Nyasa. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amekula ‘kiapo’ mbele ya wananchi wa Ruvuma kwamba atakuwa mwaminifu na mweledi kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan na kamwe:”Sitawaangusha, sitamuangusha.”
Dk Nchimbi amesema Rais Samia amempa heshima kubwa yeye binafsi na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kumpendekeza kisha mkutano mkuu wa CCM ukampitisha kuwa mgombea mwenza wa urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mkutano mkuu wa CCM wa Januari 18-19, 2025 uliofanyika jijini Dodoma, pamoja na mambo mengi uliwapitisha Rais Samia kuwa mgombea urais, Rais Hussein Mwinyi kuwa mgombea urais wa Zanzibar na Dk Nchimbi kuwa mgombea mwenza.

Dk Nchimbi ambaye yupo ziarani mkoani Ruvuma ambako ni nyumbani kwao na ikiwa ni ziara ya kwanza tangu kuwa mgombea mwenza mteule wa urais, wanachama na wana-CCM wamekuwa wakimpongeza kwa hatua hiyo wakiwemo wabunge wa mkoa huo.
Leo Jumamosi, Aprili 5, 2025, Dk Nchimbi akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi ya Mbamba Bay, Wilaya ya Nyanza ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia kwa heshima aliyompa.
“Natambua heshima kubwa aliyonipa mimi na watu wa Ruvuma, Mungu akijaalia tukamaliza uchaguzi, nitamsaidia Rais kwa uaminifu mkubwa, nitaitumikia nchi kwa uaminifu nisimuaibishe Rais wetu, nisiwaaibishe wananchi wa Ruvuma,” amesema Dk Nchimbi huku akishangiliwa.
“Nimeamua kuyasema hapa nikiwa Ruvuma. Rais wetu ametoa heshima anajibiwa kwa heshima.”
Dk Nchimbi anakuwa mgombea mwenza baada ya Rais Samia kuuleza mkutano mkuu kwamba Dk Philip Mpango ambaye kwa sasa ni makamu wa Rais aliomba kupumzika.
Dk Mpango mwenyewe katika moja ya mikutano alisema ameamua kuomba kupumzika wadhifa huo aliohudumu kwa miaka minne baada ya kutumikia nafasi mbalimbali ndani na nje ya Serikali, hivyo anahitaji kupumzika ili kupisha wengine.
Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amesema chama hicho kipo imara na kiko tayari kwa uchaguzi na kiwaomba wananchi wakati ukifika wakichague kwa kura nyingi ili kiendelee kuwatumikia na kuwapelekea maendeleo.
“Hakuna eneo Ruvuma ambalo halijaguswa na miradi ya maendeleo. Serikali ya Rais Samia inajali maisha ya wananchi, hatutaki viongozi wanawaza maisha yao tunataka wanaojali maisha ya wananchi,” amesema.

“Viongozi na wanachama wa CCM wanawajibu wa kuhakikisha chama hakitoki katika misingi ya kuundwa kwake ambayo ni kutetea wananchi, kusimamia amani, kutounga mkono uonevu kila mweye shida kuona faraja ya kukimbilia.
“Yoyote anayeona raha kunyanyasa raia, kuchonganisha wananchi, weye kuona raha kudhulumu Chama Cha Mapinduzi siyo mahala pake, CCM ni mahala pa watu wenye kutaka kujenga nchi yao chama hiki ni cha wanachama malengo makini kutumikia wananchi,” amesema.
Mtendaji mkuu huyo wa CCM amesema: “Chama siyo cha viongozi ni cha wanachama kura za maoni wabunge, madiwani wanaCCM wachague wanaokubalika, wachague watakaokwenda na mbio za maendeleo, msione aibu katika kuchagua. CCM italeta wagombea wazuri kwenye ngazi zote, tutashinda kwa kishindo.”
Katika mkutano huo, Dk Nchimbi ametoa fursa kwa wananchi kutoa kero zao mbalimbali na moja ya changamoto iliyoelezwa ni ujenzi wa barabara ya Mbamba Bay kwenda Lutui ambayo wananchi walishangilia zaidi.
Baada ya mwananchi huyo kumaliza kutoa kero hiyo na kushangiliwa, Dk Nchimbi akasema:”Huyu ametisha kuliko wote siyo?” Nao wakaitikia ndiyoooooo naye akawajibu tutalizungumza.
Katika kulizungumzia hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Ruvuma, Salehe Mkwama amesema ni kweli kero hiyo ya barabara wanaifahamu, “hii barabara ni ya muhimu si kwa wananchi tu hata sisi wenyewe na imeanza kujengwa mkandarasi yupo anaendelea.”
Amesema ikikamilika (hakusemi lini) itagharimu Sh95 bilioni akidokeza kwamba ujenzi wa madaraja unaendelea.
Katika kusisitiza hilo, Dk Nchimbi amesema, “kama Mungu akitupa uzima, tukachaguliwa, hivi kweli tukalala, tukaamka, Makamu wa Rais Dk Nchimbi kweli hizi kilomita 40 tutashindwa kweli? Kama hizi hela hazipo kwa makamu wa Rais, nitakwenda kwa mheshimiwa Rais kumwomba. Kwa hiyo hilo msiwazeeee.”
Kero za ukosefu wa maji katika Shule ya Msingi Muungano na ukamilishaji wa boma la Shule ya msingi Kitungi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa, Khalid Khalif Amir amesema halmashauri hiyo imeshafanya mchakato wa kufunga maji na hii inafanyika baada ya ziara hiyo kumalizika.
Kuhusu kero za umeme kwa baadhi ya maeneo kutokuwapo ikiwemo taasisi za umma, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali inatambua hilo na tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji mkoani Ruvuma na Nyasa vitongoji 94 vinakwenda kupelekewa umeme.