Dar es Salaam. Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha) kupitia chombo maalumu (caucus) kilichoundwa kutatua migogoro limeanza mchakato wa maridhiano kutibu majeraha yaliyotokana na uchaguzi ndani ya chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi inazo, chombo hicho Aprili 4, 2025 kilikutana na Mwenyekiti mstaafu, Freeman Mbowe, nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Haja ya kutibu majeraha iliwahi kuzungumzwa na Mbowe Januari 21, 2025 alipohutubia mkutano wa chama hicho baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho kutangazwa.
“Tumemaliza uchaguzi kwa kumshukuru Mungu kwa kupata viongozi, kitu ambacho tunapaswa kukisema, uchaguzi huu umeacha majeraha mengi ndani mwetu.
“Ushauri wangu kwa viongozi mnaoingia madarakani kakiponyeni chama chetu, niliahidi nikishinda ningeunda tume ya ukweli na upatanishi ili watu wakazungumze yaliyojiri kuelekea katika uchaguzi huu,” alisema.
Katikati ya jitihada hizo, ndani ya Chadema bado kuna fukuta, wanachama wanaounga mkono uongozi wa sasa na ule uliopita hawako sawa, huku ajenda ya ‘No reforms, no election’ ikionekana kuwagawa zaidi.
Lipo kundi linaloungana na viongozi kukubaliana na msimamo huo, lakini jingine linapinga likijenga hoja kadhaa, ikiwemo hofu ya kutofanikiwa kuzuia uchaguzi, athari kwa chama na wanachama ambao tayari walishajipanga kugombea.
Akizungumzia mchakato wa safari ya maridhiano Aprili 4, 2025, Mwenyekiti wa Bazecha, Suzan Lyimo amelieleza Mwananchi kwa kutambua hali inayoendelea ndani ya chama, baraza limeunda chombo maalumu (caucus) kwa ajili ya kutatua na kusuluhisha migogoro.
“Kimeanza (caucus) kazi rasmi jana (Alhamisi Aprili 3), kinaongea na viongozi wakubwa wawili kwa kuanzia, kwa maana ya Mbowe na Lissu (Tundu- Mwenyekiti wa sasa), kwa sababu tatizo la kutoelewana limetokana na uchaguzi.
“Kwa hiyo kuna kundi linaloona ajenda ya kuzuia uchaguzi haiwezekani na wanasema kwa nini haiwezekani sasa wakati ilianzishwa wakati wa Mbowe, katika hali ya kawaida unaona inawezekana walio upande wa Mbowe wanataka mabadiliko na uchaguzi uwepo,” amesema.
Kwa mujibu wa Lyimo, wawili hao hawakuwahi kukutana baada ya uchaguzi ndani ya chama, hivyo lengo la chombo hicho ni viongozi hao wakutane, wajadiliane kumaliza tofauti zilizopo.
Amesema ikiwezekana kuwakutanisha na kuwapatanisha, makundi yatatawanyika na kuungana kuwa kitu kimoja.
“Tunavyoongea hapa tayari imeshaongea na mmoja jana (Alhamisi Aprili 3) na wanaongea na mwingine leo (Aprili 4) kwa hiyo yanapotokea mambo kama haya kuna kitu kinaendelea,” alisema.
Ingawa Lyimo hakuweka wazi kiongozi waliyezungumza naye, Mwananchi limefahamishwa chombo hicho kimeshakutana na Mbowe Aprili 4 saa nne asubuhi nyumbani kwake Mikocheni.
Taarifa zinadai katika kikao kati ya Mbowe na jopo la chombo hicho likiongozwa na Lyimo na wazee wenye kuaminika ndani ya Chadema, kilichukua muda mrefu.
Wakati wa uchaguzi ndani ya chama hicho kulitolewa kauli zilizosababisha chuki na mgawanyiko miongoni mwa wanachama wa Chadema.
Kutokana na hilo, inatarajiwa viongozi hao watatoa dukuduku zao mbele ya chombo hicho ili kuweka mambo, hivyo kurejesha umoja na mshikamano ndani ya Chadema.
Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema -Zanzibar, Said Mohamed amesema njia pekee ya kurudisha utulivu ndani ya Chadema ni viongozi wa sasa wakutane na wanachama na viongozi wastaafu ili kutafakari mitazamo inayosababisha watofautiane.
Kwa mujibu wa Mohamed, tofauti iliyopo inasababishwa na kundi linalounga mkono ajenda ya ‘No reforms, no election’ na lile linaloipinga.
“Ni vyema uongozi ufanye juhudi za kukaa na wote hawa na kutafakari kwa pamoja,” amesema.
Amesema viongozi wasiende kwenye kikao na msimamo wao, badala yake watoe nafasi ya hoja kujadiliwa pande zote na upatikane mwafaka wenye masilahi kwa chama na wanachama.
