Kyiv. Jeshi la Russia limetekeleza mashambulizi ya anga kwa kutumia ndege zisizo na rubani (droni) na kombola la ‘balistiki’ katika Mji wa Kryvyri nchini Ukraine na kusababisha vifo vya watu wanne, huku 14 wakijeruhiwa.
Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa mashambulizi hayo ya Russia nchini Ukraine yametekelezwa usiku kucha wa kuamkia leo Alhamisi Aprili 3,2025.
Mbali na kusababisha vifo na majeruhi mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu nchini Ukraine.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Utawala wa kijeshi wa Mkoa wa Dnipropetrovsk, nchini Ukraine, Serhiy Lysak imesema mashambulizi hayo yalianza jana saa 11:20 jioni ambapo shambulio moja lililenga moja ya viwanda vya jiji hilo.
“Tunaendelea kuthibitisha taarifa. hatari bado ipo. Tafadhali baki mahali salama hadi tahadhari ya mashambulizi ya angani itakapomalizika,” imeeleza taarifa ya Lysak.
Dakika chache baadaye, alitangaza kuwa kwa mujibu wa taarifa za awali, watu wanne walikufa kutokana na shambulio la Russia katika eneo la Kryvyi Rih, huku wengine watatu wakijeruhiwa.
“Wote wanapatiwa matibabu. Madaktari wanasema hali zao ni za wastani,” amesema Lysak.
Kulingana na taarifa hiyo, shambulio hilo lilisababisha moto jijini Dnipropetrovisk.
Jana saa 11:40 jioni, Mkuu wa Baraza la Ulinzi la Kryvyi Rih, Oleksandr Vilkul, aliripoti kuwa Russia ilishambulia kituo cha miundombinu ya kiraia kwa kombora la balistiki.
“Operesheni ya uokoaji inaendelea. Kuna moto mkubwa,” alisema Vilkul huku akisisitiza kuwa majengo ya makazi ya ghorofa nyingi yaliharibiwa.
“Miongoni mwa waliojeruhiwa ni mwanamke mwenye umri wa miaka 29 na wanaume wenye umri wa miaka 35 na 41. Wote wamelazwa hospitalini,” alisema Serhiy Lysak.
Kufikia jana saa 12:30 jioni, iliripotiwa kuwa watu tisa walikuwa wamejeruhiwa kutokana na shambulio hilo la kombora. Wote walikuwa katika hali ya wastani.

Baadaye, Serhiy Lysak aliripoti kuwa jumla ya watu 10 waliokuwa wamejeruhiwa walikuwa hospitalini, huku wawili wakipatiwa huduma ya kwanza eneo la tukio.
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni mvulana mwenye miaka minane, ambaye alilazwa hospitalini akiwa katika hali ya wastani.
Baadaye, iliripotiwa kuwa msichana wa miaka sita pia alijeruhiwa Kryvyi Rih, ambapo alipatiwa matibabu eneo la tukio.
“Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa mpya, mvulana huyo wa miaka minane yupo katika hali mbaya na amelazwa kwenye kitengo cha dharura cha majeraha. Madaktari wapo karibu naye na wanafanya kila linalohitajika,” alisema mkuu wa utawala wa kijeshi wa mkoa.
Ilipofika Saa 1:13 usiku, mkuu wa utawala huo aliripoti kuwa maofisa wa zimamoto walikuwa wakipambana kuzima moto uliosababishwa na shambulio hilo.
Akizungumzia shambulizi hilo, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, alisema: “Kote ulimwenguni, mashambulizi kama haya huitwa jina moja, ugaidi. Njia pekee ya kuyakomesha ni kwa kuiwekea shinikizo la kutosha ili kulazimisha mfumo wa Russia kuachana na vita na ugaidi. Hili linategemea washirika wetu Marekani, Ulaya na mataifa mengine ulimwenguni.”
“Kitu pekee kinachotutenganisha na kusitisha mashambulizi haya kikamilifu na bila masharti ni ukosefu wa makubaliano ya Russia kusimamisha vita. Ni shinikizo la kimataifa pekee linaloweza kuhakikisha makubaliano kama hayo,” alisema.
Aliongeza kuwa mashambulizi hayo ya Russia yanathibitisha kuwa Ukraine inahitaji mifumo ya kutosha ya ulinzi wa anga na makombora ili kulinda watu wote dhidi ya ugaidi wa Russia.
Mnamo Machi 29, 2025, Jeshi la Russia lilishambulia Kryvyi Rih kwa kombora la balistiki. Kutokana na shambulio hilo, angalau watu wanane walijeruhiwa, na miundombinu iliharibiwa.
Bado jitihada za Marekani kupata mwafaka wa mzozo huo hazijazaa matunda baada ya kila upande kurushiana mpira kwa madai ya kukiuka makubaliano ya usitishwaji mapigano wa hiari kwa siku 30.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.