Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewaweka njiapanda watia nia katika uchaguzi mkuu ujao baada ya kusisitiza msimamo wake wa hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi kushinikiza mifumo ya uchaguzi kurekebishwa.
Watia nia wa ubunge na udiwani wametakiwa kuchagua ama kukihama chama hicho kwenda kugombea kupitia vyama vingine au kuungana na viongozi kupigania mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi.
Wakati viongozi wa Chadema wakiweka msimamo huo, vyama vya siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) vimeainisha changamoto zinazozorotesha mchakato wa kidemokrasia wakati wa uchaguzi ili kuingia kwenye meza ya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan.
Leo, Aprili 3, 2025, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amekutana na watia nia jijini Dar es Salaam ambao amewaeleza kinagaubaga kwamba, ajenda yao ya ‘No reforms, no election’ iko palepale na Oktoba 2025, hakutakuwa na uchaguzi.
Hata hivyo, baadhi ya watia nia waliohudhuria mkutano huo, wameliambia Mwananchi kwamba walikuwa na ndoto za kugombea ubunge lakini hawana budi kuunga msimamo wa chama hicho.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Lissu amesema makada wanaopinga msimamo wa chama kwa kueleza washiriki uchaguzi huo anaona hawako serious (makini).
“No reforms, no election ndiyo msimamo wa chama uliopitishwa na kamati kuu, mimi sikuwa mwenyekiti, alikuwa Freeman Mbowe, mimi nilikuwa makamu. Kesho yake tulipeleka kwenye mkutano mkuu wa Taifa na ulipitisha msimamo huu.
“Kwa katiba yetu, mkutano mkuu ukisema twende hivi, ni chombo gani kingine kinaweza kubisha? Vinginevyo wajumbe mniambie kama huu si msimamo sahihi,” amehoji Lissu.
Lissu amesema ‘No reforms, no election’ ni mwelekeo wa chama ingawa kuna baadhi ya watu wanadai unakwenda kuua chama hicho. Hata hivyo, amehoji hata sasa hawana wabunge, kwani chama kimekufa?
Lissu amewaeleza chama kimeanza ‘kukinukisha’ kwa walio tayari na watakwenda nao kwenye mapambano ya kudai mabadiliko, lakini kwa wanaofikiria kuingia katika uchaguzi, milango iko wazi kwenda kujaribu bahati yao sehemu nyingine.
“Tunafungua milango, nendeni mnakohitaji, lakini kama unataka kuwa mbunge makini twende tukapiganie mifumo huru ya uchaguzi. Kama unafikiri utakuwa mbunge Oktoba au Novemba 2025, sahau. Hiyo ni kweli,” amesema Lissu.
Lissu amewaeleza hata yeye alikuwa anafikiria urais lakini ndoto zake zimepotea na amesahau, akisema hata wanaofikiria udiwani wasahau kwani wanaenda kukinukisha.
“Tutaingia kwenye mapambano, tutaumia, lakini naamini mafanikio tutapata. Katika siasa za ukombozi na si za udalali, kukamatwa na kupelekwa mahakamani kwa sababu ya kupigania demokrasia ni kuvikwa taji la nishani ya dhahabu,” amesema.
Amesema kuna viongozi wengi walipitia mapito magumu ya kudai demokrasia lakini mwisho wa siku walipata mafanikio makubwa, hivyo hawataki kukata tamaa wala kurudi nyuma.
“Ni kweli msimamo wetu huu ni mgumu, hamu ni wabunge, tutachelewa kidogo lakini tutapata mageuzi yatakayotupeleka wengi zaidi bungeni. Watu wanataka tukapate asilimia tano na wabunge saba halafu tukapigane vikumbo, nani aende viti maalumu,” amesema.
Amesema hakuna chama kimewahi kuzungumza lugha hiyo ngumu, akiwataka wananchama wasiogope kwani tangu wameanza mikutano ya ‘No reforms, no election’ wanaungwa mkono na wananchi wengi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche amesema yeye na Lissu wanahitaji nafasi, lakini mazingira yaliyopo si rafiki kwao kuzipata, hivyo ni lazima wachukue hatua kwani hata viongozi wa dini wanazungumzia hilo.
“Ajenda ya ‘No reforms, no election’ si ya Chadema peke yake bali ni ajenda ya nchi nzima, anayepinga ajenda hii anania gani na unasema wewe ni Chadema. Maaskofu na masheikh wamesema kwani hatujawasikia? Mambo yamebadilika, nani anasimama na kusema tunaenda kwenye uchaguzi katika mazingira haya,” amehoji.