Hata hivyo, amesema njia ya maridhiano inaweza kuwa bora zaidi katika kufanikisha mageuzi kama ilivyowahi kufanyika na matokeo yakapatikana.
Maridhiano anasema ndiyo sababu ya Chadema kuwa na ofisi ya makao makuu, yamerudisha ari ya ushiriki wa siasa za upinzani na hata waliokimbia wamerejea.
“Lakini, ukisema unazuia uchaguzi, sioni kama hiyo ni njia ya kufikia lengo, binafsi naona kuna umuhimu wa kukaa na kuzungumza tuondokane na mitazamo iliyopo na tuje na njia moja itakayotufikisha,” amesema.
Katika mazingira ambayo siasa ni historia, amesema ni vigumu kwa chama cha upinzani tena kimoja kutoka na msimamo kitazuia uchaguzi.
“Siasa ni historia, sasa lazima uangalie nani alifanikiwa kwa njia hii. Chama kimoja kinaposema kinataka kuzuia uchaguzi lazima ufikirie kitafanyaje, lakini muhimu ni kuja na mbinu mbadala,” amesema.
Mkurugenzi wa Fedha mstaafu wa chama hicho, Roderick Lutembeka amesema changamoto iliyopo ni tafsiri ya ajenda ya kuzuia uchaguzi na namna ya utekelezwaji wake.
Amesema hilo ndilo jukumu ambalo uongozi wa sasa unapaswa kuhakikisha unalitekeleza kwa wanachama hadi waelewe.
Kwa mtazamo wake, tayari limeshaanza kutekelezwa.
“Elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwa sababu ni muhimu ili wanachama waelewe namna ya uchaguzi utakavyozuiwa,” amesema.
Amesema migongano kuhusu ajenda hiyo imechanganyika na ‘songombingo’ za uchaguzi wa ndani uliopita na ndiyo sababu sintofahamu inaonekana kubwa.
Hali ilivyo amesema inaonekana kama kuna watu bado hawajapona vidonda, ndiyo maana wanaendeleza harakati za uchaguzi.
Amesema ni jukumu la viongozi wa chama kuendelea kukaa na makundi yote ambayo hayakuwa yamepona majeraha ya uchaguzi ili kuzungumza nayo na kuelewana.
Hata hivyo, amesema wanapokuwapo binadamu wenye akili timamu lazima kuwepo mgongano wa mawazo na fikra na hicho ndicho kinachoendelea Chadema.
Lutembeka aliyewahi kuwa Katibu wa Bazecha, amesema ajenda inayolalamikiwa sasa imepitishwa tangu uongozi uliopita na ilipitia vikao vyote stahiki.
Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Chadema, Azaveli Lwaitama amesema haoni kama ndani ya chama hicho kuna mgogoro wowote zaidi ya tatizo la uelewa na tafsiri.
Amesema kinachotajwa kuleta tofauti ni ajenda iliyopitishwa kwenye Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu, hivyo ni halali.
Amesisitiza hata kama kuna mwenye nia ya kugombea ana uhakika gani kama kilichotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa hakitamtokea naye pamoja na maandalizi aliyoyafanya.
“Hata kilichotokea Novemba mwaka jana, kuna ambaye ana uhakika na hakikisho kwamba haitamtokea kwa maana akaenguliwa au akashinda na asitangazwe. Kinachofanyika sasa tunatafuta suluhu ya yote hayo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Lissu ametengua uteuzi wa Catherine Ruge aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti na mtaalamu wa Dawati la Jinsia.
Ndani ya siku tatu wajumbe wawili wa sekretarieti uteuzi wao utenguliwa kwa nyakati tofauti na mamlaka tofauti za uteuzi wao.
Aprili 2, 2025 Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alitengua uteuzi wa Julius Mwita aliyekuwa Katibu wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chadema, akidaiwa kwenda kinyume cha msimamo wa chama hicho wa ‘No reforms, no election’ lakini mwenyewe alidai kuondolewa kwake ni chuki na visasi vya uchaguzi.
Ruge, katibu mkuu wa zamani wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), uteuzi wake umetenguliwa leo Jumamosi Aprili 5, 2025 na Lissu aliye ziarani mikoa ya Kusini.
Mwananchi limemtafuta Ruge ambaye amesema: “Ni kweli nimetenguliwa, lakini sijaambiwa sababu labda uulize mamlaka za uteuzi wao ndio watakuwa na sababu.”
Alipoulizwa iwapo amepewa barua ya uamuzi huo, Ruge amesema: “Nilishapewa barua ya kutenguliwa nafasi hii muda kidogo umepita.”
Kupitia akaunti yake ya X, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia ameandika: “Mwenyekiti wa chama (Tundu Lissu) leo Aprili 5, 2025 ametengua uteuzi wa mjumbe wa sekretarieti na mtaalamu wa dawati la jinsia @catherineruge.
“Operesheni ‘No reforms, no election’ inaendelea kuchanja mbuga kanda ya Kusini.”