Mlipuko kiwanda cha TOL Mbeya wasababisha hasara

Mbeya. Mlipuko ulitokea kwenye mtambo ya kaboni katika kiwanda cha gesi cha Tanzania Oxygen Ltd (TOL) kilichopo kwenye wilayani Rungwe, mkoani hapa umesababisha uharibifu mkubwa wa kiwanda hicho na miundombinu inayozunguka.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Daniel Warungu, amewahakikishia umma kuwa hakuna vifo wala majeraha makubwa yaliyotokea wakati wa tukio hilo na kwamba shughuli tayari zinaendelea kurejea.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mlipuko ulisababishwa na shinikizo kubwa ndani ya taki la lori, ambalo lilizidi kikomo salama cha bar 18 hivyo kuzifanya valvu kushindwa kumudu shinikizo hilo.

Akizungumza na gazeti dada la The Citizen, Warungu alieleza kuwa mlipuko ulitokea kwenye lori moja la TOL lenye uzito wa tani 9.5 ambalo linatumika kusafirisha gesi kutoka kiwanda cha Kyejo kilichopo Busokelo hadi kiwanda cha Ikama huko Rungwe.

“Tuna matumizi ya malori haya kusafirisha bidhaa kutoka kiwanda chetu cha Kyejo, ambacho kiko kilometa 29 kutoka kiwanda cha Ikama. Barabara hiyo siyo ya lami, jambo linalofanya kuwa vigumu kwa malori makubwa kufika, na inawezekana kwamba lori hilo lilipata ufa kutokana hali mbaya ya barabara,” alisema Warungu.

Licha ya ukali wa mlipuko, alisisitiza kuwa hakuna majeraha makubwa yaliyotokea.

“Jambo muhimu ni kwamba hakuna aliyejeruhiwa vibaya, mabati ya majengo ya jirani yaliharibika, lakini shughuli katika viwanda visivyohusika na mlipuko zinaendelea kama kawaida. Kipaumbele chetu kikuu ni usalama, na tunafanya kazi kwa bidii kuhakikisha viwango vya juu vya tasnia kwa usalama na ubora,” alisema.

Hata hivyo, kulingana na vyanzo vya ndani kutoka kiwandani, nguvu ya mlipuko ililirusha lori hilo angani, ambapo liliharibu miundombinu muhimu, ikiwemo jengo la ofisi, kantini, kiwanda cha kaboni namba 1, na pampu ya dizeli. Aidha, lori lingine pamoja liliharibiwa katika mlipuko huo.

Kaboni hiyo iliyokuwa imehifadhiwa kioevu katika nyuzi joto -50°C, ilisababisha changamoto za ziada ikiwemo baridi kali iliyosababisha baridi kali (cold burn) ambayo iliharibu lori la pili na vifaa vingine vya kiwandani, ikiwemo vya kipima ubora wa bidhaa.

Vyanzo huru kutoka kiwandani vinaelezea kuwa mlipuko huenda umetokana na kushindwa kwa valvu za usalama, ambazo zimekusudiwa kutoa shinikizo la ziada na kuzuia milipuko kama hii. Uchunguzi bado unaendelea na mamlaka za TOL zinakagua kwa karibu ukubwa kamili wa uharibifu huo.

Mlipo huo umesababisha kusitishwa kwa muda kwa baadhi ya sehemu za kiwanda, ingawa Warungu alithibitisha kuwa uzalishaji katika viwanda vingine hauathiriki.

“Tunaendelea na ukaguzi wa usalama, na tunatarajia uzalishaji katika kiwanda kilichohusika kurudi katika hali ya kawaida mwishoni mwa juma lijalo,” alisema.

Warungu alisisitiza kuwa usalama na ustawi wa wafanyakazi na jamii inayozunguka ni kipaumbele cha juu cha kampuni hiyo. TOL imejizatiti kudumisha sifa yake kama kiongozi wa usalama na ubora katika tasnia hiyo.

Related Posts