari 22, 2025, kilifuata utaratibu kwa mujibu wa Katiba ya Chadema.
Utaratibu alioutaja Mnyika ni uliotajwa katika katiba ya chama hicho, Ibara ya 6.2;2 (a), inayotaja kuwa akidi ya wajumbe wa mkutano huo iwe asilimia 50.
Kauli hiyo ya Mnyika imekuja siku moja tangu Msajili kuiandikia barua Chadema, akiwataka kujibu malalamiko ya Mchome kuhusu akidi kutotimia ya Baraza Kuu, iliyoidhinisha uteuzi wa Katibu Mkuu, manaibu makatibu wakuu na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho.
Kutokana na hilo, Msajili ametoa siku saba kwa Chadema kujibu malalamiko hayo.
“Tayari tumeiandikia barua Chadema, kuanzia leo (jana) Machi 24, 2025, walete maelezo. Utaratibu ni kwamba ukilalamikiwa, ukapewa barua, na wewe ujibu. Tumewapa wajibu hadi Machi 31 na Mchome tumempatia nakala,” amesema Nyahoza.
Mchome, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, anapinga uteuzi wa viongozi wa juu na wajumbe wa Kamati Kuu uliofanywa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Januari 22, 2025, akidai umekiuka katiba ya chama hicho.
Kada huyo, kupitia barua yake, amelalamikia uteuzi wa Katibu Mkuu, John Mnyika, Aman Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar), akidai waliidhinishwa bila akidi ya kikao cha Baraza Kuu kutimia.
Katika barua ya malalamiko yake pia, Mchome amewataja wajumbe wa Kamati Kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na kikao hicho, akiwemo Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala, akidai uteuzi wao ni batili.
Mchome aliwasilisha malalamiko yake ofisi za Chadema Februari 18, na baadaye, Machi 18, 2025, kada huyo wa Chadema akawasilisha malalamiko yake ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Akizungumza na wanachama wa chama hicho leo, Jumanne, Machi 25, 2025, wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Kanda ya Kusini, Mnyika amesema Chadema inaongozwa kwa mujibu wa Katiba, kanuni, maadili na itifaki ya chama hicho.
Hivyo, akijibu uhalali wa kikao kilichowaidhinisha viongozi wakuu wa chama hicho, Mnyika amechambua katiba ya chama hicho na kuainisha halali wa kikao hicho na visivyo halali.
“Ibara ya 6.2;2 ya katiba ya chama inahusu uhalali wa vikao vya chama, na ibara hii ina sehemu mbili juu ya akidi ya vikao. Sehemu ya kwanza, 6.2;2 (a), inasema itahitajika akidi ya asilimia 50 ya wajumbe kwenye vikao halali kwa ngazi ya kawaida,” amesema.
Ameongeza kuwa, “Ibara ya 6.2;2 (b) inazungumzia akidi nyingine, lakini vikao halali vya kurekebisha au kubadilisha katiba, uchaguzi na sera za chama zitahitaji akidi ya asilimia 75. Kwa hiyo, kuna akidi za aina mbili kwenye chama.”
Amesema kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika Januari 22, 2025, hakikuwa na ajenda ya uchaguzi.
“Baada ya mimi, Katibu Mkuu, kupokea rufaa za wajumbe wa Kamati Kuu ya kuchaguliwa, ajenda ya uchaguzi ikawa si sehemu ya ajenda ya kikao cha Kamati Kuu,” amefafanua Mnyika.
Amesema baada ya kuondoa ajenda ya uchaguzi, kikao kiliendelea na ajenda za kawaida ambazo ni kuthibitisha uteuzi wa Katibu Mkuu na manaibu wake, pamoja na kuthibitisha wajumbe wa mkutano mkuu waliopendekezwa na mwenyekiti.
Amesema ajenda hizo za kawaida zinaongozwa na katiba, Ibara ya 6.2;2 (a), ikielekeza akidi iwe asilimia 50.
“Baraza Kuu la Januari 22, 2025, idadi ya wanachama wajumbe wa Baraza Kuu waliokuwepo, ambao walisaini wenyewe, ni 234, si wa kuandikiwa majina.
“Kila mjumbe aliandika jina lake mwenyewe, cheo, mahali wanakotoka, namba ya simu na kusaini. Ni sawa na asilimia 56.8, na tuna ushahidi wa mahudhurio yao,” amesema kiongozi huyo.
Hata hivyo, amewataka wanachama wa Chadema na Watanzania kuwa na amani, kwa kuwa michezo haramu inayofanywa ndani ya chama hicho na baadhi ya wanachama, wakishirikiana na wadau wengine, itadhibitiwa kama walivyodhibiti mbinu nyingine haramu.