Aliyewahi kuwa RPC Kilimanjaro afariki duniani

Moshi. Aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Absalom Mwakyoma amefariki dunia leo April 7, 2025 mkoani hapa baada ya kuugua ghafla.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa kifo hicho leo, April 7, 2025 akisema amefariki njiani akipelekwa Hospitali ya KCMC.

“Kifo chake kimetokea leo Aprili 7, 2025 saa 2 asubuhi akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya KCMC kutokea nyumbani kwake eneo la Shule ya Msingi JK Nyerere Manispaa ya Moshi baada ya kuugua ghafla,”amesema Kamanda Maigwa.

Maigwa amesema Mwakyoma ambaye aliwahi kuhudumu katika mikoa ya Pwani, Kilimanjaro, Mara na mikoa mingine, alistaafu Januari Mosi, 2013 akiwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara.

Pia, amesema mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kupelekwa kwao mkoani Mbeya baada ya kukamilika kwa taratibu za maziko.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya KCMC.

Endelea kufuatilia taarifa zaidi kupitia tovuti ya Mwananchi na mitandao yake ya kijamii.

Related Posts