WANADIPLOMASIA KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII NCHINI.


Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeandaa ziara maalum kwa Jumuiya ya
wanadiplomasia nchini kutembelea vivutio vya utalii kwa madhumuni ya kutangaza
sekta ya utalii nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Said Shaib Mussa aliwambia waandishi habari kuwa ziara hiyo
itakayofanyika kuanzia Aprili 11 hadi 15, 2025 ni utekelezaji wa mpango wa
Serikali wa kuitangaza Tanzania kama kituo bora cha utalii na uwekezaji
duniani.

Katika ziara hiyo wanadiplomasia hao watapata fursa ya kutembelea Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro na visiwa vya Zanzibar ambavyo
vimebarikiwa kuwa na fukwe nzuri na bora duniani.

Wakiwa Zanzibar wanadiplomasia hao watapata fursa ya kushiriki hafla ya chakula
cha jioni itakayoandaliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambapo tuzo ya Rais ya Utalii
itatolewa ikiwa ni sehemu ya kusherehekea uhusiano wa karibu kati ya Tanzania
na Jumuiya ya Kimataifa.

Balozi Mussa alieleza kuwa kupitia ziara hiyo, makala fupi na filamu za utaliii
zitaandaliwa na kugaiwa kwa wanadiplomasia ili wazitumie kutangaza vivutio vya
utalii kupitia majukwaa mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari vya nchi zao.

Balozi Mussa aliongeza kuwa mpango huo unaotarajiwa kuongeza idadi ya watalii, kukuza
uchumi na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia unatekelezwa kwa ushirikiano
baina ya Wizara na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, wakiwemo Bodi ya Utalii
Tanzania (TTB), Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT) na kampuni binafsi
zinazohusika na biashara ya utalii.

Related Posts