Dakika 630 zaitenga Coastal na ushindi

KOCHA wa Coastal Union, Juma Mwambusi ana kazi kubwa ya kufanya katika mchezo wa kesho, Jumatatu dhidi ya Yanga kuhakikisha anapata ushindi, huku rekodi za mechi saba zilizopita zikiiweka katika mtego mkubwa.

Coastal Union ya Tanga itakuwa mgeni wa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Yanga inayoongoza msimamo wa ligi kwa pointi 61 huku ikifunga mabao 61 yakiwa mengi zaidi ya timu zote zinazoshiriki ligi hiyo, inakutana na Coastal Union ambayo katika mechi saba zilizopita za ligi sawa na dakika 630 imefunga bao moja pekee ikiwa imeruhusu nyavu zake zikitikiswe mara saba ukiwa ni wastani wa kuruhusu bao moja kila mechi.

Kitendo cha wastani wa kuruhusu bao kila mechi huku yenyewe ikiwa na ubutu eneo la ushambuliaji, ndicho kinampa wakati mgumu Mwambusi kuelekea mchezo dhidi ya Yanga ambayo mechi saba zilizopita imefunga mabao 25 ikiwa na wastani wa kufunga 3.6 kwa mechi ilhali ikiruhusu matatu pekee.

Kabla ya mchezo uliopita ambao Coastal ilifunga bao moja dhidi ya Kagera Sugar ikipoteza kwa 2-1 ugenini, timu hiyo ilikuwa haijatikisa nyavu za wapinzani wake katika mechi sita mfululizo. Mara ya mwisho kwa Coastal kufunga bao ilikuwa Februari 7, 2025 katika ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Tanzania.

Baada ya hapo, matokeo ya mechi zake yalikuwa dhidi ya Mashujaa 0-0 Coastal, Pamba Jiji 2-0 Coastal, Coastal 0-0 Azam, Namungo 0-0 Azam, Coastal 0-3 Simba na Dodoma Jiji 0-0 Coastal.

Mwambusi amekiri mchezo dhidi ya Yanga utakuwa mgumu kwani wanakwenda kucheza na timu ambayo inataka kutetea taji la ligi kwa mara nne mfululizo, lakini anaweka matumaini ya lolote linaweza kutokea ndani ya dakika 90.

“Tunaheshimu timu zote kwani kila mpinzani lazima tumkabili, kwa sasa malengo ni kubaki kwenye ligi,” alisema Mwambusi.

Kocha huyo ambaye pia amewahi kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Yanga, alisema licha ya safari ndefu waliyonayo kutoka Kagera ambako walicheza na Kagera Sugar wiki hii hadi Dar, lakini wanajipanga vyema kushindana na kupata matokeo mazuri.

“Namna gani sasa tutakwenda kujipanga katika mchezo ujao ni siri yetu lakini makosa na upungufu wote uliotufanya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar tutaufanyia kazi,” aliongeza kocha huyo.

Kwa sasa Coastal Union yenye pointi 25, imetofautiana pointi tisa na KenGold inayoburuza mkia na pointi 16. Pia timu hiyo imepishana pointi tatu na Kagera yenye 22 iliyopo kwenye mstari wa kucheza playoff kukwepa kushuka daraja ikibakiwa na mechi sita.

Msimu uliopita ilimaliza nafasi ya nne kwa pointi 43 na kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, lakini huu mambo yamekuwa magumu na imebidi kubadili malengo kutoka kumaliza nafasi za juu hadi kupambania kusalia kwenye ligi.

Timu hiyo imecheza mechi 24, ikishinda tano, sare 10 na kupoteza tisa, huku ikifunga mabao 19 na kuruhusu 25 matokeo ambayo yameiweka katika nafasi ya 10. Katika mechi sita zilizosalia kwa timu hiyo, itaanza dhidi ya Yanga.

Baada ya hapo, timu hiyo itaikaribisha Singida Black Stars na KenGold, kisha itaifuata Tanzania Prisons na kumalizia nyumbani dhidi ya Fountain Gate na Tabora United ambapo mechi zake za nyumbani zitapigwa Mkwakwani jijini Tanga baada ya uwanja huo kukamilika marekebisho yaliyokuwa yakifanyika kwa muda mrefu na kuilazimisha Coastal kutumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Arusha tangu kuanza kwa msimu huu.

Related Posts