Heche amesema Watanzania wanahitaji uongozi mbadala na hauwezi kupatikana kwa njia ambazo haziheshimu kura za wananchi walio wengi wanaopatikana nje ya mfumo wa sanduku la kura.
“Kazi tuliyonayo tupeleke karatasi za ‘petition’ kutafuta saini za Watanzania, tukiondoka hapa watia nia tuchukue fomu twende kila jimbo, tunataka saini milioni 15 wanaosema uchaguzi kwa njia hii haiwezekani na hatukubali kuingia kwenye uchaguzi. Tutazikusanya na kuzipeleka kwenye taasisi zote duniani,” amesema.
Amesema baada ya kusambaza saini hizo kwenye taasisi, uchaguzi utakosa uhalali, akiwasisitiza wananchi wasiandikiwe bali waandike wenyewe.
“Wananchi wanajua uchaguzi unaibwa, Chadema tuko tayari kuongoza chama hiki kipate Tume Huru ya Uchaguzi zaidi ya hapo hatuwezi kuwa pamoja huo ni msimamo wa chama na mwenyekiti atazungumza na ni makubaliano,” amesema.
Kada wa Chadema, Selestine Simba amesema anaunga mkono msimamo huo kwa sababu wanapokwenda kwenye uchaguzi kama wagombea, kuna vitu vingi wanaweka rehani.
“Tunaweka rehani muda, tunawekeza fedha za kugharamia kampeni lakini tunaweka rehani uhai wetu, inakuwa ngumu unaingia kwenye uchaguzi ambao mifumo yake haitendi haki vitu vyote unapoteza na hutegemei kupata chochote,” amesema.
Amesema yeye ni mwathirika wa uchaguzi wa mwaka 2020 alifunga duka la nafaka, kwamba alikomba kila kitu kuwekeza kwenye kampeni za uchaguzi lakini hadi sasa hajafanikiwa kurejesha mtaji wowote.
“Tulishindwa katika mfumo ambao si halali ni kama tuliibiwa kura, kuna watu walitengeneza mazingira tushindwe na naunga mkono kwa asilimia 10 msimamo wa chama,” amesema.
Wakili Peter Madeleka amesema pamoja na kwamba alikuwa na ndoto ya kugombea ubunge baada ya kuona demokrasia ndani ya chama hicho imefikia uamuzi huo, hana budi kuzingatia hilo.
“Kila mwananchama na kiongozi anawajibika kusimamia msimamo wa chama uliopitishwa kwenye vikao halali hadi pale itakapoamuliwa vinginevyo kama mtia nia na mwana-Chadema, nasimamia kwenye ‘No reforms, no election,” amesema.
Kuhusu wanaopinga kampeni hiyo, Madeleka amesema hiyo ni taasisi kubwa ya kidemokrasia lazima wawepo baadhi wenye mtizamo tofauti na hiyo inaleta tafsiri sahihi.
“Kutamani kwenda mjengoni ni jambo moja, lakini uhakika kupitia mifumo iliyopo ni jambo lingine, unaweza kwenda mifumo ikawa mibaya na lile tamanio lako linaweza lisiwe na faida,” amesema.
Julius Mwita, aliyevuliwa uongozi katika nafasi ya Katibu wa Sekretarieti ya Chadema, ameweka wazi kwamba hapingani na ajenda ya kutaka mabadiliko, bali anapingana na mpango wa kuzuia uchaguzi, akisema ni jambo lisilowezekana.
Amesema hicho ndicho walichojadili katika kundi sogozi akiwa na wanachama wenzake (watia nia) ambao miongoni mwa mambo waliyokuwa wakijiuliza ni namna gani Chadema itaweza kuzuia uchaguzi wakati vyama vingine vimeshaanza maandalizi.
“No Reforms sawa, lakini ukianiambia No election… kwa wale mliobahitika kuona ‘screen shot’, maswali yangu yalikuwa ni haya, tutazuiaje uchaguzi? Kama mtu anaweza kunijibu sawa. CCM imeshaanza maandalizi, imeteua mgombea urais na mgombea mwenza na inaendelea kuwaanda wagombea ubunge na udiwani.
“Kama kuzuia tungeanza kuzuia uandikishaji kwanza, sasa unashindwa kuzuia halafu unasema ‘No election, how? (kwa vipi). Hakuna anayesema tunazuiaje uchaguzi, tunaambiwa tu ‘No Reforms, no Election,” amesema.
Msimamo wa Mwita unaungwa mkono na makada wengine waandamizi waliopo katika kundi la G55 la Chadema, wakiwemo vigogo ambao wanasema wanaunga mkono ‘No reforms’ lakini siyo kuzuia uchaguzi.
