Saba wafariki dunia ajali ya basi Mwanga, 32 wajeruhiwa

Mwanga. Watu Saba wamefariki dunia papo hapo huku wengine 32 wakijeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Mvungi, walilokuwa wakisafiria kupinduka katika eneo la Kijiji cha Mamba, Kata ya Msangeni, Tarafa ya Ugweno, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Kamanda ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo,  ambapo amesema ajali hiyo imetokea leo Alhamisi saa moja asubuhi, ambapo basi hilo lilikuwa likitoka Ugweno kwenda mkoani Dar es salaam.

Amesema waliofariki katika ajali hiyo ni wanawake watatu akiwemo mtoto mdogo  na wanaume wanne.

“Ajali imetokea kijiji cha Mamba,  kata ya Msangeni, tarafa Ugweno, watu Saba wamefariki dunia wakiwemo wanawake watatu na wanaume wanne,”amesema Mkomagi

Ajali hiyo imetokea ikiwa zimepita siku nne  tangu itokee ajali nyingine Machi  30,2025 iliyoua watu saba kwa matukio mawili tofauti wilayani Same, ikiwemo iliyoua wanakwaya sita wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mmeni Chome,  Dayosisi ya Pare  iliyotokea  katika milima ya Pare  baada ya gari walikuwa wakisafiria kupinduka katika milima hiyo.

Akizungumzia tukio hilo la ajali, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema  chanzo cha ajali hiyo ni  basi hilo lilikuwa likijaribu kupishana na gari jingine na ndipo lilipoteleza kwenye tope na kupindika.

Basi la mvungi likiwa limeanguka na kusababisha vifo vya watu Saba na majerahi 32.

“Ajali imetokea saa 1:30 asubuhi ya leo, likihusisha basi la Mvungi, limeanguka na  kutumbukia bondeni na mpaka sasa kwa taarifa za awali vifo ni saba na majeruhi wameshawahishwa katika Hospitali za KCMC, Mawenzi na Usangi kwa  ajili ya matibabu,”amesema RC  Babu.

Ameongeza: “Kule ni milimani, barabara yetu ni ya lami lakini kulikuwa na magari mengine ambayo yalikuwa yamesimama, moja limebeba mwili linapandisha juu mlimani, lakini wakati anajaribu kulipita hilo gari lililoharibika, kuna lingine lilikuwa linakuja kwa mbele, akaona wapishane na yule mwenye gari dogo hivyo  likaingia pembeni ya barabara kutokana na mvua zinazoendelea eneo hilo kulikuwa na matope likateleza na kupinduka “amesema RC Babu.

Aidha, RC Babu amesema kwa sasa bado wanaendelea kufuatilia tukio hilo la ajali na taarifa kamili itatolewa hapo baadaye.

Related Posts