· Stanbic Tanzania imethibitisha tena dhamira yake ya
kusaidia kukuza biashara, kufadhili miundombinu, na ushirikiano wa kikanda wakati
wa huu nyeti wa usafirishaji shehena na uchukuzi kwa ujumla.
· Benki hii ya tatu kwa ukubwa wa faida inayo
masuluhisho ya kifedha ya kuboresha ufanisi wa uchukuzi, kupanua wigo wa masoko,
na kuhamasisha fursa za kibiashara nje ya nchi.
· Kushirikiana na wafanybiashara na Serikali kuifanya
Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uchukuzi barani Afrika
Kadri Afrika Mashariki inavyozidi kukua kibiashara,
Tanzania inaendelea kujizatiti kama kitovu cha uchukuzi wa shehena na biashara,
ikichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa kiuchumi katika ukanda huu ulioneemeka
kwa rasilimali asili na watu.
Uwekezaji na ushirikiano wa wadau mbalimbali, hasa
katika kuboresha miundombinu na kufadhili upatikanaji wa mitaji, umewezesha
kuunganisha wafanyabiashara kutoka mataifa tofauti wa eneo hili na kuimarisha
nafasi yake kama lango kuu la biashara katika nchi za Afrika Mashariki, Kati,
na Kusini mwa Afrika.
Benki ya Stanbic Tanzania, taasisi inayoongoza
katika ufadhili wa biashara na uwekezaji katika miundombinu, imethibitisha
utayari wake wa kuwa sehemu ya maono haya ya Tanzania wakati wa Mkutano wa East
Africa Cargo Connect Summit (EACCS) 2025 uliofanyika jijini Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki jana.
Mkutano huu uliwakutanisha viongozi wa sekta,
watunga sera, na wawekezaji kujadili fursa na changamoto katika urahisishaji wa
biashara, uchukuzi na usafirishaji wa shehena, pamoja na ufadhili wa miradi ya
miundombinu stahiki.
Kupitia kaulimbiu ya “Tanzania: Kinara wa Mustakabali
wa Kuunganisha Mitandao ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika,” mkutano wa
EACCS 2025 ulisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu, kuwezesha upatikanaji
wa ufadhili unaofaa, na kutekeleza sera za biashara zinazowezesha miamala ya
biashara kufanyika bila vikwazo kati ya mataifa mbalimbali.
Benki ya Stanbic imekuwa kiongozi katika kusaidia
wafanyabiashara kushindana kwa ufanisi katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kupitia ushirikiano na serikali na sekta binafsi, tunatoa masuluhisho maalum ya
kifedha yanayolenga kukabiliana na mahitaji yanayobadilika ya sekta ya uchukuzi
na usafirishaji wa shehena.
“Kwetu sisi Benki ya Stanbic, Tanzania ni nyumbani,
na tunajivunia kushiriki kikamilifu katika ukuaji na maendeleo yake. Hii si
kauli tu – ni ahadi tunayothibitisha kwa vitendo. Katika kipindi cha miaka
miwili pekee, tumetoa ufadhili wa zaidi ya dola bilioni 1 za Marekani,
tukichangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo yake ya kiuchumi,” alisema Bw.
Stephen Mpuya, Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa kwa Biashara wa Benki ya Stanbic
Tanzania.
“Huu ni mwaka wa kipekee kwetu, kwani tunasherehekea
miaka 30 ya uwepo wetu nchini. Imekuwa ni safari iliyojaa ustahimilivu,
mafanikio, na mchango mkubwa katika kusaidia biashara kuimarika, huku
tukichangia kwa kiwango kikubwa katika ujenzi wa miundombinu bora, na hivyo
kuchochea ukuaji na maendeleo ya taifa letu kwa ujumla,” aliongeza huku
akishauri kuwa:
“Ili Tanzania itimize uwezo wake kama kitovu cha
biashara na uchukuzi, tunapaswa kuharakisha uwekezaji katika miundombinu,
kurahisisha michakato ya biashara, na kuwapa wafanyabiashara uwezo wa kifedha
unaostahili.:
Kauli
hiyo iliungwa mkono na washiriki wa mkutano wa pili wa EACCS, akiwemo muwakilishi
wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bi Fatima Rajabu, aliyekuwa
mgeni rasmi wa mkutano wa siku moja uliofanyika Mlimani City tarehe 27/03/2025
kwa niaba ya Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA.
“Mkutano
huu unafanyika katika kipindi nyeti kwa ukanda wetu, unaoshuhudia ukuaji
mkubwa, fursa nyingi, na changamoto katika mnyororo wa thamani wa usambazaji
duniani. Kadri Afrika Mashariki inavyoendelea kuwa mshiriki muhimu katika
biashara ya kimataifa, ni muhimu kuitumia nafasi yetu ya kijiografia,
rasilimali, na miundombinu inayokua haraka ili kuhamasisha ushirikiano wa
kikanda na kuimarisha mitandao ya biashara ya kimataifa kwa ajili ya maendeleo
endelevu,” alibainisha Bi Rajabu.
Mjumbe
kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw Daudi Stephano Riganda, alisema:
“Usafirishaji ni muhimu katika ukuaji wa kiuchumi, kutengeneza ajira na
kuunganisha watu na huduma muhimu. Miundombinu imara ya usafiri ni kipengele
muhimu katika kuvutia Uwekezaji wa Moja kwa Moja kutoka Nje (FDI) kwa sababu
inarahisisha biashara, kupunguza gharama, na kuboresha ushindani wa kiuchumi.”
Mwenyekiti
wa Baraza la Wasafirishaji Shehena Tanzania (TSC), Bw alisisitiza umuhimu wa
miundombinu bora na ushiriki wa tasnia ya fedha katika maendeleo ya sekta ya
usafirishaji. Mbali na kudhamini mkutano huu, mchango wa Benki ya Stanbic ni
muhimu kwani maendeleo ya sekta hii yanahitaji ufadhili na ushiriki mkubwa wa
taasisi za fedha,”.
Stephen Mpuya, Mkuu wa kitengo cha bidhaa kwa biashara, Benki ya Stanbic akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa usafirishaji Afrika mashariki uliofanyika alhamisi wiki iliyopita Jijini Dar es salaam.