Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tanga, imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Waziri Amiri baada ya kumkuta na hatia ya kumuua mtoto wa mdogo wake, Athuman Mussa kwa kumkata na panga.
Tukio hilo lilitokea Februari 3, 2023 katika Kijiji cha Mziragembei, Kata ya Kwekanga wilayani Lushoto mkoani Tanga, ambapo marehemu alikuwa akijenga kibanda chake katika shamba lake la kurithi.
Ambapo mshtakiwa alitokea katika eneo hilo na kumuuliza kwa nini anajenga katika shamba hilo na kumtaka aache, marehemu alimjibu kuwa hawezi kuacha kujenga kibanda katika shamba hilo kwa sababu alirithi kutoka kwa wazazi wake.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa Waziri alichomoa panga lake na kumkata Athuman kichwani na kufuatia shambulio hilo alipiga yowe kuomba msaada wakati huo mshtakiwa akikimbia eneo la tukio.
Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 4, 2025 na Jaji Messe Chaba aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ambapo baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, alisema upande wa mashitaka umethibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka na kumuhukumu mshtakiwa adhabu hiyo ya kifo.
Ilielezwa kuwa baada ya Athumani kupiga yowe la kuomba msaada wananchi walifika na kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kwekanga, Ally Abdallah Seif (shahidi wa tano), ambaye alifika haraka katika eneo la tukio na kumkuta Athuman akiwa amelala karibu na kibanda chake akivuja damu.
Alisema alipomuuliza nini kimetokea alimtaja Waziri kuwa alimkata kwa panga kichwani, hali iliyolazimu shahidi huyo wa tano kutoa taarifa polisi kuhusu tukio hilo.
Ilielezwa kuwa muda mfupi baadaye dada wa Athumani, Amina Mussa (shahidi wa tatu) alifika eneo la tukio na kumkuta mdogo wake akiendelea kuvuja damu na katika jitihada za kumsaidia, alichukua kanga kwa ajili ya kuzuia damu iliyokuwa ikitoka kichwani.
Shahidi huyo alisema alipomuuliza nini kimempata, mdogo wake alimweleza amekatwa na baba yao mkubwa na baada ya hapo alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwa matibabu, lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia usiku.
Mshtakiwa aliyekimbia eneo hilo pamoja na makazi yake alikuja kukamatwa Desemba 8,2023, kupelekwa polisi kisha mahakamani aliposhtakiwa kwa kosa hilo la mauaji.
Katika kesi hiyo ya mauaji upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Thomas Gahigi, huku mshtakiwa huyo akiwakilishwa na wakili wa utetezi, Ahmed Makalo.
Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi watano, vielelezo vinne huku upande wa utetezi ukiwa na shahidi mmoja (mshtakiwa).
Shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka alikuwa Dk Keneth Macha, aliyesema akiwa katoka Hospitali ya Wilaya ya Lushoto, alimpokea na kumuhudumia Athuman aliyekuwa amepelekwa na askari polisi.
Shahidi huyo alisema Athuman alieleza kuwa alivamiwa shambani kwake na Waziri, aliyemkata kwa panga na kuwa alikuwa na maumivu makali, nguo zake zilikuwa zimelowa damu, na alikuwa akitokwa na damu nyingi kutokana na jeraha kichwani, ambapo baadaye alifariki dunia.
Alisema Februari 6, 2023 alipewa kazi ya kuchunguza mwili wa marehemu na kuhitimisha kwa mtazamo wa kimatibabu chanzo cha kifo ni kutokana na majeraha makubwa aliyopata kichwani yaliyosababisha kuvuja damu nyingi.
Shahidi wa tatu, ambaye ni dada wa marehemu alisema siku ya tukio saa saba mchana alipigiwa simu na shangazi yake aliyemtaja kwa jina moja la Amina, aliyemweleza Athuman amevamiwa na kujeruhiwa na kumtaka aende.
Alisema wakati simu hiyo ikipigwa, shangazi yake alikuwa akihudhuria mazishi katika Kijiji cha Mlalo, kufuatia kifo cha mama mkwe wake.
Alieleza kuwa alipofika eneo la tukio alimkuta mdogo wake akiwa na majeraha makubwa kichwani, huku akivuja damu nyingi na kuwa licha ya hali yake mbaya aliyomkuta nayo, alimweleza kuwa amejeruhiwa na mjomba wao ambaye kwa wakati huo alikimbilia kusikojulikana.
Alisema baada ya kuhakikisha kwamba mdogo wake kuwa chini ya uangalizi wa matibabu, alirudi nyumbani kutokana na hali yake ya ujauzito ila usiku baadaye alipigiwa simu kujulishwa Athuman amefariki dunia.
