UBALOZI WA TANZANIA UJERUMANI WAPONGEZWA

 

NA. MWANDISHI WETU BERLIN – UJERUMANI

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga (Mb) ameupongeza Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani uliopo jijini Berlin.

Mhe. Nderiananga ametoa pongezi hizo hii leo 04 Aprili, 2025 alipotembelea Ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Berlin, Ujerumani na kuzungumza na watumishi wa Ubalozi huo.

Akizungumza na watumishi hao baada ya kupokea taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya Ubalozi iliyotolewa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mhe. Hassan Mwamweta, Mhe. Nderiananga ameupongeza Ubalozi huo na watumishi wake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuiwakilisha nchi na kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa vitendo.

Mhe. Ummy amesema Watumishi walioko Ubalozini hapo, wanafanya kazi kubwa katika kutafuta fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuitangaza nchi ilikuvutia wafanyabiashara na wawekezaji waje nchini kuwekeza.

Mhe. Nderiananga amewasihi watumishi hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania na kuchapa kazi kwa moyo na kwa kuzingatia weledi.

“Kipekee nawapongeza kwa namna mnavyotekeleza majukumu yenu , mmekuwa vinara wa kutekeleza demokrasia ya uchumi kwa vitendo na hivyo kumuwakilisha Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kikamilifu, hakika kwa hili pokeeni maua yenu, pia nawasihi muendelee kufanya hivyo kwa maana kuwa mnaliwakilisha vyema Taifa letu ,” alisema Mhe. Ummy

Awali Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mhe. Hassan Mwamweta alieleza jinsi Ofisi za Ubalozi jijini Berlin zinavyotekeleza majukumu yake na kuongeza kuwa Ofisi hizo zinajukumu la msingi la kuhakikisha uhusiano kati ya Tanzania na Ujerumani unaimarika na kuleta tija kwa pande zote mbili.

“Tunashukuru kwa ziara hii Mhe. Naibu Waziri Ummy hii inaonesha namna Serikali inavyojali na inaendelea kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Nchi hizi, tuendelee Kuitangaza Tanzania hususani katika masuala ya uwekezaji na biashara na yale ya utalii” alieleza Mhe. Balozi Hassan.

Aidha amesema wataendelea kuchangamkia fursa zilizopo Ujerumani kwa tija ya Watanzania hasa zile za  kibiashara.

Related Posts