BENKI YA CRDB YATAMBULISHA MKOPO WA KIDIJITALI WA ‘JINASUE’

Katika mpango wake wa kuongeza ujumuishaji wa wananchi kiuchumi, Benki ya CRDB imezindua huduma ya mikopo ya Jinasue inayowalenga wateja wake wote wenye uhitaji wa fedha.


Huduma hiyo iliyozinduliwa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili itawaruhusu wateja wa benki wenye salio dogo kwenye akaunti zao kuliko muamala wanaotaka kuifanya au wateja wanaohitaji fedha kutokana na dharura walizonazo.


Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Adili amesema ujumuishi wa kifedha ni ajenda ya kimkakati ndani ya Benki ya CRDB inayoamini suala hilo ni msingi wa mapinduzi ya kiuchumi katika jamii yoyote.


“Tunayo mikopo inayowalenga baadhi ya wateja wetu kama vile watumishi, wanafunzi wa vyuo vikuu na wastaafu pamoja na wafanyabiashara. Tumegundua kuna watu ambao hawapo kwenye makundi hayo ambao wanahitaji uwezeshaji hivyo kuja na Jinasue, mikopo inayomlenga kila mteja wa benki yetu,” amesema Adili.

Mikopo hiyo, amesema itakuwa inatolewa kwa kushirikiana na kampuni ya CreditInfo na itatolewa kupitia SimBanking kuwawezesha wateja wetu kumudu gharama za huduma, bidhaa, na ankara mbalimbali wanapokuwa na changamoto za kifedha.

Kupitia SimBanking, wateja watapata mikopo ya Jinasue kwa urahisi kuanzia Shilingi 1,000 hadi Shilingi milioni 1 kwa riba ya asilimia 8 tu. Ili kupata mkopo huu, mteja anatakiwa kuwa anatumia akaunti ya Benki ya CRDB na amejiunga na huduma ya SimBanking. 


“Mkopo wa Jinasue ni suluhisho muhimu kwa wateja wanapokabiliwa na changamoto za kifedha wakati wa kulipa ankara na huduma muhimu. Huu ni mkopo wa haraka, wa kidijitali, na wa gharama nafuu ambao utawasaidia wateja wetu kukabiliana na changamoto za uhaba wa fedha,” amesema Adili.


Kwa muda mrefu, Benki ya CRDB imekuwa ikibuni huduma za aina tofauti zinazolenga kukidhi mahitaji ya wateja wake huku ikiwekeza nguvu katika matumizi ya teknolojia.


Katika jitihada hizo, mwaka 2017, ilizindua “salary advance,” mikopo inayowalenga wafanyakazi na watumishi wa umma inayotolewa hadi shilingi milioni 3 kwa riba ya asilimia 5 tu, na mwaka 2019 ikazindua “boom advance,” kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu ikitolewa kuanzia shilingi 1,000 hadi shilingi 150,000 na kurejeshwa hadi kwa siku 60 tangu walipochukua mkopo.


Mwaka 2020 Benki ya CRDB ilitambulisha sokoni “pension advance,” mikopo mahsusi kwa ajili ya wastaafu wanaoruhusiwa kukopa kuanzia shilingi 5,000 hadi shilingi milioni 1.

Related Posts