Marekani yamvaa Hesgeth, yadai kavujisha siri ya uvamizi

Washington. Serikali ya Rais wa Marekani, Donald Trump imethibitisha kuwa Mwandishi na Mhariri wa jarida la ‘The Atlantic’ alijumuishwa kwenye taarifa za siri zilizovuja katika mitandao ya kijamii kuhusu mpango wa mashambulizi dhidi ya kundi la waasi wa Kihouthi wa nchini Yemen.

Jumatatu, The Atlantic ilichapisha makala ya Mhariri Mkuu wake, Jeffrey Goldberg iliyoeleza mshtuko wake baada ya kugundua kuwa alikuwa ameongezwa kwenye mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea kwenye kundi hilo na maofisa wa ngazi ya juu Serikalini walikuwa wakijadili hatua za kijeshi.

“Dunia iligundua muda mfupi kabla ya saa nane mchana kwa saa za Mashariki, Machi 15, mwaka huu, kuwa Marekani ilikuwa inashambulia maeneo ya Wahothi kote Yemen,” Goldberg aliandika katika aya za mwanzo za makala yake.

“Hata hivyo, mimi nilijua saa mbili kabla ya mabomu ya kwanza kulipuka kuwa shambulio hilo lingeweza kutokea. Sababu ya mimi kujua ni kwamba Pete Hegseth, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, alinivujishia mpango wa vita saa 11:44 asubuhi,” amesema.

Goldberg alieleza kuwa alipokea ombi la mawasiliano kutoka kwa mtumiaji aliyejitambulisha kama Michael Waltz ambaye ni Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Trump, kupitia kwenye programu ya ‘Signal’.

Lakini muda si mrefu, alijikuta katika mazungumzo na maofisa 18 wa Serikali, baadhi yao wakionekana kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, Makamu wa Rais, JD Vance, na Hegseth.

“Sijawahi kuona uvunjaji wa usalama wa aina hii,” Goldberg aliandika.

Hatimaye aliiarifu Ikulu ya White House kuhusu uvunjaji huo wa usalama na kujiondoa kwenye kundi hilo la mazungumzo.

Serikali ya Trump imethibitisha tukio hilo kupitia taarifa kutoka Baraza la Usalama wa Taifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari.

“Kufikia sasa, mfululizo wa jumbe ulioelezwa unaonekana kuwa halisi na tunachunguza jinsi nambari isiyo sahihi ilivyoongezwa kwenye mazungumzo,” amesema Msemaji wa Baraza hilo, Brian Hughes.

“Majadiliano hayo yanaonyesha uratibu wa kina na wa kimkakati kati ya maafisa waandamizi wa serikali,” amesema.

Katika mkutano wa waandishi wa habari baadaye Jumatatu, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Tammy Bruce, alikataa kutoa maoni na kuwataka waandishi wa habari waelekeze maswali yao kwenye masuala ya Ikulu ya White House na siyo suala hilo.

Trump pia alishinikizwa kutoa maoni kuhusu kashfa hiyo wakati wa hafla ya kuzindua kiwanda cha chuma cha Hyundai huko Louisiana ambapo alisema:“Sijui lolote kuhusu hili,”

Trump alianza kwa kusema hivyo, kisha akatoa kauli ya dharau kuhusu jarida lenyewe.

“Si shabiki wa The Atlantic. Kwangu, hilo ni jarida linaloelekea kufilisika. Sidhani kama ni jarida la maana, lakini sifahamu chochote kuhusu suala hili,” alisema Rais Trump.

Baada ya kukebehi jarida hilo, Trump alienda mbali na kuwaomba waandishi wa habari wampatie maelezo kuhusu uvunjaji huo wa usalama.

“Walikuwa wakizungumzia nini?” Trump aliuliza. Kisha akaonekana kuchanganya uvunjaji huo wa usalama na jaribio la makusudi la kuvuruga operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Yemen.

“Lazima halikuwa na athari kubwa kwa sababu shambulio lenyewe lilifanikiwa sana. Naweza kukuhakikishia hilo,” Trump alisema. “Sijui chochote kuhusu hili. Ninyi ndio mnanieleza kwa mara ya kwanza,” alisema.

Kutokana na sakata hilo, wakosoaji wa Trump wametoa wito wa uchunguzi kufanyika. Seneta, Chris Coons, wa Democrats katika Jimbo la Delaware, ni miongoni mwa waliotaka Bunge la Congress lifanye uchunguzi na kuwajibisha waliohusika.

