Rekodi hizi zinasubiriwa Championship 2024/25

WAKATI Ligi ya Championship ikibakisha raundi tano kwa kila timu, ushindani umekuwa mkubwa kuanzia kwa zinazowania kupanda Ligi Kuu Bara, kushuka daraja na nyingine zinazopigania kuhakikisha zinaendelea kusalia tena msimu ujao.

Licha ya kufikia hatua hiyo yenye ushindani na msisimko mkubwa, zipo rekodi mbalimbali za kuvutia zilizowekwa na hadi sasa bado hazijafikiwa, ingawa huenda ikatokea kwa michezo iliyobakia, kama ambavyo Mwanaspoti linazielezea kwa kina.

Mshambuliaji anayeongoza ni Andrew Simchimba wa Geita Gold mwenye mabao 17, akifuatiwa na nyota wa Mtibwa Sugar Raizin Hafidh aliyefunga 16, huku Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ anayeichezea TMA ya jijini Arusha akiwa amefunga 15, hadi sasa.

Licha ya kasi yao nzuri, ila rekodi inayosubiriwa kuvunjwa ni ya Edgar William ya msimu uliopita wa 2023-2024, wakati akiwa na kikosi cha KenGold alichokipandisha Ligi Kuu msimu huu, alikifungia mabao 21, ya Ligi ya Championship.

Nyota huyo anayeichezea Fountain Gate msimu huu, mabao hayo 21 aliyofunga, yanamfanya kushikilia rekodi ya mshambuliaji aliyefunga mengi zaidi katika Ligi ya Championship, kwani tangu msimu wa 2017-2018, hakuna aliyefunga idadi kama hiyo.

Msimu wa 2017-2018, mfungaji bora alikuwa ni Hassan Mwaterema anayeichezea Dodoma Jiji, japo wakati huo alikuwa na JKT Tanzania aliyoifungia mabao 16, kisha msimu wa 2018-2019, alikuwa ni Reliants Lusajo aliyefunga pia 16, akiwa na Namungo FC.

Anuary Jabir akafuatia msimu wa 2019-2020, akiwa na Dodoma Jiji na alifunga mabao 10, huku msimu wa 2020-2021, Edgar William alifunga 13, akiwa Mbeya Kwanza, huku 2021-2022, Edward Songo akatwaa tuzo baada ya kuifungia JKT Tanzania mabao 16.

Msimu uliofuatia wa 2022-2023, Songo akaitetea tena tuzo ya mfungaji bora akiwa na JKT Tanzania baada ya kuifunga mabao 18 na kuipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara, kisha 2023-2024, ndipo akaibuka Edgar William akiichezea KenGold alipoifungia 21.

Wakati Ligi Kuu Bara ikiwa haina kipa aliyefunga bao hadi sasa tangu msimu uliopita, katika Ligi ya Championship tayari imeshatokea kwa misimu miwili mfululizo, jambo linalosubiriwa kuona pia kama na msimu huu rekodi hiyo ya pekee itatokea.

Msimu wa 2023-2024, kipa wa zamani wa Biashara United, David Kissu Mapigano alifunga bao wakati timu hiyo iliposhinda kwa mabao 2-0, dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo uliopigwa Februari 15, 2024, kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Mara.

Bao lingine katika mchezo huo lilifungwa na Abeid Athuman likiwa ni la kwanza kwa nyota huyo akiwa na kikosi hicho tangu aliposajiliwa dirisha dogo la Januari 2024, baada ya kuachana na timu ya Geita Gold iliyokuwa inashiriki Ligi Kuu Bara.

Mbali na Mapigano anayeichezea Polisi Tanzania kwa sasa, huku akichezea pia timu za Gor Mahia ya Kenya, Simba, Azam FC, Namungo FC na KMC FC zote za Tanzania, kipa mwingine aliyewahi kufunga bao katika Ligi ya Championship ni Alain Ngeleka.

Ngeleka, raia wa DR Congo anayeichezea kwa sasa Dodoma Jiji, alifunga bao wakati huo akiwa na Kitayosce ambayo ni Tabora United, aliyeifungia timu hiyo licha ya kupoteza kwa mabao 3-1, dhidi ya JKT Tanzania, mechi iliyopigwa Desemba 3, 2022.

