Uhifadhi Ni Uti Wa Mgongo Wa Sekta Ya Utalii Nchini – Global Publishers



Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi imepongezwa kwa kazi kubwa inayoifanya ya kuandaa na kutoa askari wengi wanaofanya kazi kubwa kwenye maeneo yaliyohifadhiwa nchini yanayohusisha Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Maeneo ya Hifadhi za Wanyamapori za Jamii, na Misitu hivyo kufanya nchi kuwa na Uhifadhi endelevu ambao ni uti wa mgongo wa Sekta ya Utalii nchini.

Pongezi hizi zimetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akifunga mahafali ya 60 fungu la kwanza kwa udahili wa mwezi Machi katika mwaka wa masomo 2024/2025 ya wahitimu wa mafunzo ya Uaskari wa Uhifadhi wa Wanyamapori na Himasheria katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza.

Akizungumzia changamoto ya Ajira, Kitandula amewataka wahitimu kutumia fursa ya uwepo wa Kampuni ya Ulinzi ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi (PASCO) kuomba kujiunga nayo na kuweza kupangiwa vituo pale huduma inapohitajika kutoka kwa wadau mbalimbali wa uhifadhi. Aidha, amewataka wahitimu watakaopata nafasi za ajira PASCO kutumia fursa hiyo kujiongezea uzoefu na maarifa, na kutangaza jina la Taasisi kwa kuwa mabalozi wazuri.

Vilevile Kitandula alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau mbalimbali
wanaojishughulisha na shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na biashara ya utalii zikiwemo taasisi za serikali na sekta binafsi kuwaajiri na kuendelea kuwatumia vijana hawa ili kuongeza tija na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.

Katika hatua Nyingine Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi Prof. Agnes Sirima ameahidi kuwa watajikita katika kuhakikisha taasisi ya taaluma ya wanyamapori Pasiansi inatoa mafunzo bora katika sekta ya uhifadhi wa maliasili na uongozaji watalii.

Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi mwaka huu imefikisha miaka 59 toka kuanzishwa kwake mwaka 1966 kwasasa ipo katika maandalizi ya maadhimisho ya miaka 60 toka kuanzishwa.

 











Related Posts