Arusha. Simanzi na vilio vimeibuka nje ya Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, baada ya majibu ya vinasaba (DNA) kutolewa na kuonyesha kuwa mkazi wa Mtaa wa Ndarvoi, Kata ya Daraja Mbili, Neema Kilugala (26), aliyedai kubadilishiwa mtoto, siyo ya kweli na kuwa mtoto aliyepewa (ambaye kwa sasa amefariki dunia) ndiye wa kwake.
Vilio hivyo kutoka kwa Neema na mama yake (Sabrina Andrew), vimesababishwa na majibu hayo ya DNA ambapo bado wameendelea kusisitiza mtoto huyo siyo wa kwao.
Majibu ya DNA, yaliyotolewa leo Alhamisi Aprili 3, 2025, yalionyesha kuwa kati ya wazazi watatu waliojifungua katika hospitali ya Mount Meru kwa wakati mmoja, majibu ya vinasaba yalifananisha mtoto aliyepewa na Neema kwa asilimia 99.99, ingawa mtoto huyo alifariki dunia kabla ya majibu kutolewa.
Hata hivyo, Neema amesisitiza kuwa bado anakataa matokeo hayo na kuomba msaada kutoka kwa Serikali ili apate mtoto wake.

Ofisa Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Geoge Onyango
Akizungumza nje ya Kituo hicho cha Polisi, Neema amesema hajakubaliana na majibu hayo na kuomba Serikali kumsaidia kupata haki yake ili ampate mtoto wake.
“Wanatuambia yule mtoto waliyetubadilishia ni mtoto wangu, ila mimi sijakubaliana nao mtoto wangu najua yupo na amebadilishwa, naomba mtusaidie katika hili nipate mtoto wangu,” amesema.
Ofisa Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, George Onyango amesema awali majibu hayo ya DNA yalikuwa yatolewe mchana ila ikashindikana kutokana na wazazi wa watoto wengine wawili waliochukuliwa sampuli kwa ajili ya vipimo hivyo kutokuwepo.
“Yule mtoto ambaye mama analalamika siyo wa kwake bahati mbaya alishafariki na vipimo vimeonyesha kwamba kuna uhusiano mkubwa wa kisampuli ambao ni asilimia 99.99 na huyo mzazi aliyelalamika.
“Wale watoto wengine wawili ukiacha huyo aliyefariki, majibu yameonyesha kwa asilimia 99.99 kwamba wanafanana na mama zao wazazi. Barua ya majibu ya DNA yalielekezwa kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arusha, ila tumesomewa wazi na ufafanuzi umetolewa,” amesema.
Amesema wamewaelekeza kuwa kwa kuwa majibu hayo yametoka kwenye ofisi yenye mamlaka kisheria, kama kuna mtu hajaridhika na majibu hayo afuate hatua za kisheria kulalamika au kudai haki yake nyingine.
Makamu wa Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), Jane Bararukuliliza, amesema baada ya kuona taarifa kuhusu changamoto hiyo iliyojitokeza hospitali ya Mount Meru, wamechukua jukumu kama chama kufuatilia suala hilo .
“Sisi ni chama cha kitaaluma tunafuatilia utendaji kazi wa wauguzi na mazingira wanakofanyia kazi, changamoto wanazokabiliana nazo katika kazi zile, tuliposikia taarifa hizo ilibidi tufike eneo la tukio kuona hali halisi na tulikuwa ujumbe wa watu 10,” amesema.
Makamu huyo amesema majibu hayo ya vinasaba yalisomwa mbele ya pande zote na vilichunguzwa kwa kuangalia maeneo 15 na kila eneo kutoka kwa watoto hao watatu pamoja na mama watatu waliokuwa wamejifungua.
“Mwisho kabisa aliitwa aliyechukua sampuli zile akatoa taarifa za sampuli kama sampuli A iliyotoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, sampuli A alikuwa ni nani, B alikuwa ni nani na C alikuwa nani na kwa hiyo mama fulani ‘amemachi’ na sampuli A, B na C na asilimia ngapi.
“Wadau wote waliokuwa pale walisikia mama yupi ameoanisha matokeo ya sampuli zile kwa asilimia 99.99 iliyothibitisha huyu na huyu wameoanisha vinasaba vyao.
“Kwenye tukio linalozunguka mtandaoni yule mama (Neema) alikuwa anakataa kwamba mtoto aliyepewa si wa kwake ila ikathibitika kwamba yule mtoto ni wa kwake na watoto wengine wakathibitika ni wa mama zao,” amesema.
Makamu huyo bila kuwataja majina wazazi hao wengine amesema Serikali imeshauri kama mtu hajaridhika anaweza kuendelea kuchukua hatua na kuwataka wauguzi kuendelea kutoa huduma vizuri kwa wananchi.
“Nichukue nafasi hii kumpa pole muuguzi mwenzetu ambaye alitoa ile huduma na ikaleta changamoto kama wananchi walivyokuwa wanafirikia, sisi kama wauguzi hatulali unapokuwa na mteja ambaye umempa huduma na hajaridhika nayo inasononesha mioyo yetu sana na hatuwi na furaha hata kidogo.
“Nimpe pole na wauguzi wengine ambao wameguswa na tukio hilo, ni kweli Glory ambaye ndiye muuguzi aliyetoa huduma, mtoto aliyempeleka kwa Neema ndiye alikuwa mtoto wake, pamoja na kwamba baada ya muda yule mtoto alipoteza maisha,” ameongeza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo jana, na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Roida Andusamile ameeleza uchunguzi ukikamilika taarifa rasmi zitatolewa na hatua stahiki zitachukuliwa.
Juzi Neema alidai baada ya kufanyiwa upasuaji alifanikiwa kumuona mtoto wake na muuguzi alimjulisha kuwa mtoto ni mzima na yuko mwenye afya njema akiwa na uzito wa kilo 3.1.
“Baada ya kuambiwa hivyo na kumuona nilimshukuru Mungu na wakanipeleka chumba cha kupumzika, kabla ya saa saba kuletewa mtoto huku amefungwa vitenge ambavyo si vya kwangu.
“Nilishangaa sana nikamwambia mama mbona huyu mtoto ana vitenge si vya kwangu? Ndio mama naye kuangalia na kwenda kumwita nesi aliyemleta mtoto akaja kumchukua,” amesema.
Neema anasema kuwa baada ya nesi kumchukua mtoto yule huo ndio ukawa mwisho wa kumuona hadi kupewa taarifa za kifo cha mtoto wake.
“Sijui kilichotokea huko maana walirudi bila mtoto huku nikiambiwa amehifadhiwa chumba cha joto nikauliza chumba cha joto vipi wakati mtoto wangu hakuwa na shida yoyote ndio wakaendelea kunizungusha kuwa watanipa kesho yake niache apumzike ila yupo vizuri.
“Asubuhi naitwa kwenda kumuona mtoto nashangaa naonyeshwa mtoto ambaye sio yule mtoto wangu, kwa sababu tumemkuta anaumwa na nimeambiwa ana shida ya moyo kuwa mkubwa.
“Mtoto wangu wamemchukua na kwa vile tu nilifanyiwa operesheni kwa sababu wasingemchukua mtoto wangu, Mimi namtaka tu mtoto wangu mwenye kilo 3.1 na mweupe tena alama mikononi kama yangu, si huyu mweusi mwenye kilo 2.285 tena ana matatizo ya moyo kuwa mkubwa” amesema Neema.