TAASISI YA BILLAL MUSLIM YATOA HUDUMA YA MACHO BURE KWA MAMIA YA WANANCHI TANGA

*****

Na: Dk. Reubeni Lumbagala

Taasisi ya Billal Muslim Mission of Tanzania (BMMT) ni taasisi ya kidini yenye kusaidia watoto, familia, jamii zisizojiweza kwa kuwasaidia huduma mbalimbali kama vile elimu, afya na maji bila kujali dini, kabila, hadhi, au jinsi ya mtu. Kwa miaka mingi, Taasisi hii ya Billal Muslim Mission of Tanzania imegusa maisha ya wananchi wengi katika maeneo mbalimbali nchini, lakini miongoni mwa wanufaika wake ni mamia ya wananchi wa Jiji la Tanga na nje ya jiji hilo kufuatia uamuzi wao wa kuweka Kambi Maalum ya Kupima Macho Bure Jijini Tanga kwa mara ya pili kufuatia ombi la Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu.

Ni kwamba, macho ni kiungo muhimu katika mwili wa binadamu. Macho yakiwa salama, ni rahisi kushiriki katika shughuli za kimaendeleo kwa ufanisi mkubwa. Na ndiyo maana Wataalam wa afya wanatuasa kulinda na kutunza macho yetu na kuwa na utamaduni wa kuyapima mara kwa mara ili kama yatagundulika kuwa na tatizo basi yaanze kupata tiba mapema badala ya kusubiri tatizo liwe kubwa zaidi na mwishoe kushindikana kutibiwa.

Kutokana na ushawishi alionao Mbunge Ummy Mwalimu kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na namna anavyowajali wananchi wake, amekubaliana na wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuwa na utaratibu wa kuweka Kambi Maalum ya Kupima Macho Bure kwa wananchi mara kwa mara. Wadau ambao Ummy Mwalimu anashirikiana nao katika Kambi Maalum ya Kupima Macho Bure Jijini Tanga ni pamoja na Bilal Muslim Mission of Tanzania, Beta Charitable Trust UK na Mtandao wa Simu wa Yas.

Aprili 05 hadi 07, 2025 , Kambi Maalum ya Kupima Macho Bure imeendeshwa ambapo mamia ya wananchi wa Jiji la Tanga na wengine kutoka nje ya jiji hilo, wamejitokeza katika wingi katika viunga vya Shule ya Sekondari Usagara iliyoko jijini Tanga ambapo huduma mbalimbali za macho zimetolewa. Wananchi wamenufaika na huduma mbalimbali za afya ya macho zikiwemo huduma ya kupima macho na kupewa miwani bure, kupewa dawa za macho bure, ushauri wa afya ya macho na kusafishwa na kufanyiwa operesheni ya mtoto wa jicho. Ikumbukwe huduma hizi zote zimetolewa bure yaani bila malipo yeyote. Huu ni upendo mkubwa sana. 

Umati mkubwa wa wananchi umejitokeza kupata huduma mbalimbali za macho. Wengi wameshukuru huduma hizi kwani kama si kambi hii, basi wangepata huduma hili kwa gharama kubwa, jambo ambalo baadhi yao wasingemudu, hivyo kuweka macho yao katika hatari ya kupata upofu, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.

Hii si mara ya kwanza kwa Taasisi ya Billal Muslim Mission of Tanzania kuratibu zoezi hili maalum ya kupima macho bure jijini Tanga. Mwaka 2019, ilifanyika kambi kama hii ambapo wananchi zaidi ya 5,000 walihudumiwa, ambapo miongoni mwao wananchi 3,000 walipata miwani huku 400 wakifanyiwa operesheni ya mtoto wa jicho na wengine wakipata ushauri wa afya ya macho.

Kwahiyo, kambi ya mwaka huu ni mwendelezo wa Taasisi ya Billal Muslim Mission of Tanzania kukubali ombi la Mbunge Ummy Mwalimu kutoa huduma ya macho bure kwa wananchi wa Jiji la Tanga. Huduma hii imegusa maisha ya wananchi wengi na kutokana na kupata tiba ya macho, wanufaika wengi wa huduma hii sasa wataweza washiriki vyema katika shughuli zao za kila siku kwa maendeleo kutokana na afya ya macho yao kupata tiba.

Kwa hakika, Taasisi ya Billal Muslim Mission of Tanzania imetoa sadaka kubwa kwa wananchi wa Tanga kwa kurejesha tumaini katika macho yao kupitia huduma walizozipata tena bila malipo yeyote. Niwaombe waendelee na moyo huo wa kuwasaidia wahitaji.






 Maoni: 0620 800 462

Related Posts