BAADA ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tabora United na kupaa hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro’ amesema mchezo ujao dhidi ya Fountain Gate ndiyo utakaowapa uelekeo kwenye michuano hiyo.
Pamba ilipata ushindi huo juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kufikisha pointi 26 baada ya michezo 25 na kupaa kutoka nafasi ya 13 na kesho, Aprili 8, itaikaribisha Fountain Gate kwenye uwanja huo mchezo wa raundi ya 26.
Minziro alisema malengo yalikuwa kuvuna pointi tisa katika michezo mitatu ya nyumbani dhidi ya Namungo, Tabora United na Fountain Gate, lakini hadi sasa wamevuna pointi nne, hivyo wanahitaji ushindi katika mchezo huo ili kufikisha pointi 29 na kujitoa kwenye presha ya kushuka daraja.
“Morali imeongezeka, naamini tutakapokutana na Fountain Gate keshokutwa, vijana wangu watakuwa katika ubora zaidi, leo (juzi) walikuwa na presha ya mechi kutokana na matokeo ya mechi iliyopita, lakini mchezo ujayo utakuwa mzuri zaidi kwa sababu tutakuwa tunatafuta kwenda kwenye pointi 29,” amesema Minziro.
Aliongeza; “Nadhani hapo ndiyo tutakuwa tumejihesabia tumetoka wapi tunakwenda wapi na je uelekeo wetu uko vipi kwenye Ligi Kuu. Tusubiri tuone mechi ya Fountain Gate, lolote linaweza kutokea na mechi itakuwa nzuri sana.”
Kocha huyo ambaye huo ni ushindi wake wa sita kwenye ligi, aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma huku akimmwagia sifa nyota wa mchezo huo, kiungo James Mwashinga ambaye pia alifunga bao pekee lililowapa ushindi dhidi ya Tabora United.
“Mwashinga (James) siku zote ni kama punda kwenye timu yetu, ni mchezaji ambaye anakimbia kuliko wachezaji wote uwanjani, sasa mtu kama yule unaweza kumtumia katika idara yoyote ile, uwepo wake, Samuel Antwi na Shassiri Nahimana pale katikati umechagiza ushindi wetu leo (juzi),” alisema Minziro.
Mwisho