MAMIA WAJITOKEZA KAMBI YA MACHO BURE JIJINI TANGA.

*****

*Wampongeza Mbunge Ummy Mwalimu kwa kushawishi kambi hii kufanyika Tanga

Na Mwandishi wetu, Tanga

Mamia ya wakazi wa Jiji la Tanga leo tarehe 5/04/2025 wamejitokeza kwa wingi kupata huduma za matibabu ya macho katika Kambi ya Matibabu ya Macho bure inayoendeshwa na Taasisi ya Billal Muslim Mission of Tanzania. 

Wakiongea katika kambi hiyo Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mhe Ummy Mwalimu amewashukuru Billal Muslim Mission of Tanzania kwa kukubali ombi lake la kuja kutoa huduma za matibabu ya macho bure kwa wakazi wa Tanga na kusema watu wengi wanahitaji huduma hizi lakini wanashindwa kumudu gharama na hivyo baadhi yao wanaingia katika upofu usio wa lazima kwa kukosa huduma sahihi za afya ya macho kwa wakati.

Nae Mratibu wa Matibabu ya Macho wa Billal Muslim Mission of Tanzania Ain Sharifu amesema wao kama Taasisi ya Billal Muslim Mission wamejitolea kutoa huduma ya macho bure kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya ibada lakini pia kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha afya za wananchi hususani wa kipato cha chini. Ameeleza kuwa watu wote wataokao hitaji kupima macho watapimwa bure, watakaohitaji kupewa dawa za macho au miwani watapewa bure na wale watakaobainika kuhitaji kufanyiwa Upasuaji wa mtoto wa Jicho watafanyiwa Bure na Madaktari bingwa waliopo katika kambi hiyo.

Wananchi mbalimbali waliopata huduma za macho wamesema huduma zinazotolewa ni nzuri na wameishukuru Billal Muslim Mission kwa kuwapatia huduma za matibabu ya macho ikiwemo miwani bure. Aidha wamemshukuru Mbunge wa Tanga Mjini Mhe Ummy Mwalimu kwa kuwashawisha Taasisi ya Billal Muslim Mission kuja kutoa huduma hizi Tanga na wamemuomba Mwenyezi Mungu awabariki wote waliohusika na zoezi hili.

Kambi hii ya Matibabu ya Macho Bure itaendeshwa kwa muda wa siku 3 kuanzia leo tarehe 5 Aprili hadi tarehe 7 April 2025 chini ya Taasisi yq Billal Muslim Mission of Tanzania kwa kushirikiana na BETA Charitable Trust, Khoja Shia Ishna Asheri Charitable Eye Centre na kudhaminiwa na Mtandao wa YAS.













 

Related Posts