Hong Kong. Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Samsung Electronics, Han Jong-Hee (63) amefariki dunia kwa mshtuko wa moyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya CNN, Han Jong-Hee ambaye ni mkurugenzi mwenza wa kampuni hiyo amefariki dunia leo Jumanne kwa mshtuko wa moyo.
Hana ambaye alizaliwa mwaka 1962, alikuwa akiongoza biashara za elektroniki na vifaa vya simu vya Samsung tangu mwaka 2022.
Aliteuliwa kuwa makamu wa rais na mkurugenzi mtendaji wa Samsung Electronics mwaka 2022.
Kwa mujibu wa CNN, Jun Young-Hyun, ameteuliwa kuchukua nafasi ya Han na kwamba atakuwa mkurugenzi pekee wa kampuni hiyo.
Han amekuwa kwenye kampuni ya Samsung kwa takriban miaka 37, kama mkuu wa biashara za elektroniki pia alichangia katika ukuaji wa kampuni hiyo katika hali ngumu ya kibiashara.
Han alijiunga na kampuni hiyo mwaka 1988 baada ya kupata shahada ya uzamili katika uhandisi wa umeme kutoka Chuo Kikuu cha Inha.
Kabla ya kuongoza idara ya elektroniki na vifaa ya Samsung, alikuwa akiongoza operesheni ya maonyesho.
Pia, taarifa zinaeleza Han alikuwa muhimu katika kuzindua Televisheni za LED za Samsung, ambazo, pamoja na uvumbuzi mwingine wake, zilisaidia kampuni kuonyesha uongozi wa kiteknolojia.
Mkurugenzi mpya aliyeteuliwa, Jun Young-hyun, atakuwa pekee anayesimamia kampuni ya teknolojia hiyo Korea Kusini wakati yanafanyika maboresho ya kibiashara.
Jun aliteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa wa Samsung wiki iliyopita katika mkutano wa kila mwaka wa wanahisa.
Changamoto za Samsung Hivi Karibuni
Samsung imekuwa ikikumbana na changamoto kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, hasa katika sekta ya semiconductor.
Kampuni hiyo imeshindwa kuendana na kasi ya washindani kama vile Taiwan Semiconductor Manufacturing Company (TSMC) katika uzalishaji wa vifaa vya hali ya juu.
Pia, katika soko la vifaa vya kumbukumbu (memory chips), Samsung imebaki nyuma ya kampuni nyingine ya Korea Kusini, Hynix, hasa kwenye teknolojia ya High Bandwidth Memory (HBM) ambayo ni muhimu kwa vifaa vya Nvidia.
Wakati wa mkutano wa mwaka na wanahisa wiki iliyopita, Han aliongoza kikao ambapo aliomba radhi kwa utendaji dhaifu wa hisa za Samsung. Alitahadharisha kuwa mwaka 2025 utakuwa mgumu kutokana na hali ya kutokuwa na uhakika ya sera za kiuchumi katika mataifa makubwa.
“Tunapanga kufanya ununuzi na uchukuzi wa kampuni (mergers and acquisitions) wenye maana ili kuimarisha ukuaji wetu,” alisema Han kulingana na ripoti ya Reuters.
Kifo cha Han kinakuja wakati Samsung inahitaji uongozi thabiti ili kukabiliana na changamoto hizi.
Wataalamu wanasema kuwa nafasi yake itakuwa ngumu kuiziba kwa sababu ya uzoefu wake wa muda mrefu na mafanikio yake katika kuweka Samsung kwenye nafasi ya juu ya soko la teknolojia.
Familia yake, wafanyakazi, na jamii ya teknolojia wameachwa katika hali ya mshtuko na majonzi.
Kifo cha Han ni pigo kubwa kwa Samsung na sekta ya teknolojia kwa ujumla, lakini kampuni inaahidi kuendelea na maono yake ya kuongoza ulimwengu katika ubunifu wa teknolojia.