Wasira aonya wanaotaka ubunge kwa rushwa CCM

Ngara. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) -Bara, Stephen Wasira, amesema ana taarifa za baadhi ya wanachama wanaotaka ubunge kuanza kuvunja maadili katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Hivyo, amewakumbusha wanaotaka ubunge na wabunge waliopo madarakani kuzingatia maadili, huku akitoa rai kwa wajumbe wa CCM, ambao watapiga kura kuchagua mgombea mmoja kati ya watatu ndani ya chama, kuhakikisha wanapiga kura kwa uhuru bila kuhongwa fedha.

Akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi katika kikao cha ndani kilichofanyika wilayani Ngara, mkoani Kagera jana, Machi 24, 2025 Wasira amesema chama chao kimebadilisha utaratibu wa kupata wajumbe wanaopiga kura ili kuwapata wagombea wake.

“Huko nyuma hapa Ngara, waliokuwa wanapiga kura ni wajumbe 700, lakini kwa sasa ni zaidi ya 10,000. Ni wengi, maana sasa hivi mabalozi wote wanapiga kura, kwenye kamati zenu za watu wanne kote huko wanapiga kura.

“Kamati za jumuiya zote zinapiga kura, kamati zao za utekelezaji zote zinapiga kura na watu wengine wengi ambao siwezi kuwataja wote. Tunachotaka mjue sababu za mabadiliko hayo; kwanza, tunatanua demokrasia ndani ya chama chetu,” amesema Wasira na kuongeza:

“Pia tunataka watu wengi wanaopiga kura watuambie kwa maoni ya wananchi wa Ngara, mtusaidie kusema katika watu watatu mmoja kati ya hawa anamzidi mwingine, ili tupate mtu wa kupeperusha bendera ya CCM kati ya hawa watatu, tujue wananchi wanasemaje.”

Amesema yeye ni Makamu Mwenyekiti na moja ya kazi yake ni kusimamia maadili, hususan kwa wanaotaka ubunge, kwa kuwa wameshabaini kuna watu wameanza kunyemelea na wananyemelea kwa kuvunja maadili.

“Wajumbe tunataka mpige kura mkiwa watu huru, muiambie CCM mkimsimamisha huyu, tutashinda bila tabu kama atakavyoshinda Dk Samia. Naamini kazi hii wajumbe mnaiweza vizuri, hivyo tuleteeni wagombea wanaokubalika.

“Lakini wale wanaotaka ubunge, baadhi yao nina habari zao, wameanza kuvuruga maadili, wanataka muwapigie kura kwa hela wanazowapa. Na Biblia inasema rushwa inapofusha; maana yake, ukiona mtu anasambaza hela, lazima ujiulize, kwa nini hiyo imekuwa huduma?” amesisitiza.

“Na hili nalisema kwa wagombea wapya na wabunge waliopo. Tunachunguza, tunajua mwenendo huo, sasa nawaambia acheni kupofusha wajumbe, na ninyi wajumbe na mabalozi wa nyumba 10 mtupe heshima ya kutuletea watu wazuri. Ndio wajibu wenu,” ameagiza.

Akizungumzia siri ya CCM kuendelea kubakia madarakani, Wasira amesema vyama vingi vya siasa vilivyofanikisha kupatikana kwa uhuru barani Afrika vimeshakufa, lakini CCM imeendelea kuwepo kwa sababu imejikita na mizizi yake inaanzia chini; kila nyumba 10 kuna kiongozi wa nyumba na ana kamati.

Amesema ndiyo maana chama hicho kinaendelea kuwa imara.

“Kama chama hiki kingekuwa kinashikiliwa na sisi huko juu, tungeweza kufikiria kipo kumbe hakipo. Ndivyo ilivyotokea kwa Kanu (chama kilichopigania uhuru Kenya), chama kilicholeta uhuru hakipo, Zambia hakipo, Uganda hakipo, lakini chama kilicholeta uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) na Mapinduzi ya Zanzibar kipo,” amesema.

Amesema baadhi ya nchi huwa zikijiuliza kwa nini CCM imekaa sana madarakani, wao huwajibu kuwa walidai uhuru ili kuendesha nchi na siyo kwa muda, bali shabaha ni kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo.

Kwa mujibu wa Wasira, CCM imeendelea kuzisimamia Serikali zake kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa na wakati mwingine maendeleo husababisha changamoto mpya.

“Wakati tunajitawala hatukuwa na chuo kikuu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzia jengo la Tanu Lumumba… Wasomi waliokuwa wanatoka pale walikuwa wanapewa kazi moja kwa moja. Kulikuwa na kazi, hakuna watu; leo tuna vyuo vikuu 40, vinatoa watu wangapi kwa mwaka?” amesema.

Hivyo, amesema kwa upande wa elimu, nchi imepiga hatua kwa watu wengi kusoma licha ya kuwa bado kuna changamoto ya ajira, ambayo amesema nayo imeshanza kutafutiwa ufumbuzi.  

Hivyo, amesema watu kwa upande wa elimu nchi imepiga hatua kwa watu wengi kusoma licha ya kuwa kuna changamoto bado ya ajira ambayo amesema nayo imeshanza kutafutiwa ufumbuzi.

Related Posts