Rais Samia kuhutubia Bunge Angola

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kulihutubia Bunge la Angola ikiwamo kufanya mazungumzo na Rais  João Lourenço wa nchi hiyo.

Rais Samia ambaye anaanza ziara ya siku tatu nchini humo kuanzia Aprili 7 hadi Aprili 9, 2025, mbali na kulihutubia Bunge pia ataweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu wa muasisi wa taifa hilo, hayati Rais António Agostinho Neto pamoja na kutembelea kiwanda cha mafuta cha Luanda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 6, na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga ziara hiyo ni kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, João Lourenço.

“Rais Samia amealikwa na Spika wa Bunge la Angola, Carolina Cerqueira ambaye naye ni mwanamke, kuhutubia Bunge la nchi hiyo na atakuwa ni Rais wa kwanza mwanamke kutoka barani Afrika kuhutubia Bunge hilo.

“Ziara hii inalenga kukuza na kuimarisha zaidi mahusiano ya kihistoria na kidugu kati ya Tanzania na Angola,’ imesema taarifa hiyo.

Akiwa nchini humo, Rais atapata fursa ya kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Lourenço.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba uhusiano wa nchi hizo mbili uliasisiwa na waasisi ambao ni hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na hayati Rais António Agostinho Neto waliokuwa na maono ya pamoja ya kuikomboa Afrika na watu wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uhusiano huo umeendelea kuimarika siku hadi siku na sasa unajikita katika kukuza uchumi hasa katika sekta za biashara, uwekezaji, maendeleo ya miundombinu, mafuta na gesi, madini, uchumi wa buluu, afya, elimu na utalii kama zilivyoainishwa kwenye tume ya pamoja ya ushirikiano.

Aidha, ziara hiyo itashuhudia uwekaji saini wa hati za makubaliano (MOU) katika masuala yanayolenga kufungua fursa za biashara na uwekezaji na jitihada za kuimarisha ulinzi na usalama.

Ikumbukwe kwamba ziara hii inafanyika miaka 19 tangu marais wa Tanzania walipofanya ziara za kiserikali nchini humo, ambapo ya kwanza ilifanywa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere.

Kwa mujibu wa taarifa, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alifanya ziara nchini humo mwaka 2006, ambapo alihutubia Bunge la nchi hiyo akiwa Rais wa Tanzania na pia Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

 “Rais Samia atahitimisha ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha mafuta cha Luanda. Angola ni nchi ya pili barani Afrika kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta na uchumi wake unaendeshwa zaidi na mafuta.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye hifadhi kubwa ya gesi barani Afrika. Hii inatoa fursa kwa nchi hizi mbili kubadilishana uzoefu katika sekta ya mafuta na gesi pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wake,” imesema taarifa hiyo.

Related Posts