Serengeti Boys yatua Morocco, hesabu Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imewasili jana Morocco ikitokea Misri tayari kwa kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri kama huo huku kocha mkuu wa kikosi hicho, Aggrey Morris akitamba kuwa lengo lao ni moja tu ambalo ni kushiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu zitakazofanyika Qatar.

Katika Afcon U17, Serengeti Boys imepangwa katika kundi A na wenyeji Morocco, Zambia na Uganda.

Serengeti Boys imewasili Morocco ikitokea Misri ambako iliweka kambi ya mwisho ya kujiandaa na Afcon U17 mwaka huu na kocha Morris amesema kuwa kambi hiyo imewaimarisha vilivyo na kuwapa ubora wa kuwawezesha kufanya vizuri katika fainali hizo.

“Kambi ya Misri imekuwa na mafanikio makubwa kwa upande wetu. Vijana wamepata mechi za kutosha za kirafiki ambazo zimewapa utayari wa kufanya kile ambacho tunakitarajia hapa Morocco ambacho sio kingine bali ni kufuzu Fainali za  Kombe la Dunia.

“Tupo kwenye kundi gumu lakini tunaamini tunaweza kufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ambayo inatosha kutupa tiketi ya kwenda Kombe la Dunia. Watanzania wasiwe na wasiwasi na vijana. Tumejiandaa vizuri na kila mmoja yupo tayari kupeperusha bendera ya Tanzania,” amesema Morris.

Serengeti Boys itaanza fainali hizo za Afcon U17 kwa kukabiliana na Zambia, Machi 31, kuanzia saa 11:00 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki, mechi ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa El Bachir jijini Casablanca.

Aprili 3, Serengeti Boys itacheza mechi ya pili uwanjani hapohapo dhidi ya Uganda, mechi ambayo itachezwa kuanzia saa 2:00 usiku na mechi ya mwisho ya hatua ya makundi itamaliza na Morocco, Aprili 06 kuanzia saa 4:00 usiku katika Uwanja huo wa El Bachir.

Fainali hizo za Afcon U17 mwaka huu zinashirikisha timu 16 za taifa za vijana wenye umri huo ambazo zimegawanya katika makundi manne mtawalia.

Ukiondoa kundi A, kundi B linaundwa na timu za Burkina Faso, Cameroon, Afrika Kusini na Misri na kundi C lina timu za Senegal, Gambia, Somalia na Tunisia huku kundi D likiwa na timu za Ivory Coast, Angola. Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mali.

Timu nane zitakazofanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali zitajihakikishia moja kwa moja tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri chini ya miaka 17.

Mara mbili zilizopita ambazo Serengeti Boys ilishiriki fainali za Afcon U17, haikufanikiwa kufuzu Kombe la Dunia ambazo ni 2017 na 2019.

Related Posts