“Ripoti ya Jeffrey Goldberg katika The Atlantic inahitaji uchunguzi wa haraka na wa kina,” Coons aliandika kwenye mitandao ya kijamii.

“Iwapo washauri wa ngazi ya juu wa Rais Trump walitumia mifumo isiyo salama na isiyo rasmi ya serikali kujadili na kusambaza mipango ya vita, basi huu ni uvunjaji mkubwa wa viwango vya kushughulikia taarifa za siri, hali ambayo ingeweza kuhatarisha maisha ya wanajeshi wa Marekani.”

Wimbi jipya la mashambulizi ya Marekani dhidi ya Wahouthi lilianza Machi 15, mwaka huu baada ya Trump kutangaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa aliagiza jeshi kuchukua hatua kali na madhubuti dhidi ya kundi hilo la Yemen.

Lakini mawasiliano ya Goldberg kwenye mazungumzo ya siri ya ‘Signal’ yanaonyesha jinsi uamuzi huo ulivyofikiwa.

Waasi wa Kihouthi kwa muda mrefu wamekuwa shabaha ya mashambulizi ya kijeshi ya Marekani, ikiwa ni pamoja na chini ya mtangulizi wa Trump, Rais Joe Biden.

Tangu Oktoba 2023, Wahouthi wamekuwa wakishambulia meli za Israel na meli za biashara katika Bahari Nyekundu na maeneo jirani, wakipinga vita vya Israel huko Gaza.

Tangu wakati huo, takriban meli 100 za kibiashara zimevamiwa na Wahouthi na mbili kuzamishwa. Hata hivyo, mashambulizi hayo yalipungua Januari, baada ya kusimamishwa kwa muda kwa vita vya Gaza.

Hata hivyo, Trump alitangaza mapema katika muhula wake wa pili kuwa angewaweka Wahouthi kwenye orodha ya makundi ya kigaidi ya kigeni hatua iliyotekelezwa mapema mwezi huu.

Kisha, Machi 2, mwaka huu, Israel ilianza kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza, hali iliyosababisha upungufu mkubwa wa chakula na vifaa vya matibabu. Wahouthi walitoa onyo kuwa wangepiga tena ikiwa vizuizi hivyo visingeondolewa.

Mkataba wa kusitisha mapigano Gaza umesambaratika tangu wakati huo, ukisababisha vifo na uharibifu zaidi katika eneo hilo la Wapalestina.

Mnamo Machi 11, mwaka huu, Goldberg alisema alipokea mwaliko kutoka kwa Waltz, mshauri wa usalama wa taifa, kupitia ‘Signal’.

“Sikuwahi kufikiria kwamba mshauri wa usalama wa taifa angekuwa na uzembe wa kiwango hiki, akimjumuisha mhariri mkuu wa The Atlantic katika mazungumzo ya ndani na maafisa waandamizi wa Marekani, hadi na makamu wa rais,” Goldberg aliandika.

Hata hivyo, mazungumzo hayo yalionyesha mgawanyiko wa sera ndani ya utawala wa Trump. Makamu wa Rais Vance alionyesha wasiwasi kuwa shambulio dhidi ya Wahouthi lingewanufaisha zaidi Wazungu kuliko Marekani.

Lakini Waziri wa Ulinzi, Hegseth alihimiza shambulio hilo lifanyike mara moja, akihofia uvujaji wa taarifa ama Israel kuchukua hatua kwanza.

Maofisa wa utawala huo walijadili jinsi Marekani inavyoweza kunufaika kiuchumi kutokana na hatua hiyo, huku mmoja wao, aliyeaminika kuwa mshauri wa Trump, Stephen Miller, alilisitiza suala hilo.

“Rais alikuwa wazi: mashambulizi yaanze, lakini lazima tuwafanye Misri na Ulaya kuelewa matarajio yetu,” alisema Miller.

Goldberg alijitoa kwenye kundi hilo na kuuliza ikiwa mazungumzo hayo yalikiuka sheria za rekodi za Serikali, kwani ujumbe zilikuwa zimewekwa kisha kufutwa kiotomatiki.

“Kundi hili lilikuwa likisambaza taarifa kwa mtu asiye na idhini ya kuziona,” Goldberg aliandika. “Hili ni tafsiri halisi ya uvujaji wa siri.”

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika ya Habari.

Related Posts