RAUNDI ya 24 ya Ligi Kuu Bara inaendelea Alhamisi hii kwa michezo mitatu kupigwa huku miwili ikiwa ya mapema kuanzia saa 10:00 jioni na mmoja saa 1:00 usiku.
Katika michezo hiyo ya leo, zinasakwa pointi za kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi hiyo kwani atakayepoteza kuna hatari ya kujiondoa kwenye malengo yake.
Kati ya timu zinazohitaji ushindi zaidi katika mechi hizi ni KenGold inayoshika nafasi ya mwisho ikiwa na pointi 16 na Kagera Sugar iliyopo nafasi ya 14 kabla ya mechi za Jumatano hii ikikusanya pointi 19. Kumbuka timu hizo zote zipo nyumbani.
Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar, wenyeji JKT Tanzania watacheza dhidi ya Dodoma.
JKT Tanzania yenye rekodi nzuri kwenye uwanja wake wa nyumbani msimu huu baada ya kupoteza mchezo mmoja tu kati ya tisa ya mashindano yote, inaikaribisha Dodoma Jiji ambayo haijashinda mechi yoyote ya ugenini kwenye ligi msimu huu.
Wenyeji wanahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kuendeleza rekodi yao nzuri nyumbani ambayo ilitibuliwa Februari 13 mwaka huu walipofungwa 1-0 na Singida Black Stars.

Mbali na hilo, JKT Tanzania inayoshika nafasi ya sita kwa pointi 30 kabla ya mechi za Jumatano hii, inazihitaji pointi tatu kuzidi kupaa nafasi za juu.
Kwa upande wa Dodoma Jiji wanahitaji ushindi kwa mambo mawili, kwanza kuondoa rekodi mbaya ya kutoshinda ugenini, pili kujisogeza nafasi za juu na kukimbia eneo la kushuka daraja.
Dodoma Jiji itashuka kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wa mwisho wa ligi kwa idadi kubwa ya mabao 6-0 dhidi ya Simba.
Kwa sasa Dodoma Jiji inakamata nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi kabla ya mechi za Jumatano hii ikiwa na pointi 27, ushindi kwake utaifanya timu hiyo kuifikia JKT Tanzania lakini itaendelea kuwa nyuma yake kwa tofauti ya mabao.
Rekodi zinaonyesha katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Dodoma Jiji ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Heritier Lulihoshi dakika ya 71 kwa penalti.

Kwa jumla, timu hizo zimekutana mara tano kwenye ligi, JKT Tanzania haijashinda zaidi ya kuambulia sare moja huku Dodoma Jiji ikiibuka na ushindi mara nne.
Ubabe huo wa Dodoma Jiji kwa JKT Tanzania, unadhihirisha mchezo huu utakuwa na ushindani mkubwa kwani mara ya mwisho kukutana uwanjani hapo wageni waliondoka na ushindi wa bao 1-0.
Mchezo mwingine utakaoanza saa 10:00 jioni utazikutaniza KenGold ambao ni wenyeji dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC.
KenGold wana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwenye mchezo huo ili kupambania harakati zao za kujinasua na janga la kushuka daraja.
KenGold ina mabadiliko makubwa ya uchezaji tangu ilipofanya usajili wa maana dirisha dogo lililofungwa Januari 15 mwaka huu ikiwaongeza nyota wengi wazoefu kama Kelvin Yondani, Obrey Chirwa na Zawadi Mauya. Kwenye mechi tano zilizopita wameambulia sare nne na ushindi mchezo mmoja.

Azam FC chini ya Kocha Rachid Taoussi, itahitaji kuendeleza wimbi la ushindi, ingawa itaendelea kusalia nafasi ya tatu kwani hata ikishinda itafikisha pointi 51 nyuma ya vinara Yanga wenye 58 na Simba 57, kwenye mechi tano zilizopita imeshinda mbili sare tatu.
Ubora wa Azam FC ni eneo la ushambuliaji kwani hadi sasa inashika nafasi ya tatu kwa kufunga idadi kubwa ya mabao (32) ikizidiwa na washindani wake waliopo juu, Yanga (58) na Simba ikifuatia kwa kutupia kambani mara 52.
Timu hizo zinakutana huku KenGold ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa idadi kubwa ya mabao 4-1 uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.
KenGold ambayo imepanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu huu, inaburuza mkia ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi 23.

