Mkenya Fountain Gate hali tete

HALI ni mbaya kwa Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mkenya Roberto Matano baada ya juzi kupoteza kwa mabao 3-0, dhidi ya Mashujaa FC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma, ikiwa ni kichapo cha pili mfululizo katika Ligi Kuu Bara.

Kabla ya kichapo hicho, Fountain Gate ilichapwa idadi ya mabao kama hayo 3-0, dhidi ya Singida Black Stars, Aprili 2, na kuongeza presha kwa kocha huyo mzoefu raia wa Kenya, juu ya hatima yakekatika kikosi hicho kwa michezo mitano ijayo.

Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu hali ya timu hiyo, Matano alikiri kupitia kipindi kigumu kwa sasa, japo anahitaji muda kutengeneza balansi nzuri kuanzia eneo la kujilinda na kushambulia kwani ndilo linalomuangusha kikosini.

“Kwa bahati mbaya kwa sasa mimi ni mgonjwa na sikwenda Kigoma kwa ajili ya mchezo na Mashujaa FC, nadhani kuanzia (leo) nitasafiri kwenda jijini Mwanza kwenye mechi na Pamba Jiji, sijaishindwa hii timu, hivyo tutapambana zaidi,” alisema.

Mmoja wa viongozi wa timu hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, aliliambia Mwanaspoti hawafikiri kufanya maamuzi ya haraka ya kuachana na kocha huyo, ingawa wapo baadhi yao wanahitaji atimuliwe ili kunusuru mwenendo wa kikosi hicho.

“Tulifanya maamuzi ya haraka kumuondoa Mohamed Muya, tunahitaji umakini zaidi japo presha ni kubwa kwani pointi zetu zinaweza kufikiwa na timu nyingine na kutuweka katika hali mbaya ya kupigania kushuka daraja,” kilisema chanzo hicho.

Kocha huyo tangu ateuliwe Januari 10, mwaka huu akitokea Sofapaka ya kwao Kenya, amekiongoza kikosi hicho katika michezo tisa ya Ligi Kuu Bara, akishinda miwili, sare miwili huku akichapwa mitano.

Matano aliyechukua nafasi ya Mohamed Muya aliyetimuliwa Desemba 29, mwaka jana baada ya kikosi hicho kuchapwa mabao 5-0 na Yanga, katika michezo hiyo tisa aliyoiongoza, safu yake ya ushambuliaji imefunga mabao manne tu na kuruhusu 14.

Hadi Muya anaondoka aliiongoza katika michezo 16, ya Ligi Kuu, akishinda sita, sare miwili na kupoteza minane, ingawa kijumla imecheza 25, ikishinda minane tu, sare minne na kupoteza 13, ikiwa nafasi ya nane na pointi 28.

Kocha huyo anayefahamika kwa jina la utani la ‘Special One’, alijiunga na Sofapaka msimu huu baada ya mkataba wake na Tusker FC aliyoingoza kwa miaka sita kuanzia mwaka 2018 kumalizika, huku akitwaa ubingwa wa Kenya msimu wa 2021-2022.

Matano aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo za AFC Leopards na Ulinzi Stars, ameiongoza Sofapaka katika jumla ya michezo 15, ya Ligi ya Kenya, akishinda mitano, sare sita na kupoteza minne akiiacha nafasi ya saba na pointi 21.

Katika kipindi chake cha ukocha, amewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mara nne akifanya hivyo na Sofapaka FC mwaka 2009 ambayo ameshaachana nayo msimu huu na Tusker FC kuanzia msimu wa 2012, 2020-2021 na 2021-2022.

MICHEZO YA FOUNTAIN GATE ILIYOBAKI

Pamba Jiji v Fountain Gate (Aprili 8, 2025)

Fountain Gate v Yanga (Aprili 20, 2025)

JKT TZ v Fountain Gate (Mei 13, 2025)

Coastal Union v Fountain Gate (Mei 21, 2025)

Fountain Gate v Azam FC (Mei 25, 2025)

Related Posts