Ngeleka aliyesajiliwa na kikosi hicho akitokea Lumwana Radiant ya Zambia, alifunga bao hilo katika mzunguko wa 12, wakati timu hizo zikiwania nafasi ya kucheza Ligi Kuu Bara, mechi ikipigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni.

RKD 02

MALALE KURUDIA YA 2022-2023?

Moja ya kitendawili kinachosubiriwa ni kuona kama kocha mpya wa Mbeya City, Malale Hamsini ataipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara msimu ujao, baada ya kufanya hivyo msimu wa 2022-2023, wakati huo akiwa na kikosi cha maafande wa JKT Tanzania.

Malale anayepambana kukirejesha tena kikosi hicho Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, amekabidhiwa mikoba ya Salum Mayanga aliyejiunga na Mashujaa, huku timu hiyo ikiwa nafasi ya pili na pointi 55, nyuma ya Mtibwa Sugar yenye 60.

Kocha huyo ndiye aliyeipandisha JKT Tanzania msimu wa 2022-2023, baada ya kuongoza na pointi 63, akifuatiwa na Kitayosce ambayo kwa sasa ni Tabora United, zilizopanda pamoja Ligi Kuu, baada ya kushika nafasi ya pili na pointi zake 60.

Malale aliyetambulishwa rasmi kukiongoza kikosi hicho Machi 31, 2025, alikuwa hana timu yoyote aliyokuwa anaifundisha tangu mara ya mwisho alipoachana na maafande JKT Tanzania Juni 14, 2024, kutokana na mwenendo usioridhisha katika Ligi Kuu.

RKD 04
RKD 04

Msimu huu umekuwa mgumu ingawa hadi sasa zimefungwa ‘Hat-Trick’ nne, akianza mshambuliaji wa Mbeya City, Faraji Kilaza Mazoea, katika mchezo baina ya timu hiyo dhidi ya Maafande wa Polisi Tanzania, walioshinda mabao 4-0, Desemba 13, 2024.

Andrew Simchimba wa Geita Gold akafunga pia wakati timu hiyo iliposhinda mabao 4-0, dhidi ya Transit Camp, Februari 10, 2025, huku Oscar Tarimo wa Mbeya Kwanza akifunga pia katika ushindi wa 5-0, mbele ya Biashara United, Februari 23, 2025.

Nyota mwingine ni William Thobias wa Mbeya City aliyefunga pia wakati kikosi hicho kinachopambana kurejea tena Ligi Kuu Bara msimu ujao, kilipoichapa Kiluvya United mabao 4-0, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Machi 17, 2025.

Kwa msimu uliopita, zilifungwa ‘Hat-Trick’ tano huku nyota wa zamani wa Biashara United, Mganda Boban Zirintusa akifunga mbili, wakati Kika Salum (Pan Africans), Abdulaziz Shahame (TMA FC) na Oscar Mwajanga aliyekuwa Mbeya Kwanza wakifunga moja.

‘Hat-Trick’ hizo tano ni nyingi zaidi kufungwa kwa sababu hata msimu wa 2022-2023, zilifungwa tatu tu zilizofungwa na Mishamo Michael wa KenGold, Fabrice Ngoy aliyekuwa anaichezea Kitayosce kwa sasa Tabora United na Francis Ndala wa Copco FC.

RKD 03

Ushindi wa mabao 3-1, ilioupata Mtibwa Sugar dhidi ya TMA FC Machi 28, 2025, umeifanya timu hiyo kuweka rekodi ya kibabe kwani tangu msimu umeanza, haijawahi kupoteza au kutoka sare mchezo wowote iliocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Mtibwa iliyoshuka daraja msimu uliopita, imecheza michezo 13, kwenye Uwanja wa Manungu Complex kati ya 25 na kushinda yote, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga jumla ya mabao 34 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.

Katika michezo mitano iliyobakia, ni miwili tu itacheza kwenye Uwanja wa Manungu Complex, huku mitatu ikienda ugenini, ingawa swali linaloulizwa ni timu gani kati ya hizo zilizosalia itaenda kuivunja rekodi ya Mtibwa Sugar ikiwa nyumbani.

Michezo miwili ya nyumbani, ni dhidi ya Mbuni FC, Aprili 12, 2025 na mechi ya kwanza Mtibwa ilishinda kwa mabao 2-0, Novemba 30, 2024, huku nyingine ni Kiluvya United Mei 10, 2025, ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa bao 1-0, Januari 12, 2025.

Related Posts