Baada ya kushindwa kumaliza mashindano ya Kimataifa ya gofu ya wanawake nchini Afrika Kusini mwezi Februari mwa mwaka huu, Vicky Elias amepania kufuta makosa yake katika mashindano ya wazi ya wanawake yanayoanza kesho jijini Nairobi, Kenya.
Viwanja vya Ruiru katika viunga vya Narobi ndiyo shuhuda wa michuano hii ya kimataifa ya Wanawake ambayo yatachezwa kwa siku tatu yakishirikisha mashimo 54, kwa mujibu wa waandaji, Chama Cha Gofu ya Wanawake cha Kenya (KLGU).
Vicky anakuwa Mtanzania wa pili baada ya Madina Iddi wa Arusha ambaye alithibitisha ushiriki wake wiki mili zilizopita.
“Nimefanya mazoezi ya kutosha kwa ajili ya mashindano haya kwa sababu yana pointi za ubora kutoka Chama cha Gofu Duniani. Naamini mambo yatakuwa mazuri safari hii kwa sababu viwanja vya Kenya tumevizoea,” alisema Vicky kabla ya kuondoka siku ya Jumatano kwa safari ya Nairobi.
Mashindano haya ya siku tatu yatakayojumuisha mashimo 54, yataanza rasmi kesho Aprili 4 na kumalizika siku ya Jumapili, Aprili 6 na yatashirikisha wacheza gofu wanawake kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
“Ni mimi na Madina tu ndiyo tutashiriki mashindano haya hakuna mwingine zaidi aliyeonyesha nia ya kwenda nchini Kenya kwa ajili ya mashindano haya,” aliongeza Vicky ambaye anatokea klabu ya Dar es Salaam Gymkhana.
Kwa mujibu wa waandaji KLGU, Machi 31 mwaka huu ilikuwa ndiyo tarehe ya mwisho ya kujiandikisha kabla ya mashindano kuanza kutifua nyasi siku ya Ijumaa.
Madina anarudi tena nchini Kenya baada kushiriki mashindano ya wazi ya wanawake katika viwanja vya Muthaiga, ambayo anasema hakuweza kucheza vizuri kiasi cha kushindwa kucheza (make cut) fainali.
“Nitakuwa barabara kwa ajili ya michuano ya Kenya Ladies Open ya Ruiru kwa sababu mfungo wa mwezi wa Ramadhan utakuwa umekwisha,” alisema Madina na kuwaomba radhi washabiki wake kwa kutofanya vizuri katika michuano ya wanawake ya Muthaiga.
Vicky na Madina waliufungua utepe wa mashindano ya kimataifa kwa mwaka 2025 kwa kushiriki katika mashindano ya gofu ya wanawake yaliyochezwa Afrika Kusini yakijulikana kama African Women Invitational Golf.
Mashindano haya ya hadhi ya kimataifa yalifanyika kuanzia Februari 5 hadi 7 mwaka huu kwenye viwanja vya Leopard Creek mjini Mpumalanga.
Wote wawili wanaamini mashindano ya Kenya Ladies Open yatawapa mafanikio mazuri endapo wataongeza jitihada.