Serikali kuanza ujenzi SGR ya Jiji la Dar, Dodoma

Morogoro. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, amesema Serikali ipo mbioni kuanza ujenzi wa reli ya Jiji la Dar es Salaam (Commuter Rail Network – CRN) ili kuboresha mfumo wa usafiri wa umma katika jiji hilo.

Akizungumza leo Aprili 3, 2025, wakati wa semina ya menejimenti ya TRC na waandishi wa habari inayofanyika mkoani Morogoro, amesema hatua za upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa mradi huo tayari zimekamilika.

Kadogosa amesema CRN itakuwa mtandao wa reli wa mijini utakaowezesha abiria kusafiri kwa urahisi kati ya maeneo ya katikati ya jiji na pembezoni, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa magari na muda wa safari kwa wakazi wa Dar es Salaam.

“Kwa hiyo, reli ya Dar es Salaam ni lazima. Uwekezaji huu utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Kadogosa.

Amebainisha kuwa Serikali inaendelea na hatua za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, huku ikitarajia kuutekeleza kwa mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

“Tayari kampuni mbalimbali zimeonesha nia ya kushiriki katika ujenzi wa reli hii,” amesema.

Kadogosa pia ameeleza kuwa, pamoja na Dar es Salaam, mpango wa ujenzi wa reli ya mijini unatarajiwa kuanza pia jijini Dodoma ili kusaidia kuimarisha usafiri wa wakazi wa mji huo mkuu wa Tanzania.

“Kama nilivyosema tunajenga treni ya Dar es Salaam na baada ya ile ya Dodoma tunaenda Mbeya na Mwanza,” amesema Kadogosa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Miundombinu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, amesema kwa kuzingatia jiografia ya Dar es Salaam, mradi huo utajumuisha treni za juu, ardhini na zile za chini ya ardhi.

Related Posts