Kauli ya atabadilika inavyowaponza wanandoa

Uhusiano wa kimapenzi, ni sehemu muhimu ya maisha ya kila mtu. Mara nyingi, watu wanatarajia kuwa na wenza wanaoendana nao katika mawazo, mitindo ya maisha na maadili.

Hata hivyo, wakati mwingine mtu anaweza kuingia katika uhusiano na mtu mwenye tabia mbaya, akiamini kuwa atakuwa na uwezo wa kumbadilisha au kumwongoza ili kuboresha tabia hizo. 

Kuna msemo,  tabia ni kama ngozi ya mwili huwezi kuibadilli. Kutozingatia mafunzo yanayotokana na msemo huu,  kumewaingiza baadhi ya watu  katika uhusiano au ndoa zenye chungu ya changamoto.

Hawa waliponzwa na imani 

 Samira Shabani,  mkazi wa Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam na mama wa watoto wawili,  anasema aliingia katika uhusiano na mwanaume ambaye alikuwa anapenda sana kumpiga.

“Kosa linaweza kuwa ni dogo tu la kueleweshana,  lakini yeye hawezi kufanya hivyo alikuwa ananipiga hadi wakati mwingine napoteza fahamu. Nilivumilia nikiamini pengine tutakapoingia kwenye ndoa, anaweza kubadilika na kuacha tabia hiyo lakini hali ilikuwa tofauti, “anasema.

Anasema hata walipoingia kwenye ndoa aliendelea na tabia hiyo ya kumpiga,  huku akisema hiyo ndiyo dawa ya mwanamke mjeuri.

“Tumeitwa mara kadhaa katika vikao na wazazi na hata viongozi wetu wa kiroho,  lakini akiwa pale anaonyesha kujutia na kuahidi kuacha tabia hiyo,  lakini zikipita siku kadhaa mambo ni yaleyale. Nikaona heri nusu shari kuliko shari kamili,  nilifuata taratibu zote za kuomba talaka na kuachana na ndoa hiyo, “anasema.

Naye Catherine Peter,  anasimulia kuwa walipokuwa katika uhusiano na aliyekuwa mpenzi wake,  mara kadhaa alikuwa akishuhudia ujumbe kutoka kwa  wapenzi wake wengine.

Anasema baada ya kuona hali hiyo ikizidi, alitaka kuvunja uhusiano huo lakini mwenza wake alisisitiza kuwa anampenda sana na hali hiyo inasababishwa na umbali unaokuwepo kati yao unaosabaishwa na kutokaa pamoja.

“Kutokana na sababu hiyo,  niliamini tutakapooana angeweza kuacha tabia yake ya kunisaliti na wanawake wengine, lakini cha ajabu hali ilizidi kuwa mbaya, ”anasema.

Anaendelea kusimulia kuwa miezi michache baada ya kuoana,  hali ilizidi kuwa mbaya hadi kufikia hatua ya kutorudi nyumbani kwa siku kadhaa.

“Alianza kwa kuchelewa kurudi nyumbani, baadaye akaanza kurudi asubuhi au kutorudi kabisa. Baada ya kufanya uchunguzi wangu nikabaini anakuwa kwa michepuko yake, ”anaeleza.

Anasema kuwa aliendelea kufanya jitihada kadhaa kumbadilisha hadi kufikia kushirikisha wazazi, lakini hazikufua dafu, hivyo  aliamua kudai talaka na kuachana naye.

Kwa upande wake,  John Jovin anasema alighairi kumuoa mpenzi wake kutokana na tabia yake isiyokoma ya kwenda kukopa katika taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo na kwenda kutunza katika sherehe za marafiki zake.

Anasema alimuonya mara kadhaa na kumsaidia kuyalipa madeni hayo lakini bado aliendelea na tabia hiyo.

Anasema tabia hiyo ilimfanya mpenzi wake huyo kuanza kuchukua baadhi ya vitu na samani za nyumbani na kwenda kuziuza,  ili aweze kupata fedha kwa ajili ya marejesho au kwenda kutunzana katika shughuli.

