Dereva Wa Lori La Mafuta Amuibia Bosi Wake Akidanganya Amepata Ajali -Video – Global Publishers

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia dereva aliyefahamika kwa jina la Ernest Okulo (40), mkazi wa Chanika, Dar es Salaam kwa tuhuma za kumuibia mwajiri wake mafuta ndoo 1,300 zenye ujazo wa lita 20 kila moja, zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 78.

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T785 CTC na trela namba T341 CTZ, aina ya Howo.

Kwa nyakati tofauti, aliuza mafuta hayo na alipofika eneo la Gwata, barabara ya Morogoro–Dar es Salaam, aliingiza gari vichakani na kudai kuwa amepata ajali na kuibiwa mzigo wote.

Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alifika katika Kituo cha Polisi Mikese kuripoti kuwa ameibiwa mzigo.

Hata hivyo, polisi walifika eneo la tukio na kuanza upelelezi, ambapo walibaini kuwa tukio hilo lilikuwa uongo na halina ukweli wowote.

Baada ya uchunguzi zaidi, polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine, Christina Elisha (44), mkazi wa Kibaha na kumkuta na ndoo 332 za mafuta hayo.

Pia, Utingo wa gari hilo, Ipyaba Odongo (29), alikamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Watuhumiwa wote watatu wanaendelea kuhojiwa na baada ya upelelezi kukamilika, watafikishwa mahakamani.

Related Posts