Hizi hapa sababu Angola kujiondoa upatanishi mzozo wa DRC, M23

Kinshasa. Angola imehitimisha jitihada zake za upatanishi katika mzozo unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kati ya Jeshi la Serikali la FARDC dhidi ya kundi la M23.

Kundi la M23 linaloongozwa na Corneille Nangaa linaendelea na mapigano dhidi ya FARDC na mpaka sasa limefanikiwa kuiteka miji mikuu ya mashariki mwa DRC ukiwamo wa Goma, Bukavu, Nyabibwe na Walikale.

Kutokana na machafuko hayo kusababisha vifo vya watu zaidi ya 7,000 mashariki mwa nchi hiyo, jitihada mbalimbali zilifanyika kuhakikisha amani inarejea katika taifa hilo kwa njia ya kidiplomasia.

Miongoni mwa njia hizo ni pamoja na viongozi na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutoa wito wa kusitishwa mapigano, kisha kuamuru vikosi vya walinda amani vya SAMIDRC kujiondoa DRC kwa awamu.

Baada ya kuamuru vikosi vya SAMIDRC kuondoka kwa awamu nchini humo, Rais Joao Lourenço wa Angola alijitosa kuwa mpatanishi kati ya pande hizo, jitihada ambazo zimegonga mwamba na sasa imetangaza kujiondoa.

Katika taarifa iliyotolewa jana na Ikulu ya Angola, imesema: “Angola inaona ni muhimu kujiondoa katika jukumu la upatanishi wa mzozo huu ili kujikita zaidi katika vipaumbele vya jumla vya Umoja wa Afrika (AU).”

Rais wa Angola, Joao Lourenço ndiye Rais wa muda wa Umoja wa Afrika (AU).

“Katika siku zijazo, Mkuu mwingine wa Nchi wa Afrika atapewa jukumu hili,” imesema taarifa hiyo.

Wakati huo huo, upatanishi ulioanzishwa na Qatar utaendelea huku Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola ikipongeza DRC na Rwanda kutoa kauli ya pamoja ya kukemea mapigano hayo na kuona haja ya kufikiwa maridhiano ya kusitisha vita hiyo.

Wizara hiyo pia ilipongeza uamuzi wa M23 kudai kuwa itakuwa tayari kuondoka katika Mji wa Walikale walioutwaa kutoka mikononi mwa FARDC mapema wiki hii. Hata hivyo, wapiganaji hao wanatajwa kuendelea kuung’ang’ania mji huo.

Mji wa Walikale, uko katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC, ulikamatwa na M23 Machi 19, mwaka huu.

Kulingana na baadhi ya vyanzo, hata hivyo, M23 imesema kuchelewesha kujiondoa kwake kutoka Walikale kunatokana na FARDC kushindwa kuondoa droni zake za kivita katika eneo hilo.

Udhibiti wa Walikale ni wa kimkakati kwa sababu ungevipa vikosi vya M23 na vikosi vinavyoviunga mkono kutoka Rwanda uwezo wa kuuteka Mji wa  Kisangani ambao ni Mji Mkuu wa Jimbo la Tshopo, kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji kilicho kwenye makutano ya mito mitatu barabarani kuelekea Kinshasa.

Katika muktadha huo, matamshi ya Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, yaliyotangazwa kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), yanazua mkanganyiko.

Kainerugaba alidai kuwa Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) ama waasi wa M23 wangeweza kuvamia Kisangani wakati wowote kwa amri ya Rais Museveni.

Alidai kuwa UPDF inalenga kuwalinda watu wa DRC na kusisitiza kuwa hatoruhusu wakazi wa asili ya Uganda kutoka makabila ya Alur, Bahema, Banande, na Batutsi kuteseka, akidai kuwa ana haki ya kuwalinda.

Kainerugaba pia alimshauri Rais wa Marekani, Donald Trump kutosaini makubaliano yoyote ya madini katika Afrika Mashariki bila kushirikisha Uganda na Rwanda.

Alikuwa akirejelea mkutano kati ya Rais wa DRC, Félix Tshisekedi na Mbunge wa Republican wa Marekani, Ronny Jackson, ambapo walijadili mapigano mashariki mwa nchi hiyo na fursa za uwekezaji wa Marekani katika sekta ya madini ya DRC.

Kwa kurudisha uungwaji mkono wa Marekani katika vita dhidi ya M23, Tshisekedi angeweza kuwapa makampuni ya Marekani upendeleo wa kipekee wa kufikia miradi muhimu ya madini na miundombinu nchini DRC.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika ya Habari.

Related Posts