Dar es Salaam. Jaribio la kimatibabu la kibunifu limeonyesha baadhi ya wanawake wanaweza kudhibiti maambukizi Virusi vya Ukimwi (VVU) bila tiba ya dawa za kufubaza makali ya virusi (ARVs) kwa muda mrefu, baada ya kupokea mchanganyiko wa matibabu.
Wanawake wanne kati ya 20 waliokuwa na maambukizi, wameweza kuishi bila dawa za ARV kwa takribani miezi 18, huku miili yao ikifubaza virusi na kinga ya mwili yenye afya (CD4) baada ya jaribio la kwanza la tiba ya ugonjwa huo kufanyika Afrika Kusini.
Katika mahojiano kwa njia ya mtandao na nation.africa yaliyofanywa na Hellen Shikanda wiki hii, Profesa Thumbi Ndung’u ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Utafiti wa Kifua Kikuu/Ukimwi Kusini mwa Jangwa la Sahara (Santhe) amesema, “utafiti huu unaonyesha kuwa mbinu rahisi kama kinga tiba zinaweza kutumika. Ni mara ya kwanza kufanyika Afrika na ulifanyika kwa wanawake. Tafiti nyingi nyingine zimefanywa kwa wanaume.”
Jaribio hilo lililohusisha mbinu ya kinga ya mwili kwa pamoja, watafiti waliwapatia washiriki dawa za ARV kwa mwaka mmoja ili kudhibiti virusi na kulinda kinga ya mwili.
Baadaye, walitumia tiba ya kinga kwa kutumia kingamwili pana zinazolemaza virusi ili kuzuia VVU kushambulia seli, pamoja na kichocheo cha kipokezi cha ‘toll-like receptor 7 (TLR7 agonist)’ ambacho huimarisha mwitikio wa seli za kinga dhidi ya virusi.
Baada ya kusitisha matibabu, washiriki waligawanyika katika makundi matatu, kundi la kwanza lilihusisha wale ambao virusi vilirejea haraka (ndani ya wiki 16).
Kundi la pili wale waliodhibiti virusi kwa wiki 16 hadi 44 kabla ya kuhitaji ARV tena na kundi la tatu ni wale waliodhibiti virusi kwa kipindi chote cha wiki 48 bila dawa yoyote.
“Bado tunawafuatilia kwa karibu, lakini angalau inaonyesha kuwa kwa baadhi ya watu, hata kama ni wachache, uingiliaji huu wa kitabibu unaonekana kufanya kazi,” amesema Profesa Thumbi ambaye ni mmoja wa watafiti wakuu wa utafiti huo.
Mwanasayansi huyu wa Kenya ni mmoja wa watafiti waliokuwa kwenye jaribio hili na aliwasilisha matokeo ya utafiti kwenye Mkutano wa 2025 unaojadili maendeleo ya tafiti za virusi (CROI) uliofanyika San Francisco, Marekani, wiki iliyopita.
Baadhi ya watafiti waliowahi kushiriki katika tafiti za kutafuta kinga na tiba za ukimwi nchini, wamesema hiyo ni hatua nzuri kufikia tiba ya ugonjwa huo.
Dk Lilian Mwakyosi ambaye ameshiriki katika tafiti kadhaa za kutafuta kinga na tiba ya VVU Afrika, amesema kulingana na mwenendo mzima wa VVU, tafiti ni sehemu inayosaidia kujua nini kipya kifanyike ili kuboresha yale mazuri ambayo yameshafanyika katika kutafuta tiba.
Dk Mwakyosi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Dare, amesema hiyo ni hatua moja inayosababisha kujua nini kingine kiongezeke kwa sababu tafiti zikifanyika hata ile ambayo haina majibu yaliyotarajiwa, husaidia hatua nyingine mbele.
“Naona ni nafasi nzuri ya kuboresha kile walichokifanya, ili kuja na namna nzuri zaidi ya kuweza kufanya matibabu zaidi, inasaidia ubunifu gani uongezeke ili kuja na tiba ya moja kwa moja ya kudhibiti maambukizi na kudhibiti waviu wasiwe na VVU tena, naamini huu ni mwelekeo kwenda huko,” amesema Dk Mwakyosi.
Mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Dk Paul Kazyoba amesema matokeo hayo chanya ni maendeleo makubwa, katika tafiti za kutafuta tiba na itafungua mlango kwa ugunduzi zaidi kwa kingamwili ambazo zitakua imara kufubaza VVU.
Dk Kazyoba amesema kilichotumika katika utafiti huo ni miongoni mwa juhudi mpya za kuangalia uwezekano wa kuangalia tiba ya kinga mwili ili kufubaza VVU.
