TRA yawashukuru Wahariri kwa Kuhamasisha Ulipaji Kodi

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, amewashukuru viongozi na wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya TRA katika kuhamasisha umma kuhusu ulipaji wa kodi.

Akizungumza katika mkutano mkuu maalum wa siku mbili wa TEF uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Bombambili, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Kayombo amesema kuwa TRA inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wahariri na vyombo vya habari katika kufikisha ujumbe wa kodi kwa wananchi kwa lugha nyepesi na inayoeleweka.

Kayombo amesema, mafanikio ya kuvuka lengo la ukusanyaji wa kodi hayawezi kutenganishwa na kazi kubwa inayofanywa na wahariri na wanahabari kwa ujumla. “Sisi na ninyi tunajenga nyumba moja ya maendeleo, mnapotumia majukwaa yenu kuelimisha, kuhamasisha, na kuhimiza wananchi kudai risiti na kulipa kodi, mnafanya kazi ya kubwa na tunathamini mchango wenu”, amesema Kayombo.

Aidha, Kayombo amewapongeza viongozi wapya wa TEF waliochaguliwa ma kueleza kuwa uchaguzi huo umekua mfano bora wa demokrasia na weledi na kuufanya kuwa uchaguzi huru na wenye haki.

Naye Meneja wa TRA mkoa wa Ruvuma, Nikodemas Mwakilembe amewapongeza wahariri kwa uchaguzi huru na wenye kuzingatia misingi ya uchaguzi na utulivu wa hali ya juu na kuongeza kuwa uongozi huo unaimarisha imani ya wadau kwa TEF na kuchochea ushirikiano mzuri baina ya vyombo vya habari na taasisi za serikali kama TRA.

TRA imeahidi kuendeleza ushirikiano wake na wanahabari kwa lengo la kufanikisha elimu ya ulipaji kodi na kuongeza makusanyo ya mapato ya serikali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa TEF aliyechaguliwa Deodatus Balile ameipongeza TRA kwa kushirikiano wa wakati wote na kuahidi kuendelea kuwa daraja kati ya mamlaka na wananchi kwa kuwafikia walipakodi kupitia vyombo vya habari.

Mkutano Mkuu Maalum wa TEF ulifunguliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Emmanuel Nchimbi na kuhudhuriwa na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, na ulihusu masuala muhimu yanayogusa uhuru wa vyombo vya habari, maadili ya taaluma hiyo, na nafasi ya wahariri katika kuchochea maendeleo ya nchi kupitia uandishi wa habari za kuelimisha.

TRA imekuwa ikishirikiana na wahariri kwa njia mbalimbali ikiwemo warsha za pamoja, mafunzo ya uandishi wa habari za kodi, usambazaji wa taarifa kwa wakati, pamoja na kudhamini mikutano ya TEF kama huu wa Songea. Ushirikiano huu umelenga kujenga uelewa mpana wa masuala ya kodi miongoni mwa wanahabari ili waweze kutoa taarifa zenye weledi, usahihi, na ushawishi kwa jamii.
Mkurugenz wa elimu ya walipa kodi Richard Kayombo akiwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma Nicodem Mwakilembe wakizungumza katika mkutano mkuu wa Jukwaa la wahariri (TEF)
mara  baada ya uchaguzi wa Mwenyekiti. Mkutano huo umefanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Bombambili uliopo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma



Related Posts