Azam mechi tano za mwisho imeshinda mbili na sare tatu hali ambayo inawalazimu kushinda mchezo huu huku rekodi yao ya ugenini ikiwa si mbaya kufuatia kupoteza mbili pekee kati ya mechi 11 ikishinda tano na sare nne.
Huu ni mchezo mwingine utakaopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Timu hizi zimekuwa zikikutana kwenye mashindano tofauti kwa muda mrefu huku mara ya mwisho Coastal Union ikiwa nyumbani iliichapa Kagera Sugar bao 1-0 lililofungwa na Semfuko Charles dakika ya 86.
Mbali na hilo, Coastal Union ni wababe wa Kagera Sugar kwani mara ya mwisho walipoenda Kaitaba pia walishinda 2-1 huku mechi tano za mwisho baina yao, Kagera Sugar imeambulia sare moja pekee na kupoteza nne.
Kagera Sugar iliyotoka kuichapa Tabora United kwa penalti 5-4 kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA), ina mzuka wa kuendeleza wimbi la ushindi chini ya kocha Juma Kaseja ambaye tangu amekabidhiwa kikosi hicho Machi 4, 2025 ameshinda mechi zote mbili dhidi ya Pamba Jiji (2-1) kwenye ligi na Tabora United (FA).
Kaseja ana kazi ya kufanya kuipambania Kagera kutoka kwenye eneo baya kwenye msimamo kwani hivi sasa inashika nafasi ya 14 ikikusanya pointi 19.
Coastal Union inayofundishwa na Juma Mwambusi, mchezo wa mwisho wa ligi imetoka suluhu dhidi ya Dodoma Jiji, baada ya hapo ikaenda kufungwa 3-1 na Yanga katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) na kutupwa nje ya mashindano hayo ambayo wapinzani wao Kagera Sugar wamesonga mbele robo fainali.
Pointi 25 ilizo nazo Coastal Union, zinawafanya kuhitaji ushindi katika mchezo huu kwani nayo haina uhakika wa kubaki kwenye ligi.
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmed Ally amesema hawataingia na rekodi kuikabili Dodoma Jiji kwasababu rekodi zinaandikwa ili zivunjwe, hivyo wamejiandaa kupambania pointi tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo.
“Tunaiheshimu Dodoma Jiji ni timu nzuri na ina wachezaji wengi wazuri, tumejiandaa kwaajili ya kubakiza pointi tatu nyumbani na tunatarajia mchezo mzuri na wa ushindani,” amesema Ally.
Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime amesema hautakuwa mchezo rahisi dhidi ya JKT Tanzania, wamejiandaa kushindana na kusaka pointi tatu ambazo zitawapa nguvu za kuwa bora zaidi katika michezo ijayo baada ya kutoka kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao.
Naye kocha wa Kagera Sugar, Kaseja amesema timu yake ipo kwenye morali nzuri ya ushindani na wanatambua umuhimu wa mchezo ulio mbele yao huku akiweka wazi kuwa kila mchezo kwao ni fainali kutokana na kusaka nafasi ya kusalia katika Ligi Kuu kwa msimu ujao.
“Hatuna mchezo rahisi, mechi zote zilizobaki kwetu ni fainali tunatafuta matokeo ambayo yatatupa nafasi ya kucheza ligi msimu ujao, wachezaji wanatambua umuhimu wa pointi tatu na hilo limefanyiwa kazi kwenye uwanja wa mazoezi, dakika 90 zitaamua,” amesema Kaseja ambaye awali alikuwa kocha wa makipa wa kikosi hicho.
Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi amesema wanaingia kucheza na timu ambayo inahitaji matokeo mazuri huku akikiri imeimarika kwa kiasi kikubwa hivyo wamejiandaa kuhakikisha wanaepuka kuruhusu mabao na kutumia kila nafasi ambayo wataitengeneza ili kujiimarisha zaidi katika nafasi waliyopo.
“KenGold licha ya kuwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo, ina wachezaji wazuri ambao ili kuwapa wakati mgumu tunahitaji kuwa imara kitu ambacho tayari nimekifanyia kazi na naamini dakika 90 zitaamua nani bora zaidi ya mwingine,” amesema Taoussi.
Omary Kapilima, kocha wa KenGold, amesema wamefanya kila kinachowezekana kuhakikisha pointi tatu dhidi ya Azam FC zinabaki Mbeya huku akiweka wazi kuwa haitakuwa rahisi lakini wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na akili moja tu ya kupata pointi tatu.
“Hatuna matokeo mazuri nyumbani, lakini hilo haliondoi kujiandaa vizuri ili kuweza kupata matokeo bora kitu ambacho tumekifanya na tunaamini dakika 90 zitakuwa upande wetu,” amesema kocha huyo.