Mechi nne za kimkakati Ligi Kuu Bara

MECHI nne za Ligi Kuu Bara zitapigwa Jumatano hii kwenye viwanja tofauti zikiwa na vita tatu, kisasi, ubingwa na kujiweka pazuri.

Pamba na Namungo zitavaana jijini Mwanza, KMC wakikwaana na Prisons Dar es Salaam. Hizo mbili kitakwimu na jinsi msimamo wa Ligi ulivyo ni mechi za kujinusuru na upepo wa kwenda na maji.

Kila moja hapo bado ipo hatarini na lolote linaweza kumtokea yoyote atakayeshindwa kuchanga karata zake kuelekea mwisho wa msimu.

Fountain Gate inacheza na Singida Black Stars kule Arusha. Kwa takwimu za mwenendo wa timu zilizoshuka daraja misimu miwili mfululizo iliyopita, Fountain inahitaji walau pointi tatu kuvuta pumzi kidogo wakati ikisoma ramani mpya. Katika misimu miwili iliyopita timu nyingi zilizoshuka daraja au kucheza playoff ni zile zilizokuwa na pointi 30 kushuka chini, Fountain sasa akiwa na 28 nafasi ya saba.

Singida BS wao mchuano wao kwasasa ni kuwania nafasi nne za juu ili kusaka nafasi ya kushiriki kimataifa sambamba na kupata mkwanja mnene wa zawadi.

Mchezo unaozungumzwa zaidi midomoni ni ule wa Tabora dhidi ya Yanga mjini Tabora. Ni mechi inayoangaliwa kwa jicho la kisasi ambapo wageni wanapambana kupindua mezani kipigo cha mabao 3-1 walichokipata Dar es Salaam.

Ni mechi ambao imekuwa na siasa nyingi na vijembe vya nje ya uwanja ikiwemo tuhuma za rushwa ambazo hatahivyo baadhi ya viongozi wamekuwa wakishindwa kuzithibitisha.

Yanga inajua ugumu wa Tabora na imekwenda mapema Mkoani Tabora kujipanga kwa vita ya uwanjani kusaka pointi za kuwaweka kwenye nafasi ya kutetea ubingwa wao.

Kocha wa Yanga, Hamdi Miloud huu utakuwa mchezo wake wa kwanza dhidi ya Tabora lakini anatambua kwamba, wenyeji wao ndio waliowatimua makocha waliosimamia mchezo wa kwanza.

Tabora nao walikuwa na Anicet Makiadi ambaye alisimamia mchezo wa ushindi lakini naye ametimuliwa na sasa kikosi hicho kipo chini ya kocha mpya Mzimbabwe, Genesis Mangombe.

Kocha wa Yanga Hamdi Miloud akizungumzia mchezo huo alisema: “Nimeambiwa ni muda mrefu Yanga haijacheza uwanja huu kwahiyo tutakwenda kuuona uwanja mpya,tumejiandaa sawasawa hii ni timu ambayo ilitufunga kwenye mechi ya kwanza, tunatakiwa kuhakikisha tunarudisha heshima yetu, nafuraha kwamba wachezaji wako sawasawa labda Khalid Aucho, tutaangalia kama ataweza kuwa tayari.”

Sio tu kushinda Yanga imekuwa na ushindi mzuri ambapo imefunga mabao 16 safu yake ya ushambuliaji na kiungo ikiwa na moto mkali huku ukuta wake ukiruhusu mabao mawili pekee.

Mambo hayapo sawa sana kwa wenyeji ambao mechi tano za ligi zilizopita imeshinda mechi moja pekee, ikitoa sare tatu na kupoteza mchezo mmoja tena wakiwa nyumbani dhidi ya JKT Tanzania ambao waliilazimisha sare isiyo na mabao Yanga.

Mangombe alisema:”Unapokutana na bingwa mtetezi lakini pia akiwa ndio anaongoza ligi lazima uipe heshima yake, tutakuwa na mpango maalum wa mchezo huu, tunakwenda kukutana na timu ambayo ina wachezaji wenye ubora mkubwa lakini hatutawaheshimu kupita kiasi tutacheza nyumbani tunataka kuwapa furaha mashabiki wetu.”

Related Posts