Shahidi huyo alisema mahakamani hapo kuwa Athuman na mshtakiwa walikuwa na mgogoro wa ardhi ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na marehemu baba yao ambaye baada ya kufariki dunia, walirithishwa kila mmoja alipewa eneo lake.
Alisema awali mshtakiwa aliwahi kumvamia Athuman kwa kutumia panga na kusababisha jeraha kwenye mkono wake wa kulia, hasa kwenye kiganja na kudai kuwa kabla ya tukio la Februari 3, 2023 mshtakiwa alikuwa akimuonya Athuman aache kutumia eneo hilo.
Shahidi wa tano, Ally Seif (Ofisa mtendaji wa Kata kwa wakati huo), alisema awali Januari 29, 2023, Athuman alienda ofisini kwake akimlalamikia kushambuliwa na Waziri kwa panga kutokana na mgogoro wa eneo hilo la urithi, na kumpatia barua aliyoenda nayo Kituo cha Polisi cha Miola kwa hatua zaidi za kisheria.
Alisema siku ya tukio, Februari 3, 2023 alipigiwa simu na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mziragembei na kupewa taarifa ya tukio la uvunjifu wa amani katika eneo la Kwemgambo kijijini hapo.
Alieleza kuwa alipofika alimkuta Athuman akiwa amelala chini kwenye dimbwi la damu huku akiwa na majeraha makubwa kichwani, hali yake ikiwa mbaya na alipomuuliza mhanga aliyemshambulia, Athuman kwa sauti ya unyonge alimtaja baba yake mkubwa.
Katika utetezi wake, Waziri alikana kuhusika na kosa hilo na akisema siku ya tukio saa nane mchana alichukua mbuzi wake mmoja na kwenda kuuza sokoni eneo la Kwa-Makame, ili kupata fedha za sare za shule za watoto wake.
Alisema alifika sokoni hapo saa 12 jioni na wakiwa pale kijana mmoja aitwaye Nzota alimjulisha kuwa Athuman amefariki dunia na kusema, baada ya kupata habari hizi, alirejea kijijini hadi katika eneo ambalo mwili wa marehemu ulipatikana, pamoja na maofisa wa polisi na wanakijiji wengine.
Alieleza maofisa wa polisi walikataa kuondoa mwili huo wakihoji nani alihusika na tukio hilo ila wote walijibu hawajui.
Mshtakiwa alikanusha kuwa na mgogoro na marehemu kuhusu eneo hilo na kuhoji kwa nini awe na mgogoro na marehemu, wakati familia hiyo ilikuwa na ndugu wengine saba.
Aidha alikanusha kusababisha madhara yoyote kwa Athuman, akisema amehusishwa na kifo cha marehemu kwa sababu Amina alimjulisha marehemu alikuwa na nia ya kuuza mali za nyumbani ikiwemo nyumba yake.
Mshtakiwa alisema alishiriki katika maziko ya marehemu na hata kutoa shuka yake ya Kimasai ili kuufunika mwili wakati wa ibada ya mazishi.
Baada ya maziko, alirudi nyumbani kwa wazazi wake, akamaliza kipindi cha maombolezo, na baada ya hapo akaendelea na shughuli zake za kila siku na kukiri kukamatwa Desemba 7, 2023.
Jaji Chaba amesema baada ya kuchambua kwa kina ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, suala la kuzingatiwa ni iwapo mshtakiwa anahusika na mauaji hayo.
Jaji huyo amesema katika kuamua kesi hiyo anaongozwa na kanuni za kisheria zilizowekwa vyema kuhusu upande wa mashitaka, kuwa na jukumu la kuthibitisha hatia ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote.
Amesema baada ya kutathmini kesi na ushahidi wa upande mashitaka kwa ujumla wake, hakuna shahidi aliyethibitisha moja kwa moja kumwona mshtakiwa akimsababishia kifo marehemu na badala yake, upande wa mashitaka unategemea tu ushahidi wa kimazingira kumuhusisha mshtakiwa na kifo cha marehemu.
“Kwa kuzingatia maelezo yaliyotangulia, na kwa kuzingatia uamuzi wa kimamlaka wa Mahakama ya Juu katika kesi ya Enock Kipela v. R, (supra), sina shaka kwamba, mshtakiwa alitenda kwa nia ya wazi na nia mbaya ya kumshambulia marehemu.”
Jaji Chaba amesema Mahakama imeridhika kuwa upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha mashaka kuwa Waziri alimuua Athuman, hivyo kumkuta na hatia ya mauaji kinyume na kifungu cha 196 na kumuhukumu kunyongwa hadi kufa.