“Niliona atakuja kunisumbua baadaye na tabia hiyo,  kwani dalili ya mvua ni mawingu,  kwa tabia hiyo angenifanya nishindwe kupiga hatua kimaendeleo, “anasema.

Wanasaikolojia wanasemaje?

Mwanasaikolojia,  Modesta Kimonga anasema baadhi ya watu wanapoingia katika uhusiano huamini wanaweza kubadili zile tabia hasi ambazo wamezikuta kwa wenza wao.

Anasema baadhi yao huamini kuwa wakiingia kwenye ndoa, kupata watoto au kufikia hatua fulani ya kimaisha, wanaweza kubadilika kutoka katika tabia hizo ambazo wakati mwingine hazikubaliki hata mbele ya uso wa  jamii.

“Baadhi yao huamini wakiingia katika ndoa, kupata watoto kutamuongezea majukumu na kumfanya aweze kukua kifikra,  hivyo ataacha tabia zake ovu,”anasema.

Anaeleza imani hiyo imewafanya baadhi ya watu kuingia katika ndoa ambazo hazina furaha huku zikigubikwa na migogoro ya kila mara.

Anasema kiuhalisia ni vigumu kwa mtu kubadilisha tabia yake hasa ikiwa ulimkuta nayo wakati mnaingia katika uhusiano.

Anaeleza kuwa tabia ya mtu inaweza kubadilika kama yeye binafsi atadhamiria ndani ya moyo wake kubadilika 

“Kama mhusika unayetaka kumbadilisha,  mwenyewe hajaamua kufanya hivyo ni ngumu kubadilika, “anasema.

 Kimonga anasema baadhi ya watu huingia katika ndoa au uhusiano wa namna hiyo,  kutokana na uoga wa kutopata mwenza mwingine.

“Baadhi yao huendelea kuvumilia uhusiano na mtu asiye sahihi kutokana na hofu ya kuwa hawawezi kupata wenza wengine, au hofu ya kuanza upya maisha”anaeleza.

Anasema  sababu nyingine ni ushauri wa kuendelea kuvumilia wanaopewa na ndugu, jamaa na marafiki.

“Baadhi ya watu wanaopitia changamoto hiyo kwa namna moja au nyingine,  husababishwa na ushauri wanaopewa na ndugu jamaa au marafiki kuwa amvumilie atabadilika, na hivyo kuendelea kumpa matumaini kuwa siku moja atabadilika, ”anaeleza.

Mtaalam na mshauri wa masuala ya uhusiano, Eva Mrema anasema kuingia katika ndoa na mtu ambaye hauridhiki na tabia zake na ukiamini unaweza kumbadilisha,  ni kujiletea changamoto ikiwamo migogoro ya mara kwa mara.

Anasema wakati mmoja anafanya jitihada za kumbadililisha mwenzake anayetarajiwa kubadilika kama hajaamua yeye binafsi kubadilika,  anaweza kuchukulia kama usumbufu na hatimaye kuzalisha mifarakano na  hata ndoa kuvunjika.

 “Baadhi ya wenza huingia kwenye ndoa wakiwa na matumaini makubwa, lakini wanapogundua kuwa wenza wao hawawezi kubadilika, ndoa huishia kuvunjika, ”anaeleza.

Anaongeza kuwa migogoro hiyo katika familia huwaathiri kisaikolojia wao pamoja na watoto kama walijaaliwa kuwapata.

Anasema kuishi na mtu mwenye tabia ambazo hukubaliani nazo huku ukitarajia abadike mtakapooana,  inaweza kusababisha msongo wa mawazo hasa pale matarajio hayo yanapokwama.

 “Watoto waliozaliwa katika ndoa yenye msuguano mara nyingi hukua wakiwa na hisia za kutokuwa salama, jambo ambalo linaweza kuwaathiri katika maisha yao ya baadaye, ”anaeleza.

Related Posts