Mbeya. Wanandoa walio wengi wako hatarini kupatwa na magonjwa ya afya ya akili, wasiwasi na mfadhaiko na kuto kushirikiana tendo la ndoa kutokana na migogoro ya kifamilia isiyoisha.
Hatua hiyo imetajwa kuathiri mfumo wa akili kwa kuzalisha kemikali zisizofaa na kupelekea kuwa na hofu, mashaka na kutokujiamini na kusikia sauti za watu masikioni.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Stephano Mkakilwa ameliambia Mwananchi Digital Leo Jumanne Machi 25, 2025 wakati akifafanua visababishi vya tatizo la afya ya akili kwa watu walio kwenye uhusiano.
Amesema kwa miaka ya sasa kumekuwa na changamoto kubwa ya ongezeko la tatizo la magonjwa ya afya ya akili hususani, wasiwasi na mfadhahiko ambayo hutokana na migogoro ya kifamilia baina ya mume na mke.
“Kimsingi athari ni kubwa tunapokea wanawake na wanaume ambao wamekuwa na dalili za afya ya akili ambao kwa kiwango kikubwa uchangiwa na mifumo ya maisha ya kila siku,” amesema Dk Stephano.
Amesema kutokana na ukubwa wa tatizo wamekuwa wakitoa elimu na ushauri kwa walengwa kabla ya kuanza tiba ya kuwarejesha katika hali ya kawaida.
Dk Stephano amesema asilimia kubwa ya walengwa wakifikia hatua hiyo huathirika kisaikolojia na kukosa hisia ya tendo la ndoa na shughuli zozote za kiuchumi sambamba na kukata tamaa ya kuishi.
“Wawili hao wakifikia hatua hiyo ndani ya nyumba hakuna kitakacho endelea maana kila mmoja anamtazama mwenzake kwa sura ya tofauti na wengine hufikia wakati kama ni mfanyakazi anaona hakuna sababu ya kuendelea na kuhisi wamerogwa,” amesema.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Stephano Mkakilwa
Dk Stephano ametaja baadhi ya dalili za kupata magonjwa ya afya ya akili ni pamoja na kusikia sauti za watu masikioni, hofu, kujitenga na watu na hata kuwa na hasira pasipo sababu na kuwa na hisia mbaya.
“Niwatake walio kwenye mahusiano ukiona miongoni mwa dalili hizo wahi kupata matibabu na elimu ya saikolojia kabla ya athari kubwa kujitokeza na kwamba asilimia kubwa wanao pokelewa ni wenye umri wa rika balehe na watu wazima kuanzia umri wa miaka 60 na kuendelea,” amesema.
Amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo wanandoa wanapaswa kujenga utamaduni wa kutoweka vitu moyoni, kuamiana na kuwa na uhusiano mzuri kwa kutovipa nafasi vitu visivyo na tija .
Mmoja wa waathirika wa changamoto za mahusiano, Tamali Samwel amesema kwa kipindi cha miezi sita sasa mumewe ataki kushiriki tendo la ndoa na hata kudiliki kuniachia chumba.
“Changamoto ni kubwa usinione naoga natembea njiani moyoni nimebeba gunia la misumari mwanaume hataki kunigusa hata nikimgusa napigwa na anaenda kulala sebuleni au chumba cha watoto,” amesema.
Amesema kutokana na kitendo hicho amejikuta akijitumbukiza kwenye tabia za ulaibu wa ulevi wa kupindukia ili kupunguza mawazo.
Naye Solomon Aloyce amesema changamoto inayosababisha kushindwa kuwa na uhusiano mzuri na mwenza wake ni mifumo ya maisha ya migogoro isiyo na mwisho.
“Kimsingi asilimia kubwa mwanaume kelele ni mwiko kwake, sasa unakuta mwanamke yeye ni hakimu ndani ya nyumba ukichelewa ulikuwa wapi? ukinukia manukato ulikuwa na danga lako, sasa hayo mapito binasfi siyawezi,” amesema.
Mtaalam wa Saikolojia na Mkurugenzi wa Taasisi ya Nasaha Hub, Silvester Mwashiuya amesema ndoa zikifikia hatua hiyo ni changamoto ambayo usababisha kuanza kujihukumu .
” Hali hiyo kwa wanandoa ufika mbali zaidi kwa kuanza kujihukumu kwa hisia na majuto kujiona ni wakosaji kwa kila mmoja hali ambayo uwasukuma kujiingiza kwenye tabia hatarishi za ulevi wa kupindukia na kufika hatua ya kujikatisha uhai,” amesema.