“Kuna kitu kinaitwa ‘virus newtorising antibodies’ kuna watu wakipata maambukizi hawapati shida yoyote, wanakuwa na maambukizi lakini kila wakati ukiangalia unakuta virusi vyao vipo chini, hawana magonjwa nyemelezi au changamoto yoyote ya kiafya.
“Utakuta CD4 zao zipo juu na virusi vichache, walipokuja kutafiti wakagundua wengi wenye hali hiyo wana kitu kinaitwa ‘antibodies’ (kingamwili) ambazo zipo imara na zinashambulia virusi mwilini na kuvifubaza kila vikitaka kuzaliana vinashambuliwa,” amefafanua.
Dk Kazyoba amesema kufuatia hilo, kukazaliwa tafiti ya kuangalia hizo kingamwili zinaweza zikafanyiwa utafiti kwa kutengeneza kingatiba, kwamba zitengenezwa maabara, zizalishwe na wagonjwa wapewe kama tibakinga; utafiti uliofanyika unataka kufanana na huo.
Katika mahojiano yake kwa njia ya mtandao na nation.africa yaliyofanywa na Hellen mapema wiki hii, Profesa Thumbi amesema ingawa tafiti nyingine za tiba ya Ukimwi zimefanywa nje ya Afrika, tafiti hizo zilihusisha mbinu ngumu kama upandikizaji wa uboho, ambao si rahisi kutekelezwa kwa kiwango cha afya ya umma.
“Tunaipa jina la ‘combination’ kwa sababu, kwanza kabisa tulitoa dawa za ARV ili kusaidia kushusha kiwango cha virusi na kulinda kinga ya mwili. Halafu tukatumia immunotherapy (kinga tiba), ambayo ni dawa zinazoweza kuua virusi moja kwa moja au kuchochea seli za kinga mwilini ili kupambana na VVU,” amefafanua Profesa Thumbi.
Sehemu nyingine ya tiba hii ilikuwa matumizi ya dawa ya TLR7 agonist, ambayo husaidia seli za kinga mwilini kupambana vyema na virusi. Baada ya hapo, watafiti walisitisha matibabu ili kuona kama virusi vingerejea.
“Tulikuwa na washiriki sita waliodhibiti virusi. Kati yao, wanne bado hawatumii dawa za ARV na wanadhibiti virusi bila dawa hizo. Hawa watu wanne, kwa wastani, wamekuwa nje ya matibabu ya ARV kwa takriban mwaka mmoja na nusu sasa.
“Bado tunawafuatilia kwa karibu, lakini angalau inaonyesha kuwa, kwa baadhi ya watu, hata kama ni wachache, tiba hii inaonekana kufanya kazi,” amesema Profesa Thumbi.
Amesema wanawake hao wanne wako katika hali nzuri kiafya.
“Tunafuatilia kiwango chao cha virusi (viral load) na kinga yao ya mwili (CD4). Mpaka sasa, kiwango cha virusi hakigunduliki na kinga yao iko kawaida. Hawajakidhi vigezo vya kurejea kutumia ARV,” amesema.
Ingawa watafiti bado hawajui ni kwa muda gani wanawake hao wataendelea bila ARV, Profesa Thumbi amesema kuwa, kwa sababu tiba hiyo ilifanya kazi kwa wachache tu, hawana mpango wa kuieneza kwa watu wengine kwa sasa.
“Tunaendelea kufanya uchunguzi wa maabara kwa wale wanne waliodhibiti virusi bila ARV. Tunatumai maarifa hayo yatatusaidia kuunda mbinu bora za tiba siku zijazo.
“Kile tunachotaka kuelewa sasa ni kwa nini wale 16 hawakuweza kudhibiti virusi? Je, kuna tofauti katika mwitikio wa kinga kati ya makundi haya mawili?” amehoji Profesa Thumbi.
Amesisitiza kuwa, utafiti huu umefungua njia kwa tafiti zaidi kufanyika Afrika.
“Tunaenda kushuhudia tafiti zaidi kama hizi barani Afrika na maendeleo zaidi katika juhudi za kutafuta tiba ya Ukimwi. Kupitia utafiti huu, tunakaribia kudhibiti Ukimwi bila hitaji la ARV, lakini bado ni safari ndefu,” amesema.
Ili ipatikane tiba ya ukimwi watafiti wanahitaji kupata majibu yafuatayo;
Iwe rahisi kama ni kumeza tu au kuchoma pekee, iwe salama, ipatikane kwa kila mhitaji na yenye unafuu wa gharama, ifanye kazi kwa watu wengi, iondoe kirusi moja kwa moja kwenye mwili, izuie maambukizi kwa mtu mwingine, mviu asiambukizwe kwa mara nyingine na iwe tiba ya kweli.