Dodoma. Mfumo unaotumia Akili Unde (AI), utakaomwezesha mtu kujipima na kubaini changamoto za afya akili kwa kutumia simu au kompyuta na kisha kupata ushauri wa kitaalamu, utazinduliwa Juni mwaka huu.
Katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/23, alisema utambuzi wa wagonjwa unaofanywa unalenga zaidi watumiaji wa dawa za kulevya, wazee, walemavu na waliopata mimba na wanaoishi katika mazingira magumu.
Alisema utambuzi huo, unapuuza wengine hali ambayo inayotokana na upungufu wa wataalamu ngazi ya jamii kwenye vijiji na mitaa.
Akizungumza Mwananchi, leo Alhamisi, Aprili 3, 2025, Mratibu wa Mradi wa Afrial Lab na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Salim Diwani amesema utafiti huo umefanyika kwa zaidi ya miaka miwili.
Amesema takwimu zilizotumika ni za Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam huku wakitegemea kuufanya pia katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili ya Mirembe na Benjamin Mkapa (Dodoma) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Dar es Salaam).
“Lazima mtu anayetaka kujipima awe na smart phone (simu janja) na application (APP) ili aweze kujipima mwenyewe afya ya akili,”amesema Dk Diwani.
Naye Kaimu rais wa Ndaki ya Sayansi za Ardhi na Uhandisi wa Udom, Profesa Godlisten Kombe akizungumza katika siku ya Ukubalifu Jumuishi na Akili Unde, amesema mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa Juni mwaka huu.
Amesema baada ya mtumiaji kufahamu hali yake ya kiafya, ataweza kuchukua hatua za kuonana na daktari wa masuala ya afya ya akili, hivyo kuokoa muda ambao angetumia kufahamu kama ana changamoto ya afya ya akili au hana.
Mmoja wa wanafunzi wa Udom, Adela Noel ameelezea umuhimu wa akili unde kwenye masuala mbalimbali na kuwa yeye imemsaidia kwenye masuala ya elimu anapojisomea.