KIUNGO wa Singida Black Stars, Mohamed Damaro,22, anaamini klabu yake ina nafasi kubwa ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, hasa Kombe la Shirikisho Afrika, endapo watamaliza nafasi ya pili au tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Kabla ya mechi yao dhidi ya Azam FC (iliyochezwa jana), Singida Black Stars ilikuwa nafasi ya nne na pointi 47 baada ya michezo 24.
“Matarajio yetu ni makubwa. Tunataka kuipeleka Singida Afrika. Tuna michezo michache tu iliyosalia na kila mmoja kwetu anaelewa uzito wake. Huu ni wakati wa kupambana zaidi ya kawaida,” alisema Damaro, ambaye alijiunga na Singida Black Stars Julai 27, 2024 akitokea Hafia FC ya Guinea.
Damaro ambaye ni kati ya wachezaji wa tatu wa Singida BS ambao wamebadili uraia, anasema nafasi hiyo si ndoto ya mbali, bali ni malengo yanayowezekana kutokana na aina ya kikosi walichonacho na kiwango bora walichokionyesha katika mechi nyingi msimu huu.
“Tumekuwa na msimu wa ushindani, lakini bado tunayo nafasi ya kuandika historia. Tuna timu yenye vipaji na morali ya hali ya juu,” aliongeza.
Mechi tano zilizosalia kwa Singida Black Stars ni dhidi ya Coastal Union (Aprili 10, ugenini), Tabora United (Aprili 19, nyumbani), Simba SC (Mei 14, ugenini), Dodoma Jiji (Mei 21, ugenini), na Tanzania Prisons (Mei 25, nyumbani).
Kulingana na Damaro, kila mchezo kati ya hiyo mitano ni kama fainali kwao.
“Tuna mechi tatu ugenini ambazo zote zitakuwa na ushindani mkali, hasa ile dhidi ya Simba. Lakini tukibeba pointi nyingi katika hizi mechi, nafasi ya kushiriki michuano ya CAF ni halisi kabisa,” alisema Damaro.
Singida ambayo imeonyesha ubora wa kushindana na vigogo kama Yanga, Azam na Simba, imejijengea jina kama moja ya timu zinazocheza soka la kisasa lenye nidhamu na mpangilio bora wa kiufundi na Damaro anajivunia kuwa sehemu ya kikosi hicho.
Msimu uliopita, Singida BS wakati huo ikiitwa Ihefu ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya saba na pointi 36 baada ya kushinda mechi tisa, sare tisa na kupoteza 12 ikiwa chini ya kocha mzawa, Meck Mexime.