“Tunaona kuwa haiwezekani kuzuia uchaguzi kwa kuwa nje ya uchaguzi. Kujaribu uchaguzi huku tukiwa nje ya uchaguzi itakuwa ni sawa na kufanya jinai.
“Uwezekano pekee wa kuzuia uchaguzi ni kushiriki uchaguzi wenyewe kwa kuhakikisha tunaingiza wagombea katika uchaguzi. Ni rahisi kwa wagombea kuhamasisha na kuongoza wananchi kuzuia uchaguzi katika vituo mahususi vya uchaguzi, katika kata au majimbo yanayoelekea kufanyiwa hujuma kuliko kujaribu kuzuia uchaguzi wote, huku tukiwa nje kabisa ya uchaguzi wenyewe,” inaelezwa katika waraka wa makada hao walioutuma kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.
Wakati huohuo, vyama vya siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) vimeainisha changamoto zinazozorotesha mchakato wa kidemokrasia wakati wa uchaguzi, lengo likiwa ni kuingia meza ya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan.
Vyama hivyo ni Chadema, CCM, ACT-Wazalendo, CUF na NCCR-Mageuzi. Vimefikia makubaliano hayo wakati wa kikao cha TCD kilichofanyika jana Aprili 2, 2025 jijini Dar es Salaam chini ya mwenyekiti wake, Lissu.
Mbali ya Lissu, wengine waliohudhuria kikao hicho ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Stephen Wasira, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu na Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi (Bara), Joseph Selasini.
Vyama hivyo vimefikia uamuzi huo wakati kila kimoja kikiwa na msimamo wake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. ACT Wazalendo, NCCR-Mageuzi, na CUF vimeweka bayana kwamba vitashiriki uchaguzi mkuu, vikidai mageuzi kwenye mifumo ya uchaguzi.
Akizungumza na chombo kimoja cha habari baada ya kikao hicho, Lissu amesema walijadili masuala yote yanayohusu uchaguzi na Aprili 14, 2025 watakutana kuangalia mambo waliyokubaliana ili kwenda mbele.
Lissu ametaja miongoni mwa mambo yanayohitaji marekebisho ni yanayohusu muundo na majukumu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), majukumu yake, ulinzi wa makamishna na waangalizi wa uchaguzi.
“Haya tunayopendekeza yafanyiwe marekebisho, yanategemea utayari wa Serikali na unapozungumzia utayari wa Serikali unazungumzia utayari wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa hiyo, haya tuliyokubaliana tutapeleka kwa Rais kama sehemu ya mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuwezesha uchaguzi huru na wa haki,” amesema.
Lissu amesema marekebisho mengine ni kwenye mchakato wa uchaguzi, majimbo ya uchaguzi, haki ya kupiga kura, utaratibu wa upigaji kura, kampeni za uchaguzi na matumizi ya kanuni za maadili kama fimbo ya kuwachapa wagombea wa vyama vya upinzani.
“Tunapozungumzia Tume, tunaangalia wanaoteuliwa na Rais, tunachukulia wengine wote wanaosimamia uchaguzi kuanzia ngazi ya vijiji, hadi halmashauri. Tumezungumzia utaratibu mzima wa kufanya marekebisho ya mfumo wa uchaguzi,” amesema.
Selasini amesema katika mambo waliyoyaazimia kwenye kikao hicho, makatibu wakuu wa vyama vyote watakutana kuyapitia na kutengeneza nyaraka.
Baada ya hapo amesema viongozi kwa mara nyingine watakutana kujadiliana na kuomba kuonana na Rais Samia.
“Tutakutana naye kwa ajili ya kujadili mwelekeo wa uchaguzi unaokuja ili yale yanayolalamikiwa yashughulikiwe na Serikali.
“Changamoto tulizoeleza ni suala la uandikishaji mbaya hasa wanafunzi kushirikishwa kwenye uchaguzi, kura feki kuwepo vituoni, matumizi makubwa ya vyombo vya dola kwenye uchaguzi,” amesema.
Hayo hayatofautiani na anachoeleza Katibu Mkuu wa CUF, Husna Abdalla Mohammed anayesema walipendekeza uchaguzi uzingatie haki na kura za wananchi ziheshimiwe.
“Tuliorodhesha, ikiwemo kuenguliwa kwa wagombea wa vyama vya upinzani bila sababu za msingi, mawakala kutoapishwa au kutojaziwa fomu, washindi wa vyama vya upinzani kutotangazwa na wagombea kuwekewa nembo tofauti kwenye sanduku la kura wakati wa uchaguzi,” amesema.