Dar es Salaam. Saa 6:30 usiku wa kuamkia kesho Jumatano, Machi 26, 2025, timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakuwa na mchezo mgumu wa kundi E la kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya wenyeji Morocco utakaochezwa kwenye Uwanja wa Manispaa ya Oujda.
Katika mchezo huo ambao unachezwa kwenye mji wa Oujda, Taifa Stars ina hesabu nne mkononi ambazo inapaswa kuzitimiza kwa ushindi dhidi ya Morocco.
Hesabu ya kwanza ni ya kuweka hai matumaini yake ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2026 kwani ikishinda itafikisha pointi tisa na kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi E linaloongozwa na Morocco yenye pointi 12.
Jambo la pili ambalo Taifa Stars inalipigia hesabu ni kuizuia Morocco kuwa timu ya kwanza ya Afrika kujihakikishia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia.
Morocco itakuwa timu ya kwanza kufuzu Fainali zijazo za Kombe la Dunia kwani itafikisha pointi 12 ambazo hazitowza kufikiwa na timu za Tanzania, Niger na Zambia hata kama zikipata ushindi katika mechi zao za mwishoni.
Hata hivyo hilo la Morocco litatimia iwap Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) litaendeleza adhabu ya kufungiwa kwa Congo ambayo ni miongoni mwa timu zinazounda kundi hilo.
Hesabu ya tatu ya Taifa Stars hapana shaka ni kumaliza unyonge iliyo nao wa miaka 12 dhidi ya Morocco ambapo tangu ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-1, Machi 24, 2013, Taifa Stars imepoteza mechi tatu zilizofuata dhidi ya Morocco kwenye mashindano tofauti ikifunga bao moja na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.
Jambo la nne ambalo Taifa Stars inalilenga kwa kuifunga Morocco ni kujiweka katika mazingira mazuri ya kupata fursa ya kucheza mechi za mchujo za kuwania nafasi moja ya kufuzu Kombe la Dunia kupitia mechi za mchujo za mabara iwapo itashindwa kukata tiketi ya kushiriki moja kwa moja fainali hizo kwa kuongoza kundi.
Mchezo huo wa Morocco dhidi ya Taifa Stars utachezeshwa na refa Alhadi Mahamat kutoka Chad ambaye amekuwa hana historia nzuri na timu za Tanzania na kumbukumbu zinaonyesha katika mechi tano ambazo timu za Tanzania zimekutana na refa huyo katika mashindano ya kimataifa, ni mechi moja tu ambayo timu ya hapa ilipata ushindi lakini michezo minne mingine zilipoteza.
Mahamat mwenye umri wa miaka 38, amechezesha idadi ya mechi 40 za kimataifa ambazo ametoa idadi ya kadi 129 sawa na wastani wa kadi tatu kwa mchezo ambapo kati ya hizo, kadi nyekundu ni tano na za njano ni 124.
Refa Mahamat katika mchezo huo atasaidiwa na wenzake watatu kutoka Chad ambao ni waamuzi wasaidizi wawili, Bogola Issa na Moussa Hafiz na mwamuzi wa akiba, Abdelkerim Ousmane.
Kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Motocco’ amesema kuwa hitajio lao leo ni ushindi na sio vinginevyo.
“Hatuna chochote tunachokihitaji zaidi ya kupata ushindi leo. Ni mchezo mgumu lakini tutawakabili Morocco bila hofu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Morocco.