Ruvuma. Ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi mkoani Ruvuma imetamatika, huku akisisitiza wananchi kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 pamoja na kuilinda amani ya nchi.
Mbali na hilo, amesema chama hicho kitaendelea kupambana usiku na mchana kuhakikisha inatatua changamoto za wananchi na kuwapelekea maendeleo ili kuchagiza ustawi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Dk Nchimbi alianza ziara yake Aprili 3, 2025 kwa kufanya mikutano ya hadhara na kukagua miradi ya maendeleo ya Serikali na ile ya CCM ambayo aliiweka jiwe la msingi la ufunguzi ama la ujenzi.
Leo Jumapili, Aprili 6, 2025, amehitimisha ziara hiyo kwa kuzungumza na wanachama na wananchi katika maeneo matatu tofauti. Mosi, amesimama eneo la
Liziboni akitokea Nyasa kwenda Songea Mjini.
Pili, Uwanja wa Majimaji kunapojengwa jengo la ghorofa lenye fremu 50 kisha akafungua fremu za chama hicho zilizopo eneo la Mshangano. Kote huko kulikuwa na wana CCM na wananchi waliokuwa wakimsubiri.
Maeneo yote yapo ndani ya Jimbo la Songea Mjini ambalo kati ya mwaka 2005 hadi 2015 yeye (Dk Nchimbi) alikuwa mbunge wao. Kwa sasa mbunge ni Dk Damas Ndumbaro ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria.
Ziara hiyo ya Dk Nchimbi ni ya ilikuwa ya kwanza tangu mkutano mkuu wa CCM uliofanyika Januari 18-19, 2025 ulipompitisha kuwa mgombea mwenza wa Urais. Ilikuwa ni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kupendekeza jina lake mbele wa wajumbe waliokuwa wamempitisha yeye (Samia) kuwa mgombea urais.
Katika siku hizo tano, amefanya mikutano ya hadhara Tunduru, Namtumbo, Nyansa. Amesalimia wananchi njiani maeneo mbalimbali. Amepokea wanachama wa upinzani hasa kutoka ACT-Wazalendoz Chadema na CUF kujiunga nao.

Kwenye mikutano ya leo Jumapili, Dk Nchimbi amesema amefikia mafanikio hayo baada ya wananchi wa Songea Mjini kumwanini kwani:”Nisingekuwa naibu waziri na au waziri kama siyo ninyi wana Songea. Tumshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan, amewaona wana Ruvuma, amewaona wana Songea, ameiona mikoa ya kusini, lakini yote ni ninyi wana Songea mlioanza kuniona.”
Huku akishangiliwa na wananchi akasema: “Na mimi nitaendelea kuwa mwakilishi wenu, nataka nikwambia mbunge atayekuwa hapa (Songea Mjini) mimi bwana nitakuwa mbunge mwenza wa jimbo hili, atake asitake.”
Ametumia fursa hiyo kusema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwani imeonesha uhai wa chama na kuwahakikishia uchaguzi wa madiwani, wabunge na urais utafanyika na kuwaomba wana Ruvuma kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
“Rais wetu ametupa heshima kubwa, sasa kumrudishia shukurani ni mkoa huo kuongoza za kura za urais,” amesema Dk Nchimbi huku akiwauliza kweli ama si kweli, wakamjibu ‘kweliiiiiiiii.’
Kuhusu maendeleo amesema, msingi wa sera za chama hicho ni kuhakikisha amani inakuwapo wakati wote na Serikali inawajibu wa kuilinda kwani amani ikivurugika maendeleo hayawezi kuwapo hivyo amewasihi wananchi kuilinda.

Wakati akizungumza hilo, moja ya kikundi kilichokuwa kikiburudisha kikaimba ubeti wa wimbo wao ‘Hatutaki fitina na watu wabaya, tunataka upendo na maendeleo.’ Dk Nchimbi akasema wimbo ni mzuri na anatamani ungekuwa unaimbwa hata nchi nzima kuwakataa wafitini na maendeleo yawe kipaumbele cha kwanza.
Katika mikutano hiyo, alikuwapo Chifu wa tano wa Kabila la Wangoni,
Imanuel Zulu ambaye amemshukuru Rais Samia kwa kuwaheshimisha huku akitumia fimbo ya asili aliyokuwa ameishika mkono wa kushoto akiizungusha akisema:”Mambo mazuri, hakuna tatizo lolote huko mbele.”
Msingi wa kauli hiyo ya Chifu Zulu ni baada ya Dk Nchimbi kuwaomba waendelee kuwaombea ili kufikia hatua hiyo ya kuwa Makamu wa Rais.
Chifu Zulu amesema wanachokisubiri ni wakati ukifika kampeni zianze na kijana wao (Dk Nchimbi) akamsaidie vyema Rais Samia kuhakikisha nchi inapiga hatua zaidi.
“Yaaani nina furaha sana, si mnaona nimevaa nini (anaonesha kifuani tisheti yenye picha ya Rais Samia akiwa amevaa kichifu), sasa mambo ni mazuri, asante sana Mama na Chifu mwenzangu,” amesema Chifu Zulu huku akishangiliwa hasa aliposema watizame kifuani kuna nini.
Mchungaji Msigwa, Kambaya
Katika ziara hiyo, Dk Nchimbi aliambatana na makada waliokuwa upinzani, Mchungaji Peter Msigwa na Abdul Kambaya. Msigwa alikuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa na Kambaya amewahi kuwa Mkurugenzi wa Habari wa CUF na kada wa Chadema.
Mchungaji Msigwa amesema tangu ameingia CCM, ameona baadhi ya mambo waliyokuwa wakiyasema (akiwa Chadema) hayana ukweli: “Kila sehemu ukienda miradi inaendelea. Hakuna sehemu hakuna mradi, hii yote ni kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi hivyo tuiunge mkono. Ukisema CCM haijafanya kitu nashangaa, najiuliza huyu ametembelea kweli nchi hii.”
“Wakija hapa wenzetu wale waulizeni wana sera ya kuwaleta maji, afya bora, miundombinu wawaoneshe, wanapiga piga maneno ambayo hayana ukweli wowote.
Tuna jemedari mahili kabisa Samia Suluhu Hassan ameonesha kwa vitendo. Mwana wa kuyumba (Dk Nchimbi) naye anakwenda kuunga naye kwa nini sasa tumwangushe. Tuwape kura za kutosha,” amesema Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini.
Naye Kambaya amewasihi wananchi wa Ruvuma kutokubali kudanganywa na wapinzani ambao amedai hawana lolote: “Mimi nilikuwa huko, nawajua vizuri, hawana kitu ni maneno tu. Nimekuja huku tuunganishe nguvu.”