Aliyeiua Simba Misri apata majanga

IMETHIBITISHWA kuwa, mshambuliaji wa Al Masry, John Ibuka, raia wa Nigeria ambaye alifunga bao la pili waliposhinda 2-0 dhidi ya Simba, atakosekana kwenye mechi ya marudiano jijini Dar keshokutwa Jumatano.

Al Masry ambao walianza safari ya kuja Dar alfajiri ya jana Jumapili baada ya juzi Jumamosi kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Ceramica Cleopatra FC katika Kombe la Ligi la Misri, wameifuata Simba kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya robo fainali kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Taarifa kutoka Misri zinabainisha kwamba Ibuka aliyetokea benchini na kufunga bao katika mchezo huo uliochezwa Jumatano iliyopita nchini Misri, amepata maumivu ya misuli ya paja, hivyo ataikosa Simba mechi ya marudiano.

“Mshambuliaji John Ibuka, ataukosa mchezo ujao wa mkondo wa pili wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Simba SC kwa sababu amepata maumivu ya misuli ya paja,” imeeleza taarifa hiyo kwa ufupi.

Katika mchezo huo, Ibuka aliingia dk78 kuchukua nafasi ya Salah Mohsen na kufunga bao dk89. Kabla ya hapo, Abderrahim Deghmoum aliitanguliza Al Masry kwa bao la dakika ya 16.

Kikosi cha wachezaji 24 ambacho Al Masry kinakuja kukabliana na Simba ni hiki; Fakhreddine Ben Youssef, Hassan Ali, Mohamed Hashem, Muhammad Shehata, Mahmoud Hamdi, Mahmoud Gad, Salah Mohsen, Youssef Al-Gohary, Papa Badji, Karim Bambo, Youssef El Gohary, Mohamed Makhlouf, Amr El Saadawy, Karim El Eraki, Baher El Mohamady, Abderrahim Deghmoum, Ahmed El Armouty, Pape Badji, Ahmed Eid, Mido Gaber, Mahmoud Hamada, Hussein Feisal, Listowel Amankona na Samadou Attidjikou.

Related Posts