Dar es Salaam. Teknolojia inaendelea kukua katika sekta ya uvuvi, na sasa biashara ya samaki na mazao yake inaweza kufanywa kidijitali kupitia mfumo wa Vua Uza na Nunua Samaki Kidijitali wa PFZ.
Mfumo huu wa programu tumizi unawawezesha wavuvi kupata taarifa muhimu kama vile hali ya hewa, maeneo yenye wingi wa samaki wa aina fulani, pamoja na fursa ya kuuza na kununua samaki na mazao yao kwa njia rahisi na ya kisasa.
Mfumo huu utasaidia kuboresha shughuli za uvuvi na kuongeza tija katika sekta hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 03,2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Edwin Mhede wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfumo huo unaolenga kuongeza tija katika shughuli za uvuvi.
Mdehe amesema kupitia mfumo huo mvuvi atapata uhakika wa soko, kuokoa muda na gharama.
Pia, kuchukua tahadhari zote muhimu kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Amesema pia itamsaidia mvuvi kuepukana na uvuvi wa kubahatisha kutokana na kuwa na taarifa kuhusu maeneo yanayopatikana samaki kwa wingi kulingana na aina anayoihitaji.
“Mfumo huu utawawezesha wavuvi kuuza mazao yao moja kwa moja kwa wanunuzi kupitia njia ya PFZ kidijitali, bila ya kulazimika kupitia madalali au kupoteza muda sokoni,” amesema.
Amewataka waendeshaji wa mfumo huo kuufungamanisha na mifumo mingine zaidi ili kuwezesha upatikanaji wa huduma zote muhimu kwa wafanyabiashara na wanunuzi wa samaki pamoja na mazao yake.
“Mfumo huu ukifungamanishwa na mifumo mingine ikiwemo ile ya kifedha itasaidia hata wafanyabiashara kutunza taarifa zao za mauzo na hata kupata mikopo kwa urahisi,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania, Dk Ismael Kimirei amesema mfumo huo ni matokeo ya utafiti uliofanywa kwa takribani miaka saba na kubaini baadhi ya changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa samaki.
Kimirei amesema mfumo huo utakwenda kuwapa urahisi wa ufanyaji wa bishara na kupelekea kuimarisha sekta ya uvuvi na kukuza uchumi wa buluu.
Amesema kwa kipindi cha miezi mitatu ya majaribio ya mfumo huo iliyoanza Januari 2025, watu takribani 915 wameshajiunga ambapo kati yao asilimia 75 ni wavuvi na 25 ni wafanyabiashara wa mazao ya samaki.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ametaka elimu kuendelea kutolewa kwa wavuvi na wafanyabiashara ili waweze kuufahamu vyema mfumo huo, namna unavyofanya kazi na faida zake.