Kocha Azam akomaa na mastaa wake

KOCHA wa Azam FC Rachid Taoussi, amesema timu yake inapitia kipindi kigumu na bado wana nafasi ya  kurudisha utulivu ili kupata matokeo mazuri.

Kikosi hicho ambacho kinashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi, kimeingia mapumziko ya kupisha mechi za timu za Taifa ambazo zinacheza michezo ya kutafuta kufuzu Kombe la Dunia .

Lakini rekodi zake zinaonyesha kuwa, imecheza mechi 23 na kuchukua pointi 48, ikishinda 14,sare sita na kupoteza mitatu.

Azam ambayo, imecheza mechi ya kirafiki dhidi ya KMC Jumamosi iliyopita na kupoteza kwa mabao 4-2 inatakiwa kufanya kazi kubwa kwenye michezo iliyobaki kutokana na kutokuwa na mwenendo mzuri.

Akizungumza na Mwanaspoti kocha huyo alisema timu yake inapitia kipindi kigumu ila anaamini kitapita na watarudi kwenye kiwango chao.

“Kupoteza  dhidi ya KMC kwenye mechi ya kirafiki ni matokeo mabaya lakini ni hatua ambayo inawapa nafasi ya wachezaji wangu, kuelewa ubora wao wakati tunajiandaa kurudi kwenye ligi.

“Makosa kama hayo isingekuwa mechi ya kirafiki yalikuwa yanakwenda kutokea kwenye mechi zetu hapo ingekuwa mbaya zaidi lakini kwasasa tuna nafasi ya kurekebisha ili tufanye vizuri kwenye mechi za mashindano.

Aliongeza kuwa mechi kama ile anataka iwaamshe wachezaji wake wote waliocheza na kujitathimini kabla ya ligi kumalizika.

“Wachezaji ambao hawajafanya vizuri wanapata muda wa kujitafakari, haitakuwa rahisi kubaki na mchezaji anayeshindwa kuhimili ushindani wa kikosi chetu,” alisema kocha Rachid.

Related Posts